Fernandes: Man City? Wenyewe tuna shida kibao
Muktasari:
- Timu hizo mbili zitakutana uwanjani Etihad leo huku viwango vyao vya uwanjani vikiwa chini na Man City imepoteza mechi nane kati ya 10 za mwisho ilizocheza kwenye michuano yote.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes amesema timu yao ina matatizo mengi kuliko hata kufikiria kiwango cha sasa cha wapinzani wao Manchester City kwenye kipute cha Manchester Derby kitakachopigwa leo Jumapili.
Timu hizo mbili zitakutana uwanjani Etihad leo huku viwango vyao vya uwanjani vikiwa chini na Man City imepoteza mechi nane kati ya 10 za mwisho ilizocheza kwenye michuano yote.
Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kabla ya mechi za jana Jumamosi kilikuwa kinashika nafasi ya nne kwenye msimamo, pointi nane nyuma ya vinara Liverpool, wakati Man United ya Kocha Ruben Amorim yenyewe ilikuwa kwenye nafasi ya 13.
Lakini, nahodha wa Old Trafford, Bruno Fernandes alisema wachezaji wa Man United wanapaswa kufikiria kupandisha viwango vyao kwanza, kuliko kuanza kuifikiria Man City inayoshuka kiwango kwa sasa.
“Haiwezi kubadili chochote kwetu kwa hali yao ya sasa, kwa sababu sisi wenyewe tuna vingi vya kuvifanya,” alisema Fernandes.
“Sote tunafahamu hii ni mechi kubwa na wana wachezaji wakubwa, licha ya kwamba hawashinda kama ambavyo wamekuwa wakifanya, lakini lazima tujichunga sana wenyewe kwa sababu hatupo kwenye viwango tunavyovitaka. Yatupasa kujifikiria wenyewe kwanza viwango vyetu tufanye nini kuwa kwenye nafasi nzuri. Tunahitaji pointi kwenye ligi, hivyo haihusiani tunacheza na nani. Tunawajua hao ni Man City, hivyo itakuwa dabi kubwa.”
Chini ya Amorim, Man United imeshinda mechi tatu, imepoteza mbili na sare moja na Fernandes amewaambia wachezaji wenzake wanapaswa kupambana kwelikweli kusaka ushindi ndani ya uwanja ili wapande kwenye msimamo na hilo linapaswa kuanzia kwenye mechi yao dhidi ya Man City.
“Ni lazima tuanze kushinda mechi,” alisema Fernandes na kuongeza. “Hicho ndicho tunachopaswa kuboresha. Tunacheza na Man City na tunataka kushinda, iwe hivyo pia kwenye mechi nyingine.â€
Kwa kufunga mabao matano na asisti 10 msimu huu, Fernandes anaendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Man United, ubunifu wake ukihitajika.