Deni laiponza Lyon, yashushwa daraja hadi Ligue 2 Ufaransa

VIGOGO wa Ligue 1, Lyon, wameshushwa daraja kutoka Ligi Kuu Ufaransa hadi Ligue 2 kutokana na deni kubwa la takriban euro milioni 500.
Lyon, pamoja na baadhi ya klabu nyingine kubwa za Ligue 1, walifika mbele ya Baraza la Kitaifa la Udhibiti wa Usimamizi wa Fedha (DNCG) ambapo walichunguzwa kuhusu hali yao ya kifedha.
Baada ya hapo, imeamuliwa rasmi kwamba Olympique Lyon itashushwa daraja na msimu ujao kucheza Ligue 2.
Mwaka uliopita, Lyon waliripoti kuwa na deni la takriban euro milioni 500. Hata hivyo, kundi la Eagle Football, ambalo ndilo wamiliki wa klabu hiyo ya Ufaransa, walichukua hatua mbalimbali za kifedha kujaribu kuishawishi DNCG kuwa hali ya kifedha ya klabu hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Hatua hizo ni pamoja na kuuza hisa za John Textor katika klabu ya Crystal Palace na timu ya wanawake ya Lyon. Hata hivyo, hatua hizo hazikukidhi matakwa ya DNCG.
Akizungumza na vyombo vya habari, Textor alisema: “Unaweza kuona kutokana na michango ya wana hisa wetu, tumewekeza mtaji mpya, si kwa ajili ya DNCG tu, bali pia kwa ajili ya mchakato wa kupata leseni ya UEFA. Na tusisahau habari njema ya mauzo ya Crystal Palace. Hali yetu ya kifedha kwa sasa imeimarika kwa kiasi kikubwa.”
Lyon sasa wanaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa DNCG, lakini iwapo adhabu hiyo itathibitishwa, vigogo hao wa soka la Ufaransa watalazimika kushiriki Ligue 2 msimu wa 2025-2026.
Ikumbukwe kuwa, Textor ambaye ni mfanyabiashara kutoka Marekani, ni mmiliki mwenza wa klab ya Crystal Palace inayoshiriki Ligi Kuu England, pia ni mmiliki wa kampuni ya Eagle Football Group ya nchini Ufaransa inayozisimamia klabu za Botafogo (Brazil), RWD Molenbeek (Ubelgiji) na Olympique Lyonnais (Ufaransa).