Chelsea, Man City kuwania ubingwa wa Kombe la FA
Muktasari:
- Wakati Chelsea, ikisaka taji lake la tisa la Kombe la FA, Manchester City inatarajia kusherehekea ubingwa wa nane katika mashindano hayo endapo ikiibuka bingwa.
LONDON, ENGLAND: FAINALI ya 145 katika Kombe la FA nchini England, inachezwa leo Jumamosi majira ya saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Wembley ambapo Chelsea itapambana na Manchester City.
Wakati Chelsea, ikisaka taji lake la tisa la Kombe la FA, Manchester City inatarajia kusherehekea ubingwa wa nane katika mashindano hayo endapo ikiibuka bingwa.
Chelsea inaingia kwenye mechi hii ikiwa na jukumu gumu la kumaliza msimu angalau na kitu mkononi baada ya kutokuwa na mwendo mzuri licha ya uwekezaji mkubwa wa fedha uliowekwa na kuwaacha mashabiki wakikosa matumaini juu ya mpango wa timu wa kuwakuza wachezaji vijana.
Wakati klabu hiyo ikiendelea kutafuta mrithi wa Liam Rosenior, huku Xabi Alonso na Andoni Iraola wakitajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaowania nafasi hiyo, kocha wa kikosi cha chini ya miaka 21, Calum McFarlane, anaiongoza timu kwa muda, akilenga kuwa kocha wa kwanza wa Chelsea kushinda Kombe la FA tangu Antonio Conte mwaka 2018.
McFarlane alianza majukumu yake wiki tatu zilizopita kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Leeds United katika nusu fainali ya Kombe la FA, ambapo kichwa cha Enzo Fernandez kipindi cha kwanza kilitosha kuipa Chelsea ushindi. Ushindi huo uliipeleka Chelsea kwenye fainali yao ya 17 ya Kombe la FA, idadi inayozidiwa tu na Manchester United (22) na Arsenal (21).
Katika njia ya kuelekea Wembley, Chelsea ilishinda dhidi ya Charlton Athletic (5-1), Hull City (4-0), Wrexham (4-2) na Port Vale (7-0), timu zote zisizo za Ligi Kuu England. Nusu fainali ikaifunga Leeds United ya Ligi Kuu bao 1-0. Mara ya mwisho Chelsea kuzifunga timu mbili za Ligi Kuu katika msimu mmoja wa Kombe la FA ilikuwa 2020-21 ilipoitoa Sheffield United robo fainali kabla ya kuitoa Manchester City nusu fainali.
Chelsea imekuwa na makali ya kutikisa nyavu kwenye Kombe la FA msimu huu, ikifunga mabao 21 katika mechi tano na kuruhusu matatu pekee. Hii ni rekodi yao ya pili bora zaidi ya ufungaji kwenye mashindano hayo, ikizidi mabao 20 ya msimu wa 2006-07 na kubaki nyuma ya mabao 25 ya msimu wa 1969-70.
Katika Ligi Kuu England, Chelsea iko nafasi ya tisa na inazidiwa pointi sita kufikia sita bora. Wikiendi iliyopita ilipata sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool, matokeo yaliyositisha mfululizo wa mechi sita za kupoteza, lakini bado imefikisha mechi saba bila ushindi wa ligi. Kushinda Kombe la FA kutawahakikishia nafasi ya kucheza Europa League msimu ujao.
Hata hivyo, Chelsea inaingia kama timu isiyopewa nafasi kubwa ya kushinda, huku historia yao ya fainali za Kombe la FA ikiwa ya wastani, imeshinda mara nane na kupoteza mara nane kati ya fainali 16 ilizocheza, ikiwemo kupoteza fainali tatu mfululizo kati ya 2020 hadi 2022.
Kwa upande wa Manchester City, tayari imeandika historia kwa kufika fainali nne mfululizo za Kombe la FA, lakini rekodi hiyo imekuwa na maumivu. Baada ya kuifunga Manchester United na kutwaa taji mwaka 2023, ilipoteza fainali mbili zilizofuata dhidi ya Manchester United na Crystal Palace.
Mbali na vipigo hivyo vya fainali, City imekuwa bora sana kwenye Kombe la FA, ikishinda mechi 21 kati ya 23 za mwisho. Tangu Pep Guardiola aanze kazi msimu wa 2016-17, City ndiyo timu yenye ushindi mwingi zaidi (45), mabao mengi zaidi (159), na clean sheets nyingi zaidi (28) katika mashindano hayo.
Safari yao ya Wembley ilianza kwa ushindi mkubwa wa mabao 10-1 dhidi ya Exeter City, kabla ya kuziondoa Salford City (2-0), Newcastle United (3-1) na Liverpool (4-0). Katika nusu fainali ilitoka nyuma na kuifunga Southampton mabao 2-1.
City inataka kuepuka rekodi mbaya ya Chelsea ya kupoteza fainali tatu mfululizo, huku pia ikisaka historia ya kutwaa makombe yote mawili ya ndani ya England, baada ya kushinda Kombe la Ligi dhidi ya Arsenal, Machi mwaka huu.
Katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, City bado inaifukuzia Arsenal baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Brentford na Crystal Palace. Hata hivyo, kwa sasa mawazo yao yote yako Wembley katika fainali yao ya 15 ya Kombe la FA, ambapo imeshinda saba na kupoteza saba kati ya fainali zao 14 zilizopita.
City pia ina rekodi nzuri dhidi ya Chelsea, ikiwa haijafungwa katika mechi 13 za mwisho kwenye mashindano yote (ushindi 10, sare 3) tangu ilipofungwa 1-0 kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021. Rekodi hiyo inajumuisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Chelsea katika nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 2024, pamoja na ushindi wa 3-0 Stamford Bridge mwezi uliopita.
HALI YA TIMU
Chelsea itawakosa nyota watatu kutokana na majeraha ambao ni Estevao Willian (goti), Jamie Gittens (misuli ya nyuma ya paja) na Jesse Derry (kichwa). Hata hivyo, Robert Sanchez, Pedro Neto na Alejandro Garnacho wamerejea mazoezini na wanaweza kucheza.
Nahodha Reece James pia ameonekana kuwa fiti mazoezini na anaweza kurejea kikosini ama beki wa kulia au kiungo wa chini sambamba na Moises Caicedo.
Enzo Fernandez amehusika kwenye mabao sita katika mechi tisa za Kombe la FA akiwa Chelsea (mabao manne na pasi mbili za mabao), huku Cole Palmer akitarajiwa kucheza upande wa kulia wa ushambuliaji dhidi ya klabu yake ya zamani.
Kwa Manchester City, Rodri ndiye mwenye shaka pekee kutokana na maumivu ya nyonga. Nico Gonzalez yupo tayari kucheza baada ya kukosekana dhidi ya Crystal Palace.
Erling Haaland, Jeremy Doku, Rayan Cherki na Nico O’Reilly wanatarajiwa kurejea kikosi cha kwanza dhidi ya Chelsea. Haaland, hata hivyo hajawahi kufunga bao katika mechi 15 za nusu fainali au fainali tangu ajiunge na City mwaka 2022.
VIKOSI
Chelsea: Sanchez; Gusto, Fofana, Colwill, Hato; James, Caicedo; Palmer, Fernandez, Cucurella; Pedro
Manchester City: Trafford; Nunes, Khusanov, Guehi, O’Reilly; Gonzalez, Bernardo; Semenyo, Cherki, Doku; Haaland