Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili la Isak Liverpool, ofa ya kitajiri

Muktasari:

  • Straika huyo wa kimataifa wa Sweden, 25, aliwaambia mabosi wa klabu yake ya Newcastle United kwamba anataka kuachana nao baada ya Liverpool kuulizia huduma yake na ada ya Pauni 120 milioni mkononi.

NEWCASTLE, ENGLAND: ALEXANDER Isak amewekewa mezani ofa ya mshahara wa Pauni 32 milioni kwa mwaka kutoka Saudi Arabia, lakini moyo wake unataka kucheza Liverpool.

Straika huyo wa kimataifa wa Sweden, 25, aliwaambia mabosi wa klabu yake ya Newcastle United kwamba anataka kuachana nao baada ya Liverpool kuulizia huduma yake na ada ya Pauni 120 milioni mkononi.

Na sasa kinachoelezwa, Isak yupo tayari kuwasilisha barua ya kuomba kwenda kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu England, Liverpool.

Anataka kwenda kukipiga Anfield licha ya ofa ya mkwanja mrefu kutoka kwa Al-Hilal, ambayo pia itamshuhudia akipata bonasi ya kusaini ya Pauni 14 milioni ikiwa ni sehemu ya marupurupu.

Isak ataweka mfukoni Pauni 3.6 milioni endapo timu itabeba ubingwa wa Saudi Pro League, Pauni 3.8 milioni ikishinda taji la Ligi ya Mabingwa Asia na Pauni 1.75 milioni akimaliza kinara wa mabao wa msimu.

Atakunja pia Pauni 120,000 kwa mwezi kwa ajili ya gharama binafsi kama usafiri wake na familia, huku akikabidhiwa nyumba na klabu na wafanyakazi wanne wa muda wote pamoja na dereva wa kumwendesha popote anaendapo. Kingine atapewa usafiri wa ndege binafsi kwa ajili ya safari zake na familia au anapoitwa kwenye timu ya taifa ya Sweden.

Mshahara utamfanya kuwa mchezaji namba tano anayelipwa mkwanja mrefu nyuma ya Sadio Mane, Karim Benzema, Riyad Mahrez na Cristiano Ronaldo. Lakini, Isak anachotaka ni kwenda Liverpool.

Newcastle haitaki kumuuza straika huyo aliyefunga mabao 27 msimu uliopita licha ya kutokuwapo kwenye ziara ya timu hiyo ya pre-season huko Asia.

Miamba hiyo ya St James’ Park imeshindwa kumshawishi kusaini dili la Pauni 300,000 kwa wiki, ambalo lingemfanya kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kwenye kikosi hicho cha Newcastle.

Na sasa wasiwasi wao ni kwamba Isak anaweza kulazimisha uhamisho kwa kuandika barua ya kutaka kuondoka. Kutokana na hilo, wameanza kumfukuzia straika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko wakiamini ni mtu mwafaka wa kuja kuchukua mikoba ya Isak endapo kama atalazimisha kuondoka.

Sambamba na hilo, Newcastle imeweka mezani pia ofa ya Pauni 35 milioni kwa ajili ya kunasa huduma ya mshambuliaji wa Brentford, Yoane Wissa baada ya ofa yao ya mwanzo ya Pauni 25 milioni kukataliwa.

Fowadi mpya wa Liverpool, Hugo Ekitike, ambaye aliigomea Newcastle na kuchagua kutua Anfield, alisema Isak atakwenda kuungana naye huko kwenye kikosi cha Merseyside ili kupita mzigo pamoja.

Straika huyo Mfaransa aliigharimu Liverpool, Pauni 69 milioni aliponaswa kutoka Frankfur, lakini kocha  Arne Slot bado anamtaka Isak  aende akaungane na Mohamed Salah na Florian Wirtz kwenye fowadi mpya ya timu hiyo.

Na Ekitike, 23, alisema anapenda kucheza mtindo wa straika pacha, aliposema: “Naweza kucheza peke yangu, lakini napenda pia kucheza kama pacha.”