Fenerbahce yakana tetesi za kumtaka Gittens
Muktasari:
- Klabu hiyo ya Ligi Kuu Uturuki imetoa taarifa rasmi ikisema haina nia ya kumsajili Gittens, huku ikizitaja taarifa zinazoendelea kusambaa kuwa “hazina msingi” na ni “majaribio ya kuendesha klabu kwa maslahi binafsi.”
ISTANBUL, UTURUKI: FENERBAHCE imekanusha taarifa zinazodai kuwa inataka kumsajili winga wa Chelsea, Jamie Gittens, ikieleza kuwa tetesi hizo hazina msingi na ni sehemu ya jitihada za kuipotosha klabu.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu Uturuki imetoa taarifa rasmi ikisema haina nia ya kumsajili Gittens, huku ikizitaja taarifa zinazoendelea kusambaa kuwa “hazina msingi” na ni “majaribio ya kuendesha klabu kwa maslahi binafsi.”
Gittens, 21, amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kuondoka Chelsea katika dirisha hili la usajili, miezi michache tu baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya pauni milioni 55.
Hata hivyo, msimu wake wa kwanza Stamford Bridge haukuwa wa kuvutia kama ilivyotarajiwa, huku akikwazwa pia na majeraha yaliyomfanya ashindwe kupata mwendelezo mzuri wa kucheza.
Kutokana na hali hiyo, kumekuwa na taarifa zinazomhusisha na klabu kadhaa zinazoweza kuwa tayari kumpa nafasi ya kuanza upya, huku Fenerbahce ikitajwa miongoni mwa zinazomuwania.
Lakini baada ya taarifa rasmi ya Fenerbahce, inaonekana Uturuki haitakuwa kituo kinachofuata kwa Gittens, hali inayofanana na Gabriel Martinelli, ambaye naye amekuwa akihusishwa na uhamisho kwenda nchini humo.