Fernandes aigomea Man United
Muktasari:
- Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalianza majira ya kiangazi kufuatia msimu mzuri aliokuwa nao kiungo huyo Mreno, ambapo alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa England (PFA).
MANCHESTER, ENGLAND: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, amekataa kwa mara ya pili ofa ya mkataba mpya kutoka kwa mabosi wa klabu hiyo, hatua inayoweza kuongeza presha kwa kocha mpya anayetarajiwa kuiongoza timu hiyo, Mauricio Pochettino.
Fernandes, ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika Juni 2027, amegoma kusaini ofa ya pili licha ya Manchester United kuboresha masharti ya mkataba huo baada ya pendekezo la kwanza kutupiliwa mbali.
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalianza majira ya kiangazi kufuatia msimu mzuri aliokuwa nao kiungo huyo Mreno, ambapo alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa England (PFA).
Hata hivyo, sasa inaonekana suala la mshahara na muda wa mkataba mpya limekuwa kikwazo katika kufikia makubaliano.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, United bado ina matumaini ya kumbakiza nahodha huyo na huenda ikatumia kipengele cha kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa.
Lakini ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa, Fernandes ataruhusiwa kuanza mazungumzo na klabu za nje kuanzia dirisha la Januari 2027, huku uwezekano wa kuondoka mwishoni mwa msimu ukibaki wazi.
Hali hiyo inakuja wakati Manchester United ikipitia kipindi kigumu, ikitajwa kuwa katika nafasi za kushuka daraja baada ya kuanza vibaya msimu, huku mabadiliko ya benchi la ufundi yakizidi kutikisa klabu hiyo.
Fernandes pia amekuwa kwenye mvutano na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Michael Carrick, kufuatia kauli zake kali alizozitoa baada ya United kuchapwa vibaya na Como kwenye Ligi ya Mabingwa.
Katika mahojiano baada ya mchezo huo, nahodha huyo aliikosoa mbinu ya benchi la ufundi, akisema timu iliwapa wapinzani nafasi kubwa ya kumiliki mpira na kujenga mashambulizi.
Alisema mbinu ya kusubiri wapinzani badala ya kuwashambulia mapema ilisababisha wachezaji kuchoka kimwili na kiakili, hali iliyowafanya washindwe kutumia vizuri nafasi walizozipata.
Kauli hizo ziliibua mjadala mkubwa, huku gwiji wa United, Gary Neville, akimkosoa Fernandes na kumtaka ajue wakati na namna ya kutoa maoni yake.
Neville alisema kama nahodha anaweza kuzungumza hivyo hadharani, basi huenda hali ya ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo ilikuwa mbaya zaidi.
Kutokana na hali hiyo, Fernandes aliachwa benchi katika mchezo uliofuata dhidi ya Bournemouth, kabla ya kurejea kikosi cha kwanza dhidi ya Chelsea.
Hata hivyo, alikanusha madai kwamba kulikuwa na mazungumzo maalumu ya kusuluhisha tofauti zake na Carrick.
Alisisitiza kwamba kuachwa benchi kulitokana na kiwango chake kushuka na kwamba kocha alikuwa na haki ya kufanya maamuzi hayo.
Fernandes alisema bado ana imani na kocha, benchi la ufundi na wachezaji wenzake, akisisitiza lengo lake ni kushinda kila mchezo.
Licha ya msimamo huo, Carrick aliondolewa kwenye nafasi yake Alhamisi baada ya siku kadhaa za sintofahamu kuhusu mustakabali wake.
Uamuzi huo pia umeibua maswali kuhusu namna viongozi wa klabu hiyo, Omar Berrada na Jason Wilcox, walivyoshughulikia suala la kocha huyo.
Taarifa zinaeleza baadhi ya wafanyakazi wa klabu hiyo hawakufurahishwa na namna mchakato wa kumuondoa Carrick ulivyochukua muda mrefu.
Sasa macho yanaelekezwa kwa Pochettino, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa jukumu la kuijenga upya United, huku moja ya changamoto zake kubwa ikiwa ni kuhakikisha Fernandes anabaki Old Trafford.