Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maajabu ya dakika za nyongeza Old Trafford

MAAJABU Pict

Muktasari:

  • Kwa sasa, United haionekani kuwa na kikosi chenye mfumo wa kueleweka wa kucheza soka, bali kundi la wachezaji wanaoonekana kutegemea nguvu, kasi na msisimko wa ghafla kuliko mbinu na nidhamu ya mchezo.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inaendelea kuonyesha sura ya timu iliyopoteza mwelekeo, huku kiwango cha wachezaji wake kikizua maswali mengi kuhusu uwezo wa benchi la ufundi na mustakabali wa kocha Michael Carrick.

Kwa sasa, United haionekani kuwa na kikosi chenye mfumo wa kueleweka wa kucheza soka, bali kundi la wachezaji wanaoonekana kutegemea nguvu, kasi na msisimko wa ghafla kuliko mbinu na nidhamu ya mchezo.

Ukweli ni kwamba, kwa sehemu kubwa, Manchester United imekuwa timu isiyo na mpangilio, inayocheza soka lisilo na ubunifu, akili wala ubora unaotakiwa kwa klabu yenye historia kubwa kama hiyo.

Kinachoshangaza zaidi ni namna mashabiki wake wanavyoendelea kushangilia timu hiyo licha ya mapungufu yanayoonekana wazi uwanjani.

Katika mchezo mwingine wa kusisimua kwenye Uwanja wa Old Trafford, United ililazimika kupambana kutoka nyuma mara mbili baada ya kujikuta ikifungwa mabao mawili ndani ya dakika nne za mwanzo na baadaye kuwa nyuma kwa mabao 4-2 dakika ya 53.

Hata hivyo, kwa namna ya kushangaza, vijana hao wa Carrick walifanikiwa kurejea na kulazimisha sare ya mabao 4-4, wakifunga mabao mawili katika muda wa nyongeza.

Matokeo hayo yaliwafanya mashabiki wa United kushangilia kwa nguvu na kuimba jina la Carrick, huku wachezaji wakifanya mzunguko wa kuzunguka uwanja kuwashukuru mashabiki.

Lakini nyuma ya shangwe hizo kuna ukweli mchungu: Manchester United bado ni timu yenye matatizo makubwa ya kiuchezaji.


MAAJAB 01

YATEGEMEA MIUJIZA

Kwa sasa, United inaonekana kupata nguvu pale inapokuwa kwenye mazingira ya kulazimika kupambana kuokoa heshima yake.

Timu hiyo ilifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Roma kwenye Ligi ya Mabingwa wiki iliyopita na sasa imejirudia dhidi ya Aston Villa.

Hata hivyo, aina hiyo ya uchezaji haiwezi kuwa suluhisho la kudumu kwa timu inayotakiwa kupambana na wapinzani wakubwa katika Ligi Kuu England.

Mabao ya dakika za mwisho yanaweza kuleta furaha kwa mashabiki, lakini hayawezi kuficha mapungufu ya kiufundi yanayoendelea kuigharimu timu hiyo.


MAAJAB 02

DALOT AIBUA HASIRA

Beki wa pembeni, Diogo Dalot, alikuwa miongoni mwa wachezaji walioonekana kuwa na mchango mkubwa katika matatizo ya United kwenye mchezo huo.

Dalot alihusika katika bao la kwanza la Aston Villa baada ya kushindwa kuzuia shuti la Mbrazil Alysson, ambaye alitumia udhaifu wa beki huyo kuifungia timu yake.

Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Dalot kusababisha penalti kipindi cha pili, kitendo kilichowafanya mashabiki wa United kumzomea alipokuwa akitoka uwanjani.

Kwa mchezaji ambaye tayari ameichezea United zaidi ya mechi 250, kiwango hicho kimeibua maswali kuhusu ubora wake na uwezo wake wa kuendelea kupewa nafasi katika kikosi hicho.

Kipa Senne Lammens naye alihusika katika bao la pili baada ya kushindwa kuzuia vizuri shuti la Alysson na kuacha mpira ukimfikia Nicolas Jackson aliyefunga kirahisi.


MAAJAB 04

BRUNO AIPA TUMAINI UNITED

United ilianza kurejea mchezoni baada ya Boubacar Kamara kufanya faulo ndani ya eneo la hatari dhidi ya Matheus Cunha dakika ya 13.

Nahodha Bruno Fernandes alisimama na kutekeleza penalti hiyo kwa utulivu na kuipa timu yake bao la kwanza.

Baada ya bao hilo, United ilionekana kupata uhai mpya, huku safu yake ya ushambuliaji ikianza kuwapa wakati mgumu mabeki wa Aston Villa. Cunha, Fernandes, Kobbie Mainoo na Amad Diallo walipata nafasi kadhaa, lakini hawakuweza kuzitumia ipasavyo.

Baadaye Amad alitengeneza nafasi nzuri iliyomfikia Youri Tielemans, ambaye alifunga bao lake la kwanza akiwa na United kwa shuti la umbali wa takribani mita 18.

Bao hilo liliifanya United kusawazisha na kuonekana kurejea kwenye mchezo.

Hata hivyo, furaha yao haikudumu kwa muda mrefu.


MAAJAB 03

VILLA YAWAADHIBU TENA

Dakika ya 47, Dalot alifanya faulo ndani ya eneo la hatari dhidi ya Alysson na kuisababishia United penalti.

John McGinn hakufanya makosa, akafunga kwa ustadi na kuirudisha Aston Villa mbele kwa mabao 3-2.

Dakika ya 53, United ilipata pigo jingine baada ya Leny Yoro kufanya kosa la kujifunga kwa kichwa, akielekeza mpira langoni kwake.

Lammens aliokoa kwa kugusa mpira uliogonga mwamba wa juu wa lango, lakini Leon Goretzka aliuwahi na kuusukuma wavuni na kuifanya Villa kuongoza kwa mabao 4-2.

Hilo lilikuwa bao la 16 kufungwa na United katika michezo yake mitano iliyopita, takwimu zinazoonyesha ukubwa wa matatizo ya safu yake ya ulinzi.


MAAJAB 06

MABAO YA MWISHO

United ilionekana kuwa katika wakati mgumu, huku Aston Villa ikianza kudhibiti mchezo na kuelekea kupata ushindi.

Lakini dakika ya pili ya muda wa nyongeza, Patrick Dorgu alitoa krosi iliyomkuta Joshua Zirkzee, ambaye alifunga bao la kupunguza pengo na kuifanya United kurejea kwenye mchezo kwa mara nyingine.

Dakika ya 96, Dorgu akawa shujaa mwingine wa usiku huo baada ya kufunga bao la kusawazisha kupitia mpira wa kona na kuifanya Old Trafford kulipuka kwa shangwe.

Aston Villa ililalamikia tukio la kipa wake Zion Suzuki kuguswa na Lammens katika harakati za kuwania mpira kabla ya bao hilo, lakini mwamuzi wa VAR hakubatilisha bao hilo.

Mwisho wa mchezo, United ilipata pointi moja ambayo kwa namna ilivyokuwa imecheza, inaweza kuonekana kama ushindi.


MAAJAB 05

CARRICK AOKOLEWA

Pamoja na sare hiyo, Carrick bado anakabiliwa na maswali mazito kuhusu uwezo wake wa kuiongoza United kurejea kwenye kiwango kinachotarajiwa.

Cha kushangaza ni kwamba, kwa sasa lawama nyingi hazielekezwi kwake, hali inayoonyesha namna klabu hiyo ilivyo katika mkanganyiko wa kutafuta chanzo cha matatizo yake.

Wakati viongozi wa klabu akiwamo Jim Ratcliffe, Jason Wilcox na Omar Berrada wakiendelea kukabiliwa na presha, baadhi ya mashabiki walionyesha kutoridhishwa kwao kupitia mabango yaliyokuwa uwanjani.

United inaweza kujivunia namna ilivyookoa pointi dhidi ya Aston Villa, lakini sare hiyo haiondoi ukweli kwamba timu hiyo bado ina mapungufu makubwa katika ulinzi, nidhamu ya mchezo na mfumo wa uchezaji.

Kwa kifupi, Manchester United imeonyesha uwezo wa kupambana hadi dakika ya mwisho, lakini kupambana pekee hakutoshi kujenga timu imara.