Fifa 'yauza' Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika mpango huo, Fifa imetangaza kuuza haki za kibiashara za mashindano yake ikiwemo Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi, hatua ambayo imeibua upinzani mkubwa kutoka mashirikisho ya soka wanachama duniani ikiwamo la Ulaya (UEFA), klabu kubwa za Ulaya na wanasiasa.
ZURICH, USWISI: SHIRIKISHO la Soka Duniani (Fifa) limeshutumiwa “kuuza roho ya soka” kutokana na mpango wa kupiga bei haki za kibiashara za Kombe la Dunia wenye thamani ya Dola 20 bilioni.
Katika mpango huo, Fifa imetangaza kuuza haki za kibiashara za mashindano yake ikiwemo Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi, hatua ambayo imeibua upinzani mkubwa kutoka mashirikisho ya soka wanachama duniani ikiwamo la Ulaya (UEFA), klabu kubwa za Ulaya na wanasiasa.
UEFA imetoa taarifa kali ikiituhumu Fifa kwa “kujaribu kuuza roho ya soka” na inaaminika kuwa inachunguza hatua za kisheria za kuchukua, huku vyanzo kutoka klabu kadhaa kubwa vikikosoa vikali mpango huo kwa faragha, ambapo Andy Burnham, Waziri Mkuu mpya wa Uingereza amepinga hatua hiyo.
Katika kuhakikisha kwamba mpango huo unafanyika Fifa imethibitisha kuwa inafanya kazi na benki moja ya Marekani, JP Morgan, kuanzisha taasisi mpya itakayojulikana kama Fifa Forward Enterprise (FFE) itakayokuwa na kazi ya kukusanya mamia ya mamilioni ya dola kwa kuuza sehemu kubwa ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia la wanaume na wanawake pamoja na Kombe la Dunia la Klabu kwa wawekezaji.
Fifa inaahidi kuwa zaidi ya Dola 10 bilioni zitakazopatikana baadaye zitasambazwa tena kwa vyama 211 wanachama.
Kampuni ya uwekezaji ya Thrive Capital, iliyoanzishwa na Joshua Kushner ambaye ni kaka wa Jared Kushner, mkwe wa rais wa Marekani, Donald Trump ndiyo inayoongoza mchakato wa kutafuta wawekezaji.
Hata hivyo, rais wa Fifa, Gianni Infantino, amesema mpango huo utaifanya sehemu ya biashara ya soka “kuendeshwa kama biashara maalumu yenye mwelekeo maalumu, huku thamani yake ikigawanywa kwa upana zaidi na kwa usawa duniani kote.”
Mpango huo unahitaji kuidhinishwa na idadi kubwa ya vyama wanachama vya Fifa, lakini Fifa imekataa kusema kura hiyo itafanyika lini.
Vyanzo vinavyofahamu mpango huo vinadai Fifa inauthamini mradi huo mpya wa kibiashara kwa takribani Dola 20 bilioni, huku Infantino akilenga kunufaika zaidi na ukuaji mkubwa wa umaarufu wa soka duniani baada ya Kombe la Dunia mwaka huu lililofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti mwezi huu kuwa mapato ya Fifa kutokana na mashindano hayo yangezidi Dola 15 bilioni, ongezeko kubwa kutoka makadirio ya awali ya Dola 13 bilioni, ongezeko linaloonekana kumpa Infantino ujasiri wa kutafuta mapato zaidi.
UEFA YAPINGA
Kutangazwa kwa mpango huo kumeibua upinzani mkubwa kutoka UEFA, ambayo imeishutumu Fifa kwa kujaribu kuuza roho ya mchezo huo.
Uhusiano kati ya taasisi hizo mbili zenye nguvu zaidi katika soka uko katika kiwango cha chini, UEFA ikidai kuwa Fifa iliharibu uadilifu wa Kombe la Dunia baada ya kuingilia suala la kadi nyekundu ya mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, baada ya Rais Donald Trump kumpigia simu Infantino na kuomba ibatilishwe.
UEFA kuhusu mpango wa FFE, ilisema: “Hii ni kuvuka mstari ambao taasisi zinazosimamia soka hazipaswi kamwe kuuvuka.”
Imeongeza kuwa, “UEFA inalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa. Ndivyo ambavyo kila chama cha soka kinapaswa kufanya. Ndivyo ambavyo kila mdau kwa maana ya ligi, klabu, wachezaji, mashabiki, serikali na kila anayejali mustakabali wa mchezo huu anapaswa kufanya. Roho na uongozi wa soka siyo mali za kuuzwa, hasa bila uwazi wowote kuhusu nani atanufaika kifedha. Hakuna kati yetu anayemiliki soka. Fifa haina haki ya kuliuza.”
Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Burnham, ambaye ni shabiki wa Everton, aliandika kwenye mitandao ya kijamii akisema: “Soka siyo mali ya wawekezaji. Ni mali ya watu wanaojaza viwanja na wale wanaosimama pembeni kila wiki, mvua iwe inanyesha au jua. Kombe la Dunia si bidhaa. Ni mashindano makubwa zaidi ya michezo duniani, na siyo ya mtu yeyote kuyauza. Unaweza kulipamba dili hili kwa namna yoyote unayotaka. Lakini ukishauza sehemu yake, umeshauza kila kitu.”
Inadaiwa kwamba Infantino alikuwa ameuficha mpango huo hadi taarifa zilipoanza kuibuka kupitia magazeti ya The Times na Financial Times ya Uingereza ikielezwa kwamba baadhi ya wajumbe wa Baraza la Fifa walishangazwa na tangazo hilo kwa sababu walitengwa katika mchakato wa kufanya uamuzi.
Hii ni mara ya pili kwa Infantino kujaribu kuvutia mitaji binafsi kusaidia miradi ya Fifa, ambapo 2018 alifikia makubaliano ya awali na benki ya Japan, SoftBank, kutoa ufadhili wa Dola 25 bilioni kwa ajili ya kupanua Kombe la Dunia la Klabu na kuanzisha Ligi ya Mataifa ya Kimataifa. Hata hivyo, mpango huo haukupata uungwaji mkono wa kutosha, hasa kutokana na upinzani kutoka Ulaya.
Kwa sasa UEFA na klabu kubwa za Ulaya zimeungana tena kupinga mpango wa Fifa, lakini Infantino anaweza kuwa na uungwaji mkono wa kutosha kutoka maeneo mengine duniani kupuuza upinzani huo.
Katika taarifa yake, Fifa imesisitiza kwamba FFE itawezesha kuongeza fedha zinazotolewa kwa kila chama mwanachama kutoka Dola 8 milioni hadi milioni 20 kwa mwaka, jambo ambalo litakuwa msaada mkubwa kwa nchi nyingi kati ya wanachama wake 211. Pia imesisitiza kuwa itaendelea kuwa na jukumu la kusimamia masuala ya uongozi wa soka na ratiba ya mechi za kimataifa.
Hata hivyo, wakosoaji wanaamini kuwa kuruhusu wawekezaji binafsi kuingia kwenye haki za kibiashara kunaweza kuleta shinikizo kubwa kutoka nje. Kuna hofu wawekezaji wanaweza baadaye kutaka kuwa na ushawishi kwenye uamuzi muhimu wa soka, kama kulifanya Kombe la Dunia kufanyika mara nyingi zaidi au kulipeleka katika masoko yenye faida kubwa zaidi ikiwamo Marekani.
Fifa kwa upande wake imesema itachagua kwa umakini wawekezaji wa muda mrefu watakaonunua sehemu ndogo zisizo na mamlaka ya kudhibiti FFE, na kwamba faida yote itakayopatikana itaelekezwa tena kwenye maendeleo ya soka duniani.
Licha ya mijadala mingi inayomzunguka, Infantino anatarajiwa kuchaguliwa tena bila upinzani kuwa rais wa Fifa mwaka ujao. Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Fifa atalazimika kuondoka madarakani 2031 baada ya kumaliza mihula mitatu kamili.