Ederson anasikilizia bado, Galatasaray yaendelea kumnyemelea
Muktasari:
- Hadi sasa timu inayohusishwa naye ni Galatasaray ya Uturuki lakini ofa iliyowasilisha kama ada yake ya uhamisho.
KIPA wa Manchester City na timu ya taifa ya Brazil, Ederson Moraes, 31, anafikiria mustakabali wake ndani ya timu hiyo ambapo amepanga kuondoka katika dirisha hili lakini bado hajachagua timu ambayo atajiunga nayo.
Hadi sasa timu inayohusishwa naye ni Galatasaray ya Uturuki lakini ofa iliyowasilisha kama ada yake ya uhamisho.
Man City inataka kumsajili kipa wa PSG na timu ya taifa ya Italia Gianluigi Donnarumma, 26, ambaye amewekwa sokoni.
Mkataba wa Ederson na Man City unamalizika Juni 2026 na mbali ya Galatasaray pia huduma yake inawindwa na vigogo wa Saudi Arabia lakini mwenyewe anadaiwa kuhitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani barani Ulaya.
Man City awali ilikuwa inasita kumpa ruhusa ya kuondoka kabla yakuwa na uhakika wa kupata kipa mwingine atakayekuwa mbadala wake kwani licha ya kumsajili James Trafford, bado kocha Pep Guardiola anahitaji kipa mwingine wa kiwango cha juu zaidi.
Hadi sasa bado Man City haina uhakika wa asilimia mia wa kumpata Donnarumma lakini mazungumzo yanaendelea na yanaonekana kufikia hatua nzuri na kinachokwamisha hadi sasa ni makubaliao ya masuala ya ada ya uhamisho pekee lakini masuala ya maslahi binafsi yapo sawa.
Carlos Baleba
MANCHESTER United haitoendelea na mchakato wa kumsajili kiungo wa kati wa Brighton na timu ya taifa ya Cameroon, Carlos Baleba, 21, katika dirisha hili baada ya timu yake kuhitaji kiasi kisichopungua Pauni 115 milioni kwa ajili ya kumuuza.
Mabosi wa Man United wanaona kiasi hicho ni kikubwa.
Baleba ambayr alijiunga na Brighton Septemba 2023 akitokea Lille, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Goncalo Ramos
MABOSI wa Newcastle wamerudi tena katika mazungumzo na PSG kwa ajili ya kumsajilj mshambuliaji wa timu hiyo na Ureno, Goncalo Ramos, 24, katika dirisha hili ili kuongeza nguvu zaidi katika eneo lao la ushambuliaji ambalo mastaa wengi waliohitaji kuwasajili katika dirisha hili wamewakosa.
Ramos alitoka Benfica kwenda PSG mwaka 2023 kwa mkopo uliogeuka kuwa uhamisho wa kudumu.
Mkataba wake na PSG unatarajiwa kumalizika Juni 2028.
Rico Lewis
NOTTINGHAM Forest inataka kumsajili beki wa kulia wa Manchester City, Rico Lewis, 20, kwa ada ya Pauni 30 milioni katika dirisha hili.
Staa huyu ambaye ni zao la akademi ya Manchester City, alianza kucheza katika kikosi cha kwanza msimu wa 2022/23.
Mkataba wake Man City, unamalizika Juni 2028.
Lewis mwenyewe anatamani sana kuondoka kwa sababu anataka muda mwingi wa kucheza jambo ambalo hatolipati ikiwa ataendelea kucheza kubakia Man City.
Jackson Tchatchoua
WOLVES wako karibu kukamilisha usajili wa beki wa pembeni wa Verona na timu ya taifa ya Cameroon Jackson Tchatchoua, 23, katika dirisha hili. Fundi huyu ambaye ni mzaliwa wa Ubelgiji lakini alichagua kuichezea Cameroon, alitoka Anderlecht kwenda Verona 2023. Mkataba wake Verona unamalizika Juni 2027. Taarifa zinaeleza Wolves imeshatuma hadi wawakilishi wake kwenda Italia kwa ajili ya mazungumzo zaidi kabla ya kukamilisha dili hilo.
Yoane Wissa
NEWCASTLE inafanya mchakato wa haraka kuhakikisha inakamilisha usajili wa mshambuliaji wa Brentford na timu ya taifa ya DR Congo, Yoane Wissa, 28, katika dirisha hilo ili kuwahi kumtumia katika mechi za mwanzo za EPL.
Wissa ambaye alijiunga na Brentford mwaka 2021 akitokea Lorient, mkataba wake unamalizika mwaka 2026.
Kingsley Coman
KLABU ya Al-Nassr iko karibu kukamilisha usajili wa winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa Kingsley Coman, 28, kwa dau la Pauni 25.8 milioni. Coman ambaye amekuwa Bayern tangu mwaka 2015 akitokea Juventus ameshinda jumla ya mataji nane ya Bundesliga hadi sasa. Mkataba wake na Bayern unatarajiwa kumalizika Juni 2027. Licha ya Bayern awali kuonyesha nia ya kumbakisha Coman amewaambia kwamba anataka kuondoka.
Nordi Mukiele
SUNDERLAND imefikia makubaliano na Paris Saint-Germain kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo na Ufaransa Nordi Mukiele,27, kwa ada ya awali Pauni 9.5 milioni pamoja na nyongeza ya Pauni 2.5 milioni katika dirisha hili.
Mabosi wa Sunderland wanajaribu kusuka kikosi chao kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vizuri katika dirisha hili baada ya kupanda daraja.
Nordi ambaye alijiunga na PSG kutoka RB Leipzig mwaka 2022, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.