Duh! Mtoto wa Totti astaafu soka
Muktasari:
- Mtoto huyo, Cristian Totti alitangaza uamuzi wa kutundika daruga zake wiki iliyopita, alipoambia La Nuova: “Sina cha kusema zaidi, ndiyo, nimefanya uamuzi, nimestaafu.”
ROME, ITALIA: MTOTO wa gwiji wa Italia na AS Roma, Francesco Totti amestaafu soka la kulipwa akiwa na umri wa miaka 19.
Mtoto huyo, Cristian Totti alitangaza uamuzi wa kutundika daruga zake wiki iliyopita, alipoambia La Nuova: “Sina cha kusema zaidi, ndiyo, nimefanya uamuzi, nimestaafu.”
Kilichoelezwa ni mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ameamua kustaafu baada ya kuona ugumu wa kufikia kile alichofanya baba yake.
Mwandishi wa habari Mtaliano, Paolo Ardovino alisema: “Mechi yake ya mwisho ilikuwa Sardinia, mwaka mmoja uliopita alipokuwa Olbia kwenye Serie D.
“Mechi chache, presha kubwa kutoka kwenye vyombo vya habari, na kumekuwa na utata mwingi huko kwenye mitandao kijamii kuhusu mwonekano wake. Lakini, ukweli amekuwa na mwili sahihi kabisa kwa mwanasoka.”
Wakati huo huo, kocha wake wa zamani, Marco Amelia alisema Cristian alikuwa na kiwango cha kutosha kabisa kuendelea na soka lake katika ligi za chini huko Italia.
Hata hivyo, kinachoelezwa ni hadhi ya baba yake aliyoweka kwenye mchezo wa soka imechangia kwa kiasi kikubwa mtoto wake kustaafu mapema.
Amelia alisema: “Nadhani angekuwa na mwendo mzuri kwenye soka lake kama mchezaji katika Serie C na Serie B. Lakini, kuwa mtoto wa Totti hilo limekuwa na madhara makubwa.”
Cristian sasa anajiandaa kwenda kufanya kazi na kaka yake, Riccardo, huko kwenye shule ya soka ya baba yao, Totti Soccer School. Atakuwa na kazi ya kutafuta vijana wenye vipaji vya soka na kufanya kazi kwa ukaribu kabisa na meneja wa akademia, Claudio D’Ulisse.
Akizaliwa mjini Rome, Cristian alitumikia miaka yake ya utoto akiwa kwenye timu za watoto za AS Roma. Baadaye alikwenda kwenye akademia za Frosinone na Rayo Vallecano kabla ya kucheza kwenye Serie D akiwa na vikosi vya Avezzano na Olbia. Baba yake alidumu Roma misimu 25, akicheza mechi 785.