Pele chanzo vita Messi, Ronaldo
Muktasari:
- Messi aliyekuwa bado kijana na Ronaldo walimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia, lakini gwiji wa Brazil, Pele alikosea na kumpa Ronaldo tuzo ya mshindi wa pili wakati wa hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Opera wa Zurich.
PARIS, UFARANSA: WAKATI nyota wa Brazil, Kaka alipotwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA mwaka 2007, kulikuwa na tukio la aibu lililotokea jukwaani ndilo lililokuja kusambaa sana mtandaoni na kutoa ishara ya kwanza ya ushindani mkubwa kati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Messi aliyekuwa bado kijana na Ronaldo walimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia, lakini gwiji wa Brazil, Pele alikosea na kumpa Ronaldo tuzo ya mshindi wa pili wakati wa hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Opera wa Zurich.
Rais wa FIFA wakati huo, Sepp Blatter, alilazimika kuingilia kati na kuwaomba wawili hao kubadilishana makombe, huku wote wakionekana kutofurahishwa na hali hiyo.
Kwa miaka 10 iliyofuata, Messi au Ronaldo walishinda kila tuzo kubwa ya Ballon d'Or na FIFA. Kwa hakika, tangu mwaka 2007, tuzo 20 kati ya 29 za Mchezaji Bora wa Ulaya zimeenda kwa mmoja wao.
Wakiwa wamefunga karibu mabao 2,000 kwa pamoja katika maisha yao ya soka, kushinda mataji 85 kwa vilabu na timu za taifa pamoja na kutwaa tuzo na kuvunja rekodi nyingi binafsi, Messi na Ronaldo watakumbukwa milele kama wawili kati ya wachezaji waliofanikiwa zaidi katika historia ya mchezo huo.
Ushindani wao umefafanua soka la miongo miwili iliyopita, ukivuka mipaka ya klabu, mataifa na mashindano mbalimbali, na kubadilisha namna soka linavyochezwa, kufuatiliwa na kujadiliwa duniani kote.
Mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na Argentina, Angel Di Maria, ambaye aliwahi kucheza na wote wawili, amesema katika filamu mpya ya BBC Sport Rivals: Messi v Ronaldo: “Wachezaji wawili kama wao, wakishindana katika kiwango hicho kwa miaka mingi, wakigombea Ballon d'Or na kufunga mabao mengi kiasi hicho... sidhani kama tutashuhudia jambo kama hilo tena.”
Wakiwa wamechochewa na tamaa ya kushinda mataji, kuvunja rekodi na kuwa bora zaidi, wawili hao, ambao huenda wanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya mwisho msimu huu, waliisukumana kila mmoja kufikia viwango vipya.
Ushindani wao unaenda mbali zaidi ya mjadala wa nani ndiye “mchezaji bora wa muda wote” (GOAT).
“Wote wawili walibadilisha soka,” amesema Di María.
Ukimuuliza mtu yeyote nani ni bora zaidi, ni vigumu kupata jibu la pamoja.
Aliyekuwa mchezaji mwenzake Ronaldo katika Manchester United, Rio Ferdinand, amesema:“Lazima awe Ronaldo.”
Lakini aliyekuwa mchezaji na kocha wa FC Barcelona, Xavi, anasisitiza:“Messi ndiye mchezaji bora kuwahi kutokea.”
Ronaldo mwenyewe aliwahi kusema mwaka 2012:
“Huwezi kulinganisha Ferrari na Porsche. Ni injini tofauti. Watu wengine wanasema mimi ni bora, wengine wanasema yeye ni bora. Wao ndio wataamua nani ni bora kwa wakati huo, na mimi nafikiri ni mimi.”
Takwimu zinasemaje? Ikiwa kipimo ni mabao au mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ronaldo anaongoza. Ikiwa ni Ballon d'Or au jumla ya mataji aliyoshinda, Messi anaonekana kuwa mbele kidogo.
Kwa baadhi ya watu, Ronaldo alitangulia mbele alipoiwezesha Ureno kushinda ubingwa wa Euro 2016. Hata hivyo, tangu hapo Messi ameiongoza Argentina kushinda mataji mawili ya Copa America na Kombe la Dunia.
Mchambuzi wa soka wa Hispania, Guillem Balague, amesema: “Kwangu, Messi ndiye mchezaji bora zaidi katika historia, na Cristiano ndiye mfungaji bora zaidi katika historia.”
Naye Deco, aliyewahi kucheza na Ronaldo katika timu ya taifa ya Ureno na Messi akiwa Barcelona, amesema: “Wao ni wa kipekee. Wako tofauti kabisa na wengine. Si jambo la kawaida kuwa katika kiwango hiki kwa miaka yote hiyo.
Kila mwaka kuna wachezaji wengi wanaofanya mambo makubwa kwa miaka michache, lakini kudumu karibu miaka 20 si jambo la kawaida.”
Labda uzuri wa mjadala wa GOAT ni kwamba huenda hautawahi kupewa jibu la mwisho, na pengine hauhitaji jibu hilo.
Mwandishi mwenza wa kitabu kuhusu Ronaldo na Messi, Jonathan Clegg, amesema:
“Wamefikia hatua ya kuthaminiana kama nyota wenza wa tamthilia ya soka ambayo wamekuwa sehemu yake kwa miaka 20 iliyopita.”
Wengi wanawaona kama watu wenye tabia zinazokinzana kabisa.
Messi ni mchezaji wa chenga za ustadi dhidi ya Ronaldo mwenye nguvu za mwili. Messi ni gwiji mtulivu dhidi ya Ronaldo anayejitangaza kwa kujiamini. Pep Guardiola na Barcelona dhidi ya Jose Mourinho na Real Madrid. Adidas dhidi ya Nike.
Lakini licha ya simulizi za tofauti zao, walikuwa na mambo mengi yanayofanana tangu utotoni.
Wote walikulia katika mazingira ya kawaida. Wote waliondoka nyumbani wakiwa wadogo ili kufuata ndoto zao, Messi alihamia Barcelona kutoka Argentina akiwa na miaka 13, huku Ronaldo akihamia Lisbon kutoka Madeira akiwa na miaka 12. Wote pia walikumbwa na huzuni ya kuwakosa familia zao.
Mwandishi wa Wall Street Journal, Joshua Robinson, amesema: “Messi na Ronaldo mara nyingi huonekana kuwa tofauti, lakini mambo yaliyowajenga utotoni yalifanana kwa kiwango kikubwa.”
Kilichowaunganisha zaidi ni hamu yao isiyotikisika ya kufanikiwa.
Xavi amesema:“Uliweza kuona mapema kwamba Messi alikuwa tofauti. Siyo tu kwa ubora wake bali kwa nguvu na ukali aliokuwa nao uwanjani. Cristiano hata alimpa msukumo wa kuwa mchezaji bora zaidi.”
Kwa upande mwingine nchini England, Ronaldo kijana alikuwa amejiunga na Manchester United akitokea Sporting.
Rene Meulensteen amesema: “Sijawahi kukutana na mchezaji kijana mwenye kujiamini kiasi hicho kuhusu kile alichotaka. Alipofika Manchester United, ilikuwa hatua ya kawaida kuelekea ndoto yake ya kuwa mchezaji bora duniani.”
Mwaka 2008, katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester United ilikutana na Barcelona. Ronaldo dhidi ya Messi kwa mara ya kwanza.
Balague amesema: “Messi alikuwa tayari bora katika La Liga na Cristiano alikuwa bora katika Premier League. Kuwaona vijana hao wawili pamoja uwanjani ilikuwa ishara ya jambo kubwa lililokuwa linakuja.”
Manchester United ilishinda taji hilo, Ronaldo akashinda Ballon d'Or, na ushindani wa kihistoria ukaanza rasmi.
Uhamisho wa Ronaldo wa pauni80 milioni kwenda Real Madrid mwaka 2009 ulimuweka moja kwa moja katikati ya ushindani mkali wa klabu kati ya Barcelona na Real Madrid.
Alipoondoka kwenda Juventus mwaka 2018, yeye na Messi walikuwa wamegawana Ballon d'Or tano kila mmoja. Katika misimu tisa waliyoitumia pamoja Hispania, Ronaldo alifunga mabao 450 katika mechi 438 kwa Real Madrid, huku Messi akifunga mabao 471 katika mechi 476 kwa Barcelona.
Lakini ushindani huo ulikuwa umevuka takwimu. Ulikuwa wa kibinafsi, na ukuaji wa mitandao ya kijamii ulifanya dunia nzima ishuhudie kila hatua yao.
Begiristain amesema: “Kwa Cristiano ilikuwa Lionel Messi, na kwa Lionel Messi ilikuwa Cristiano. Kila mmoja alihitaji kumshinda mwenzake.”
Mwandishi wa soka wa Hispania, Sid Lowe, aliongeza: “Ushindani wa Mourinho na Guardiola ulikuwa kama kioo cha ushindani wa Ronaldo na Messi.”
Messi na Barcelona walitawala zaidi La Liga, lakini Real Madrid na Ronaldo walitawala Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwaka 2012, Ronaldo aliiongoza Real Madrid kushinda La Liga yao ya kwanza ndani ya miaka minne, lakini Messi akachukua Ballon d'Or yake ya nne mfululizo, jambo lililomkera mpinzani wake. Messi aliendelea kushinda nne kati ya tano zilizofuata.
Robinson amesema:“Kulikuwa na uhasama wa kweli uliokuwa ukiongezeka. Hawakupenda kulinganishwa.”
Deco aliongeza:“Sidhani kama kuna kitu kinachofanana na kilichotokea kati ya Messi na Ronaldo, kwa sababu wakati huo Barcelona na Madrid zilikuwa katika kiwango sawa na zikigombea mataji makubwa.”
Mwaka 2017, Messi alifunga bao la ushindi dakika ya 92 dhidi ya Real Madrid na kuinua jezi yake mbele ya mashabiki. Miezi michache baadaye, Ronaldo aliiga shangwe hiyo baada ya kufunga katika Kombe la Super la Hispania dhidi ya Barcelona.
Balague amesema: “Kama ulihitaji ushahidi wa jinsi walivyotaka kushindana, picha hizo zinatosha.”
Ingawa ushindani wao wa moja kwa moja nchini Hispania ulimalizika Ronaldo alipojiunga na Juventus mwaka 2018, mjadala wa nani ni bora haukuisha.
Ronaldo alirejea Manchester United kabla ya kujiunga na Al-Nassr nchini Saudi Arabia, huku Messi akihamia Paris Saint-Germain kabla ya kusaini kwa Inter Miami CF nchini Marekani ambako bado anacheza.
Athari zao nje ya uwanja pia zilikuwa kubwa sana kibiashara.
Mtaalamu wa soka wa Italia, Mina Rzouki, amesema:“Hununuzi tu ubora wa michezo, unanunua uchumi mzima wa mtu mmoja.”
Mwaka 2018, Ronaldo alipouzwa Juventus, jezi 520,000 ziliuzwa ndani ya saa 24 za kwanza. Mwaka 2021, Messi alipojiunga PSG, jezi 150,000 ziliuzwa ndani ya dakika saba tu.
Kwenye Instagram, Ronaldo ana karibu wafuasi milioni 700 huku Messi akiwa na karibu milioni 500.
Kwa mapato, Ronaldo anaongoza. Kwa mujibu wa Forbes, amekuwa mwanamichezo anayelipwa zaidi duniani kwa miaka minne mfululizo akiwa na mapato ya dola300 milioni, huku Messi akiwa nafasi ya tatu kwa dola140 milioni.
Ushindani wao pia unaonekana katika mikataba ya vifaa vya michezo: Messi akiwa na Adidas na Ronaldo akiwa na Nike.
Joshua Robinson amesema:“Wamekuwa chapa kubwa za kimataifa, na jambo la kushangaza ni kwamba hawahitaji kusema mengi ili kuwa mabalozi wakubwa zaidi wa bidhaa duniani.”
Picha yao maarufu ya mwaka 2022 wakicheza chess juu ya sanduku la Louis Vuitton kabla ya Kombe la Dunia la Qatar ilivunja rekodi za mitandao ya kijamii.
Robinson alihitimisha: “Messi hana kitu kingine cha kushinda. Ana kitu kimoja ambacho Ronaldo hana, Kombe la Dunia. Sasa swali ni, je, Messi ndiye aliyeshinda zama hizi za soka?”
Hata hivyo, hadithi hii bado haijaisha. Ikiwa Argentina na Ureno zitakutana katika hatua za mwisho za Kombe la Dunia la mwaka huu, huenda sura ya mwisho ya ushindani huu bado haijaandikwa.