Dortmund yamkomalia Sancho, Man United yashusha bei
Muktasari:
- Inaelezwa kwa sababu, Man United ilikuwa na makubaliano na Chelsea ya kugeuza mkopo wa Sancho kuwa uhamisho wa kudumu kwa kulipa Pauni 25 milioni mwishoni mwa msimu uliopita, lakini klabu hiyo yenye maskani yake London iliamua kutoendelea naye na badala yake ikalipa faini ya Pauni 5 milioni na kumrudisha Old Trafford.
BAADA ya kuona hakuna timu iliyo tayari kutoa Pauni 25 milioni kwa ajili ya kumnunua winga wa kimatafa wa England, Jadon Sancho, mabosi wa Manchester United sasa wanaripotiwa kuwa wako tayari kumuuza staa huyo kwa bei pungufu na Borussia Dortmund inatajwa kutaka kumsajili
Inaelezwa kwa sababu, Man United ilikuwa na makubaliano na Chelsea ya kugeuza mkopo wa Sancho kuwa uhamisho wa kudumu kwa kulipa Pauni 25 milioni mwishoni mwa msimu uliopita, lakini klabu hiyo yenye maskani yake London iliamua kutoendelea naye na badala yake ikalipa faini ya Pauni 5 milioni na kumrudisha Old Trafford.
Kutokana na kupata kiasi hicho, sasa Man United imeamua kushusha bei ya Sancho ambaye awali alikuwa anauzwa kwa Pauni 25 milioni.
Sancho anadaiwa kuwa yupo tayari kujiunga na Dortmund ambayo inataka kulipa bei ya punguzo ambayo Man United inaihitaji.
Staa huyu alijiunga na Man United akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya Pauni 73 milioni mwaka 2021, na alirejea tena kwenye klabu hiyo ya Bundesliga kwa mkopo Januari 2024 baada ya kutofautiana na kocha wa zamani wa Man United, Erik ten Hag.
Vilevile Juventus pia imekuwa ikimfuatilia kwa muda mrefu katika kipindi hiki cha uhamisho cha majira ya kiangazi lakini inataka kumchukua kwa mkopo wakati Manchester United ikihitaji kumuuza mazima winga huyo ambaye aliwahi kutabiriwa kuwa angetisha sana katika ulimwengu wa soka lakini amejikuta akishindwa kufikia matarajio ya wengi.
Nick Pope
KIPA wa Newcastle United na England, Nick Pope, 33, huenda akatimkia Manchester United katika dirisha hili ikiwa timu yake itafanikisha mchakato wa kumsajili kipa wa Southampton, Aaron Ramsdale katika dirisha hili. Pope ni kati ya makipa ambao wamependekezwa na benchi la ufundi la Man United ambalo licha ya kukubali kumbakisha Andre Onana bado halina imani naye sana. Mkataba wa Pope unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Eberechi Eze
ARSENAL bado ina nia ya kumsajili winga wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Eberechi Eze, 27, lakini haiko tayari kulipa Pauni 60 milioni zinazohitajika ili kuvunja mkataba wake, hivyo inafanya mazungumzo na Palace kuona kama bei itapunguzwa.
Eze ameshawaambia mabosi wa Palace kwamba anahitaji changamoto mpya kwa msimu ujao. Msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao 14.
James McAtee
MANCHESTER City imekataa ofa ya Pauni 25 milioni kutoka Nottingham Forest kwa ajili ya kumuuza kiungo wao wa kimataifa wa England, James McAtee mwenye umri wa miaka 22. Taarifa kutoka tovuti ya Sky Sports zinaeleza kuwa City inahitaji walau Pauni 30 milioni kwa ajili ya kumuuza McAtee ambaye anataka kuondoka ili kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.
Illia Zabarnyi
PARIS St-Germain inaendelea kufanya mchakato wa kukamilisha dili la kumsajili beki kisiki wa Bournemouth, Illia Zabarnyi, 22, katika dirisha hili.
Staa huyu wa kimataifa wa Ukraine amekuwa katika kiwango bora sana kwa msimu uliopita na Bournemouth ipo tayari kumuuza lakini kwa kiasi kisichopungua Pauni 40 milioni.
Mkataba wa Zabarnyi, unaisha 2029. Msimu uliopita alicheza mechi 39 za michuano yote.
Trossard
BORUSSIA Dortmund inamfuatilia winga wa Arsenal, Leandro Trossard, 30, lakini staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji pia anawaniwa na klabu mbili za Ligi Kuu England.
Taarifa kutoka tovuti ya Sky Sports Germany zimefichua kuwa timu hiyo inahitaji sana huduma ya Trossard na mwenyewe yupo tayari kujiunga nao katika dirisha hili.
Federico Chiesa
FENERBAHCE imeanza kuwasiliana na mshambuliaji wa Liverpool, Federico Chiesa, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Staa huyu mwenye umri wa miaka 27, hakupata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Liverpool kwa msimu uliopita hali inayosababisha atafute sehemu ya kucheza kwa msimu ujao.
Tyler Morton
MABOSI wa Olympique Lyon wanavutiwa sana na kiungo wa Liverpool na England, Tyler Morton, 22, na tayari wamewasiliana na mabosi wa majogoo hao wa London kwa ajili ya kuulizia ada ya uhamisho. Tyler mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kuondoka katika dirishahili. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.