Ederson: Sijui kwa nini usajili wangu ulivunjika
Muktasari:
- Ederson, 27, alikuwa akitarajiwa kujiunga na United kwa ada ya pauni39 milioni ikiwa sehemu ya mpango wa klabu hiyo kuimarisha safu yake ya kiungo.
MANCHESTER, England. Kiungo wa Atalanta, Ederson, amefichua kuwa bado hajui sababu halisi iliyofanya uhamisho wake wa kwenda Manchester United kuvunjika mapema msimu huu wa joto.
Ederson, 27, alikuwa akitarajiwa kujiunga na United kwa ada ya pauni39 milioni ikiwa sehemu ya mpango wa klabu hiyo kuimarisha safu yake ya kiungo.
Hata hivyo, mwanzoni mwa Julai United ilisitisha mchakato huo baada ya vipimo vya awali vya afya kuonyesha kuwa kiungo huyo alikuwa na tatizo kwenye goti.
Ederson ambaye baadaye alisaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Atalanta, amesema bado anashangazwa na kilichotokea.
“Kwa kweli sijui nini kilitokea,” alisema Ederson alipokuwa akizungumza kabla ya mchezo wa Atalanta dhidi ya Hapoel Tel Aviv katika mchujo wa Ligi ya Mikutano ya Ulaya.
“Nilikuwa na ofa kutoka klabu nyingine na hata ningeweza kujiunga na timu nyingine ya England. Vipimo vilikwenda vizuri, sijui ni nini kilibadilika. Nimekuwa Atalanta kwa miaka minne na nimekuwa nikicheza mara kwa mara.”
Kiungo huyo alisema angeweza kusubiri kuona mambo yangeishia wapi, lakini uhusiano mzuri aliokuwa nao na Atalanta ulimshawishi kubaki na kusaini mkataba mpya.
“Ningeweza kusubiri tu kuona kitakachotokea, lakini uhusiano mzuri na klabu ulinishawishi kubaki na kusaini mkataba mpya,” alisema.
Awali, vyanzo vya ndani vya Manchester United vilisisitiza kuwa klabu hiyo ilikuwa na mpango wa kukamilisha usajili huo mwanzoni mwa Julai baada ya kufikia makubaliano kuhusu muundo wa ada na maslahi binafsi ya mchezaji na Atalanta.
Hata hivyo, Ederson aliitwa kwa kuchelewa kwenye kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia na kocha Carlo Ancelotti baada ya beki wa Roma, Wesley, kupata jeraha.
Hali hiyo ililazimisha United kuanza sehemu ya kwanza ya vipimo vya afya nchini Marekani.
Baada ya tatizo la goti kugundulika, vipimo kamili vilipangwa kufanyika kwa ushirikiano na madaktari bingwa baada ya Brazil kuondolewa kwenye mashindano.
United baadaye iliamua kutokamilisha usajili huo kwa masharti yaliyokuwa yamekubaliwa awali.
Vyanzo vya habari vilieleza kusikitishwa kwao na hali hiyo kwa mchezaji na familia yake, huku vikikanusha vikali taarifa kwamba United ilisitisha usajili kabla ya kufanyika kwa vipimo kamili vya afya.
Hata hivyo, hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu afya ya Ederson iliifanya United kuanza kuangalia chaguo nyingine kwenye soko la usajili.
Klabu hiyo badala yake ilimfuata Youri Tielemans na pia ikamsajili Andrey Santos kutoka Chelsea kwa pauni milioni 50.
United bado inataka kuongeza nguvu zaidi kwenye kiungo na imeendelea na harakati za kumsajili Carlos Baleba wa Brighton kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Licha ya kuvunjika kwa uhamisho huo, Ederson amekuwa sehemu muhimu ya Atalanta. Katika misimu minne iliyopita amecheza mechi 180 kwa klabu hiyo, huku msimu wa 2025/26 akicheza mara 41 katika mashindano yote.
Kiungo huyo pia amesema ameamua kuangalia mbele baada ya tukio hilo na ana furaha kuendelea kubaki Atalanta.
“Nilikuwa na wakati mzuri nilipoenda Kombe la Dunia na Brazil, halafu… bado sijui kwa kweli nini kilitokea,” alisema.
“Lakini jambo muhimu ni kwamba niliweza kukabiliana na hali hiyo, nikarudi nikiwa na mtazamo sahihi na kutoa kila nilichokuwa nacho kwa klabu ambayo imenipa mengi.”
Ederson amesema tukio hilo halijabadilisha mtazamo wake kuhusu uwezo wake.
“Bado mimi ni Ederson. Kila mtu hapa ananijua na anajua ninachoweza kufanya. Wanajua kwamba nitatoa kila nilicho nacho,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wake wa kubaki Atalanta, Ederson alishukuru uongozi wa klabu hiyo kwa namna ulivyomsimamia wakati wa kipindi kigumu.
“Nina furaha sana kuendelea kuwa Atalanta. Nawashukuru sana klabu na mtendaji mkuu Luca Percassi. Walinipigia simu mara nyingi na nilihisi walikuwa upande wangu,” alisema.
“Ingawa nilikuwa na ofa kutoka klabu nyingine, baada ya kila kilichotokea nilifikiri ni bora kubaki na wale ambao walinionesha kwamba walinitaka kweli, na huyo alikuwa Atalanta siku zote.”
Ederson alihitimisha kwa kueleza furaha yake ya kuendelea kuvaa jezi ya klabu hiyo ambayo imekuwa sehemu muhimu ya safari yake ya soka.
“Nilifurahi kuvaa jezi ambayo imenipa furaha kubwa sana,” alisema.