Rasmi Man United imemtimua Carrick, Pochettino atajwa
Muktasari:
- Carrick, aliyewahi kuinoa Middlesbrough, alipewa mkataba wa miaka miwili baada ya kuiongoza United kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini ameshindwa kuendeleza mafanikio hayo katika kampeni za sasa.
MANCHESTER United imeamua kumtimua kocha wake mkuu, Michael Carrick, mwenye umri wa miaka 45, kufuatia mwanzo mbaya wa msimu uliosababisha timu hiyo kutumbukia katika eneo la hatari la kushuka daraja Ligi Kuu England.
Carrick, aliyewahi kuinoa Middlesbrough, alipewa mkataba wa miaka miwili baada ya kuiongoza United kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini ameshindwa kuendeleza mafanikio hayo katika kampeni za sasa.
United imekuwa na mwenendo mbaya, ikikumbwa na matokeo ya aibu yakiwamo kichapo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Bournemouth, kufungwa 4-1 na Como katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kupoteza 2-0 dhidi ya Hull City katika mchezo wa ufunguzi wa msimu.
Kutokana na mwenendo huo, viongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na mmiliki mwenza Sir Jim Ratcliffe wameamua kuchukua hatua ya kumuondoa kocha huyo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao cha viongozi wa klabu kilichofanyika Monaco, kilichohusisha pia mtendaji mkuu Omar Berrada na mkurugenzi wa ufundi Jason Wilcox, ambapo walijadili hatma ya Carrick.
Mchezo wake wa mwisho akiwa kwenye benchi la ufundi ulikuwa Jumapili iliyopita, United ilipolazimishwa sare ya mabao 4-4 na Aston Villa, matokeo yaliyoiacha timu hiyo ikiwa ndani ya eneo la kushuka daraja.
Wakati huohuo, aliyekuwa kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, ametajwa kuwa chaguo la kwanza kuchukua nafasi ya Carrick, huku kocha huyo raia wa Argentina akionyesha nia ya kutua Old Trafford.
Taarifa zinaeleza kuwa United ilikuwa imefikia makubaliano ya awali ya mdomo na Pochettino, ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya taifa ya Marekani, kabla ya kuchukua uamuzi wa kumtimua Carrick.
Hata hivyo, kuchelewa kwa klabu hiyo kufanya uamuzi kuhusu Carrick kunaweza kuilazimisha kumteua kocha wa muda kwa ajili ya mchezo dhidi ya Liverpool, Novemba 22.
United pia inakabiliwa na changamoto ya muda katika kukamilisha ujio wa Pochettino iwapo itaamua kumteua, kwani kwa sasa kocha huyo yuko katika maandalizi ya michezo ya Ligi ya Mataifa ya CONCACAF akiwa na Marekani dhidi ya Haiti.
Wakati wa utawala wake, Carrick pia alikumbana na mvutano na nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes, ambaye aliikosoa mbinu yake ya uchezaji baada ya United kufungwa mabao 4-1 na Como.
Akizungumza na TNT Sports, Fernandes alisema benchi la ufundi liliamua kutowataka wachezaji kukaba wapinzani mmoja mmoja, badala yake kusubiri wapinzani wafanye mashambulizi huku wakiacha nafasi nyuma.
“Ni uamuzi wa benchi la ufundi kutotaka tukabe kila mchezaji mmoja mmoja na wakati mwingine kuacha nafasi nyuma, tukisubiri wapinzani ili kupata mpira.
“Lakini unapozipa timu hizo nafasi ya kucheza, zinapata ujasiri,” alisema Fernandes.
Alipoulizwa kama Carrick alikosea mbinu katika mchezo huo, Fernandes alisema hilo lilikuwa jukumu la kocha na benchi lake la ufundi kulitathmini, akisisitiza kuwa wakati mwingine timu inapaswa kuwa jasiri zaidi inapokuwa chini ya presha kwa kusukuma mashambulizi na kuwafanya wapinzani wakose utulivu.
Naye beki Lisandro Martinez aliongeza mvutano ndani ya klabu hiyo baada ya kumkosoa mkurugenzi wa soka Jason Wilcox, katika kauli kali iliyotolewa kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya.