DILI TAMU! Rashford aende Napoli, Osimhen aje Man United
Muktasari:
- Fowadi, Rashford, ambaye Manchester United inamthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 60 milioni aligomea ofa tatu za kutoka Saudi Arabia ambazo zingemshuhudia akilipwa mshahara wa Pauni 675,000 kwa wiki kwa sababu anataka kurudisha namba yake kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA, Marcus Rashford huenda akahusishwa kwenye dili la kubadilishana mchezaji litakalomhusu straika wa Napoli, Victor Osimhen kwenye dirisha hili.
Fowadi, Rashford, ambaye Manchester United inamthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 60 milioni aligomea ofa tatu za kutoka Saudi Arabia ambazo zingemshuhudia akilipwa mshahara wa Pauni 675,000 kwa wiki kwa sababu anataka kurudisha namba yake kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England.
Uhamisho wa kwenda kwenye klabu nyingine ya Ulaya itampa Rashford fursa hiyo na ndio maana kocha wa Napoli, ambaye aliwahi kufanya kazi kwenye Ligi Kuu England kuzinoa Chelsea na Tottenham Hotspur, Antonio Conte anahitaji huduma ya mchezaji huyo akakipige Serie A.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim anataka kuboresha kikosi chake kwenye dirisha hili la Januari na kocha Conte ameonyesha dhamira ya kutaka saini ya Rashford, 27, hivyo hilo wanaamini litafungua milango kwa miamba hiyo ya Old Trafford kunasa huduma ya straika Osimhen.
Straika huyo Mnigeria — ambaye mkataba wake una kipengele kinachotaja bei anayouzwa, ambayo ni Pauni 62 milioni — kwa sasa yupo kwa mkopo Galatasaray huko Uturuki, lakini Man United inaweza kunasa saini yake kwenye dirisha la mwezi huu.
Osimhen, 26, amefunga mabao 65 katika mechi 108 alizocheza kwenye Serie A akiwa na Napoli tangu alipojiunga kutokea Lille mwaka 2020.
Amorim atapenda pia kufanya kazi na fowadi wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres tena huko Old Trafford, lakini wakati anaondoka kwenye klabu yake hiyo ya zamani alifikia makubaliano kwamba hatasajili wachezaji wa timu hiyo katikati ya msimu hadi mwishoni mwa msimu, dirisha la majira ya kiangazi.
Amorim hana wafungaji wa kutosha kwenye timu yake na hivi za karibuni alimweka kando Rashford kutokana na ubora wake wa mazoezini tangu kwenye mechi ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao Manchester City kwenye kipute cha Ligi Kuu England katika Manchester derby, Desemba 15.
Rashford hajaichezea Man United kwenye mechi tano zilizopita — licha ya kwamba kwenye mechi hizo, Man United imekumbana na vipigo vitatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England na kuifanya timu hiyo kuporomoka hadi kwenye nafasi ya 14 katika msimamo na kukabiliwa na vita ya kukwepa kushuka daraja. Staa huyo alipata ofa ya kuwa Mwingereza anayelipwa pesa nyingi zaidi huko kwenye klabu za Saudi Arabia, ambako ingezidi kiwango anacholipwa kwa sasa cha Pauni 315,000 kwa wiki, wakati huko Mashariki ya Kati, angelipwa Pauni 675,000 kwa wiki.
Ofa hiyo ya Pauni 35 milioni kwa mwaka ingekuwa karibu asilimia 70 zaidi ya mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki, anaolipwa nahodha wa England, Harry Kane, 31, huko kwenye klabu ya Bayern Munich.
Rashford alifunguka mwezi uliopita kwamba yupo tayari kwa ajili ya kwenda kukabiliana na changamoto mpya, licha ya kwamba mkataba wake huko Old Trafford ni mrefu hadi 2028. Man United inaweza kumpiga bei Rashford ili kuweka vitabu vyao hesabu sawa ili kuwa na pesa za kutosha kumpa Amorim asajili wapya.
Man United ilionyesha dhamira ya kumsajili Osimhen tangu kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, huku Chelsea na timu nyingine za Saudia zilikuwa zikimtaka Mnigeria huyo pia kabla ya kwenda Galatasaray katika dakika za mwisho kabisa za dirisha la usajili kufungwa.
Kocha Conte alimwondoa Osimhen kwenye kikosi cha Napoli ili kumsajili Romelu Lukaku, ambapo sasa kama Rashford atanaswa pia atakwenda kucheza timu moja na wachezaji wenzake wa zamani wa Man United akiwamo straika Romelu Lukaku na kiungo Scott McTominay.
Bayern Munich yenyewe imeshafuta mpango wa kumsajili Rashford. Juventus nayo imekatishwa tamaa na mshahara wa straika Joshua Zirkzee kwenye mpango wao wa kumnasa kwa mkopo fowadi huyo wa Kidachi.