Ronaldo, Georgina kufunga ndoa Madeira
Muktasari:
- Harusi hiyo inatarajiwa kuanza saa 9:00 alasiri kwa saa za huko, huku mapokezi yakifanyika katika Hoteli ya kifahari ya nyota tano ya Savoy Palace, ambayo pia imeripotiwa kuhifadhiwa na wanandoa hao kwa wageni wao.
LISBON, URENO: NYOTA Cristiano Ronaldo anatarajiwa kufunga ndoa na mchumba wake, Georgina Rodriguez, katika kisiwa cha Madeira, alikozaliwa na kukulia.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya eneo hilo, wawili hao wamechagua kufunga pingu za maisha jijini Funchal, huku Kanisa Kuu la jiji hilo likiwa limehifadhiwa kwa ajili ya sherehe ya harusi itakayofanyika Jumamosi ijayo.
Harusi hiyo inatarajiwa kuanza saa 9:00 alasiri kwa saa za huko, huku mapokezi yakifanyika katika Hoteli ya kifahari ya nyota tano ya Savoy Palace, ambayo pia imeripotiwa kuhifadhiwa na wanandoa hao kwa wageni wao.
Chanzo kimoja kilisema wageni wa hoteli hiyo wamejulishwa kuwa ghorofa mbili hazitatumika Ijumaa na Jumamosi, pamoja na baadhi ya maeneo ya baa, kutokana na maandalizi ya sherehe hiyo kubwa.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41 na ambaye kwa sasa anakipiga katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia, alianza uhusiano na Georgina, mwenye asili ya Hispania na Argentina, mwaka 2016 kabla ya kumvisha pete ya uchumba Agosti mwaka jana.
Wiki iliyopita, wawili hao walionekana wakiwa wamevaa pete za almasi walipokuwa wakipanda boti ya kifahari katika kisiwa cha Majorca, jambo lililozidi kuchochea taarifa za harusi yao.
Awali Ronaldo aliweka wazi kuwa yeye na Georgina walipanga kufunga ndoa baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia, mashindano ambayo Ureno ilitolewa na Hispania, timu iliyokuja kutwaa ubingwa.
Akizungumza na mtangazaji Piers Morgan kabla ya mashindano hayo, Ronaldo amesema alikuwa na ndoto ya kufika siku ya harusi akiwa amebeba kombe la ubingwa wa dunia.
"Natumaini nitafika kwenye harusi yangu nikiwa na ubingwa," amesema Ronaldo.
Nyota huyo pia aliwahi kueleza kuwa Georgina ndiye mwanamke pekee aliyewahi kuwa naye katika uhusiano ambaye alitamani kuanzisha naye familia na kutumia maisha yake yote pamoja.
AITEKA SHOO
Mpenzi wa nyota wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo, Georgina Rodriguez, aliiba shoo kwa muonekano wake wa kuvutia alipohudhuria hafla ya kutunukiwa tuzo ya mshambuliaji huyo mjini Monaco.
Ronaldo alishiriki hafla ya upangaji wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo alikabidhiwa tuzo maalumu ya kutambua rekodi yake ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa michuano hiyo akiwa na mabao 140.
Baada ya hafla hiyo, Georgina aliandamana na Ronaldo kusherehekea mafanikio hayo na kuchapisha picha mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wakiwa ndani ya boti wakipiga picha na tuzo hiyo.
Ronaldo alionekana akiwa amevalia suti nyeusi pamoja na shati jeupe, huku Georgina akivutia wengi kwa gauni refu jeupe lililoendana na mkufu wa thamani.
Miongoni mwa picha alizoshiriki kwenye Instagram, kulikuwa na moja akiwa amelala kwenye ngazi za boti hiyo, huku nyingine ikimuonyesha Ronaldo akimbusu shavuni kwa ishara ya upendo.
Katika ujumbe wake, Georgina alimpongeza mpenzi wake kwa mafanikio hayo.
"Hongera kwa mfungaji bora zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, @cristiano. Unastahili kila kilicho bora duniani, mpenzi wangu. Tunakupenda," aliandika.
Chapisho hilo lilipokea maelfu ya maoni kutoka kwa mashabiki, wengi wao wakimsifu Georgina kwa muonekano wake wa kuvutia pamoja na namna alivyomuunga mkono Ronaldo.
Ronaldo na Georgina wamekuwa pamoja tangu mwaka 2016 na wamejijengea familia yenye watoto kadhaa.
Mwaka 2017 walipata binti yao wa kwanza pamoja, Alana Martina.
Mwaka 2022 walipata mapacha, lakini kwa masikitiko mtoto wa kiume alifariki dunia wakati wa kujifungua, huku mtoto wa kike, Bella Esmeralda, akinusurika.
Mbali na hao, Ronaldo pia ana watoto wengine watatu ambao ni Cristiano Jr pamoja na mapacha Eva na Mateo waliozaliwa kupitia uzazi wa kusaidiwa.