Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo, Messi ni vita ya fedha

VITA Pict

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa ripoti ya Bolavip, Ronaldo ameendelea kuwa kinara wa mapato baada ya kujiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia mwanzoni mwa mwaka 2023.

MADRID, HISPANIA: USHINDANI wa muda mrefu kati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo haujaishia uwanjani pekee, bali sasa umehamia pia katika vita ya fedha, huku mastaa hao wawili wakiendelea kuvunja rekodi za mapato tangu walipoondoka soka la Ulaya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Bolavip, Ronaldo ameendelea kuwa kinara wa mapato baada ya kujiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia mwanzoni mwa mwaka 2023.

Nyota huyo wa Ureno amekusanya takribani dola 675 milioni (Sh1.82 trilioni za Kitanzania) kupitia mshahara wake na bonasi mbalimbali alizopewa na klabu hiyo, kiwango kinachomfanya kuwa miongoni mwa wanamichezo wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani.

Kwa upande wa Messi, alipojiunga na Inter Miami ya Marekani mwaka 2023 alichagua mfumo tofauti wa malipo.

Mkataba wake unamhakikishia mshahara wa msingi wa dola 20.4 milioni kwa mwaka, huku mapato yake yote yakifikia kati ya dola milioni 50 hadi 60 kwa msimu. Tangu atue Marekani, nyota huyo wa Argentina anakadiriwa kuingiza kati ya dola 210 na 240 milioni (Messi amekusanya takribani Sh648 bilioni tangu ajiunge na Inter Miami mwaka 2023).

VIT 01

MESSI ANANUFAIKA ZAIDI NJE YA MSHAHARA

Licha ya pengo kubwa la mishahara, Messi hajabaki nyuma kwenye upande wa biashara.

Kwa mujibu wa Chama cha Wachezaji wa MLS (MLSPA), bado ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika historia ya ligi hiyo.

Hata hivyo, nguvu kubwa ya kifedha ya Messi ipo kwenye makubaliano ya kibiashara aliyoyafanya wakati akisajiliwa Inter Miami.

Mkataba wake unampa sehemu ya mapato yanayotokana na usajili mpya wa huduma ya Apple TV MLS Season Pass, sambamba na asilimia ya mauzo ya bidhaa rasmi za Adidas zinazobeba jina lake.

VIT 04

Mbali na hilo, ripoti mbalimbali za kifedha, ikiwemo za Forbes, zinaeleza kuwa Messi amepewa fursa ya kununua hisa za umiliki wa Inter Miami baada ya kustaafu soka, jambo linaloweza kuongeza utajiri wake kwa kiwango kikubwa kadri thamani ya klabu hiyo inavyozidi kupanda.

VIT 02

RONALDO AFAIDI MABILIONI YA SAUDI

Kwa upande wa Ronaldo, maisha yake ndani ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia yamekuwa ya kifahari zaidi kutokana na kiwango kikubwa cha fedha anacholipwa.

Taarifa za Capology zinaonyesha mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United hupokea karibu euro200 milioni kwa mwaka baada ya makato ya kodi.

Kiasi hicho kinamfanya kuwa mwanamichezo anayelipwa zaidi duniani, huku usajili wake ukiwa sehemu ya mkakati mkubwa wa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF) wa kuinua hadhi ya soka la nchi hiyo na kuvutia mastaa wengine duniani.

Mbali na mshahara, Ronaldo anaendelea kuvuna mamilioni kupitia biashara zake mbalimbali chini ya chapa ya CR7, inayojumuisha hoteli, vituo vya mazoezi, bidhaa za mavazi, manukato na miradi mingine ya kibiashara.

VIT 03

VITA MBILI, NJIA TOFAUTI

Takwimu hizo zinaonyesha Messi na Ronaldo wamechagua njia mbili tofauti za kujijengea utajiri katika hatua za mwisho za taaluma zao.

Ronaldo amechagua mfumo unaompa fedha nyingi moja kwa moja kupitia mkataba wake wa kucheza, wakati Messi ameelekeza nguvu kwenye ushirikiano wa kibiashara unaoweza kuendelea kumuingizia mabilioni hata baada ya kustaafu.

Ingawa Ronaldo anamzidi Messi kwa zaidi ya dola400 milioni (sawa na Sh1.08 trilioni) katika malipo ya moja kwa moja kutoka klabuni, ushindani wao unaendelea kuwa mkubwa ndani na nje ya uwanja.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, mastaa hao wamekuwa wakishindana kwa mabao, mataji na tuzo binafsi, na sasa wamehamisha pambano hilo kwenye eneo la biashara, wakithibitisha kuwa thamani ya majina yao imevuka mipaka ya soka na kuwafanya kuwa miongoni mwa wanamichezo wenye ushawishi mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani.