Eduardo Camavinga aingia anga za Liverpool
Muktasari:
- Hata hivyo, Real Madrid haijaonyesha nia ya kumuachia kirahisi kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye ni sehemu muhimu ya mipango ya kikosi cha kwanza.
LIVERPOOL imeweka mezani ofa inayokadiriwa kufikia Pauni 60 milioni kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Real Madrid, Eduardo Camavinga, 23.
Hata hivyo, Real Madrid haijaonyesha nia ya kumuachia kirahisi kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye ni sehemu muhimu ya mipango ya kikosi cha kwanza.
Awali, Camavinga aliripotiwa kwamba anaweza kuondoka kwa sababu hakuwa anapata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.
Mkataba wa sasa wa Camavinga unatarajiwa kumalizika 2029, huku msimu huu akiwa ameshacheza mechi 16 za michuano yote na kufunga mabao mawili.
Mabosi wa Real Madrid wanadaiwa kuwa tayari kumuuza fundi huyo lakini kwa kiasi cha pesa kisichopungua Pauni 70 milioni.
Baada ya kuanza vibaya msimu huu, Liverpool inataka kufanya maboresho katika dirisha la usajili la majira ya baridi ifikapo Januari ili kujaribu kujiokoa na hali inayopitia kwa sasa.
Ricardo Pepi
FULHAM imefufua tena harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji wa PSV Eindhoven, Ricardo Pepi, ambaye ni raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 22.
Mabosi wa PSV wapo tayari kumuuza Pepi lakini kwa kiasi kisichopungua Pauni 40 milioni. Fulham inataka kumsajili staa huyo ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji. Kwa sasa Pepi ni miongoni mwa wachezaji tegemeo kikosini.
Antoine Semenyo
LIVERPOOL ipo tayari kuingia katika vita dhidi ya Manchester City katika mbio za kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth, Antoine Semenyo, 25.
Mabosi wa Liverpool wamefikia hatua hiyo baada ya hivi karibuni taarifa kudai Semenyo ameichagua Man City kama moja kati ya timu ambazo angependa kujiunga katika dirisha lijalo akidai kupendezwa na mpango kazi ambao Man City wameuwasilisha.
Omar Marmoush
TOTTENHAM Hotspur inapanga kusajili mshambuliaji mpya katika dirisha la usajili la Januari ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Miongoni mwa mastaa ambao imewaweka katika orodha ni pamoja na Omar Marmoush, 26, wa Manchester City na timu ya taifa ya Misri, Samu Aghehowa, 21, wa FC Porto pamoja na Kenan Yildiz 20 wa Juventus na timu ya taifa ya Uturuki.
Leon Goretzka
TOTTENHAM Hotspur imepewa nafasi ya kumsajili kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Leon Goretzka, 30. Bayern iko tayari kumuuza kutokana na mipango ya kufanya mabadiliko katika safu ya kiungo.
Spurs inamwangalia Goretzka kama mchezaji mwenye uzoefu mkubwa anayeweza kusaidia kuongeza ubora katika safu hiyo.
Van de Ven amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Spurs kutokana na kasi, nguvu na uwezo wa kuzuia mashambulizi ya kushtukiza.
Nathan Ake
MANCHESTER City ipo tayari kumuuza beki wa kati Nathan Ake, 30, katika dirisha la usajili la Januari iwapo itapokea ofa isiyopungua Pauni 21 milioni.
Ake amekuwa sehemu ya kikosi cha Man City kwa misimu kadhaa akichangia mafanikio ya klabu hiyo ndani na nje ya England. Hata hivyo, mpango wa Man City kufanya mabadiliko na kuingiza damu changa zaidi umefungua milango zaidi ya fundi huyo kuondoka katika dirisha lijalo.
Marc-Andre ter Stegen
GIRONA ina mpango wa kumsajili kipa wa Barcelona na timu ya taifa ya Ujerumani, Marc-Andre ter Stegen katika dirisha lijalo na imepata matumaini makubwa baada ya Aston Villa kuripotiwa kuachana na mpango huo.
Tangu kuanza kwa msimu huu Ter Stegen amekuwa akihusishwa kuondoka kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Barca.
Lucas Paqueta
WEST Ham United inaweza kumruhusu kiungo wa kimataifa wa Brazil, Lucas Paqueta, 28, kuondoka katika dirisha la usajili la Januari iwapo itapokea ofa inayoridhisha.
Paqueta amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha West Ham kutokana na ubunifu na uwezo wake wa kuchezesha timu, lakini West Ham inataka kumuuza ili kupata fungu litakaloisaidia kufanya usajili majira ya baridi na kiangazi.