Dili la Chelsea kwa Xavi Simons laingia ugumu, ipo hivi
Muktasari:
- Chelsea inadaiwa ilitaka kutoa mmoja kati ya wachezaji wake pamoja na kiasi kidogo cha pesa kama sehemu ya ofa ya kuipata saini yake.
JARIBIO la Chelsea kumsajili mshambuliaji wa RB Leipzig raia wa Uholanzi, Xavi Simons, mwenye umri miaka 22, limekwama baada klabu ya mchezaji kusisitiza kwamba inahitaji pesa ili kumuuza.
Chelsea inadaiwa ilitaka kutoa mmoja kati ya wachezaji wake pamoja na kiasi kidogo cha pesa kama sehemu ya ofa ya kuipata saini yake.
Katika msimu uliopita Simons amecheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao 11. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Inaelezwa Leipzig inahitaji ada ya uhamisho inayofikia Pauni 60 milioni kwa ajili ya kiungo mshambuliaji huyo.
Wakala Ali Barat anayemsimamia Simons anadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Chelsea na kwa sababu hiyo ameshamshawishi mchezaji wake kujiunga nao ingawa tatizo limebakia kwenye ada ya uhamisho.
Simons alijiunga RB Leipzig kwa mkopo akitokea Paris Saint-Germain mwaka 2023 kabla ya kusaini mkataba wa kudumu baadae.
RB Leipzig ililipa ada ya uhamisho ya Pauni 43 milioni iliyovunja rekodi ya usajili wa klabu yao, pia ilikubali kulipa nyongeza kulingana na kiwango atakachoonyesha na kiujumla dili hilo linaweza kuwagharimu Pauni 70 milioni.
Staa huyu anataka kuondoka RB Leipzig baada ya klabu hiyo kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Simons, ambaye ni zao la akademi ya La Masia ya klabu ya Barcelona, alisaini mkataba na Paris Saint-Germain (PSG) mwezi Julai 2019, ambapo alijiunga kwanza na kikosi cha wachezaji wa chini ya umri wa miaka 19 kabla ya kuitumikia timu ya wakubwa kwa mara ya kwanza 2021.
Yann Bisseck
BEKI wa Inter Milan, Yann Bisseck mwenye umri wa miaka 24, amekataa kujiunga na Crystal Palace licha ya timu hiyo kuwasilisha ofa ya Pauni 28 milioni ambayo ilikubaliwa na mabosi wa Inter. Bisseck anadaiwa kukataa ofa hiyo kwa sababu anahitaji kucheza Ligu ya Mabingwa msimu ujao na anaona namna pekee ya kufanikisha hilo ni kuendelea kusalia katika kikosi cha Inter. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Ademola Lookman
ATALANTA imekataa ofa ya Pauni 36.5 milioni kutoka kwa Inter Milan inayohitaji huduma ya winga wa kimataifa wa Nigeria, Ademola Lookman, mwenye umri wa miaka 27. Mabosi wa Atalanta wamekataa ofa hiyo kwa sababu wanaona ni ndogo kwani wanahitaji angalau Pauni 43.5 milioni ili kumuuza. Ademola ambaye ni mmoja kati ya washambuliaji wanaofanya vizuri Italia, mkataba wake na Atalanta unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Callum Brittain
MIDDLESBROUGH imefikia makubaliano na Blackburn kumnunua beki wa timu hiyo Callum Brittain, mwenye miaka 27, katika dirisha hili. Katika makubaliano hayo Middlesbrough itatoa Pauni 3.5 milioni kama ada ya uhamisho ya Brittain CallumMkataba wa sasa wa Brittain unatarajiwa kumalizika mwakani. Msimu uliopita akiwa na Blackburn alicheza mechi 35 za michuano yote na kufunga mabao mawili.
Rasmus Hojlund
RB Leipzig ni kati ya klabu kadhaa zinazomfuatilia Rasmus Hojlund, katika dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya Mashetani Wekundu kuonyesha nia ya kuachana naye. Staa huyu wa kimataifa Denmark mwenye umri wa miaka 22 anaweza akatumika katika dili la mabadilishano ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Slovenia, Benjamin Sesko, mwenye umri wa miaka 22. Hojlund mkataba wake unaisha mwaka 2028.
Joao Palhinha
TOTTENHAM imemalizana na Bayern Munich katika dili la kumsajili kwa mkopo kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Ureno, Joao Palhinha, mwenye umri wa miaka 30. Palhinha ambaye aliwahi kucheza Fulham ya England ameondoka Bayern kwa sababu hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Spurs imemchukua kwa mkopo ambao una kipengele cha kumnunua lakini sio lazima.
Nico O’Reilly
KIUNGO wa timu ya taifa ya vijana ya England chini ya miaka 20, Nico O’Reilly, mwenye umri wa miaka 20, atasaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Manchester City baada ya klabu hiyo kukataa ofa mbili za uhamisho kutoka Bayer Leverkusen ya Ujerumani. Awali, Leverkusen iliwasilisha ofa ya kutaka kumchukua fundi huyu kwa mkopo.
Matt O’Riley
JUVENTUS imeungana na Atalanta, Napoli na AS Roma kuiwania saini ya kiungo wa kimataifa wa Denmark anayechezea Brighton, Matt O’Riley, mwenye miaka 24. Tovuti ya Sky Sports Italia imefichua kuwa vigogo hawa wameshatuma hadi wawakilishi wao kwenda England kwa ajili ya mazungumzo. O’Riley, anatamani sana kuondoka katika dirisha hili.