De Ligt aiokoa Man United dakika za mwisho ugenini
Muktasari:
- Beki Mdachi, De Ligt, aliruka juu kufunga kwa kichwa mpira wa kona kwenye dakika ya 90+6, hivyo kuifanya Man United kupata sare ya pili mfululizo kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England na kupoteza fursa ya kupanda hadi kwenye nafasi ya pili katika msimamo.
LONDON, ENGLAND: MPIRA wa kichwa wa dakika za mwisho kabisa kutoka kwa Matthijs de Ligt, uliiokoa Manchester United kukumbana na kichapo kutoka kwa Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika London, jioni ya leo Jumamosi Novemba 8, 2025.
Spurs iliyokuwa nyumbani, ilifunga mara mbili kwenye dakika 10 za mwisho kupitia kwa Mathys Tel na Richarlison na kuonekana kama ingetoka uwanjani hapo na pointi zote tatu kabla ya Man United kugoma na kusawazisha kwenye dakika za majeruhi kufanya ubao usomeke 2-2.
Beki Mdachi, De Ligt, aliruka juu kufunga kwa kichwa mpira wa kona kwenye dakika ya 90+6, hivyo kuifanya Man United kupata sare ya pili mfululizo kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England na kupoteza fursa ya kupanda hadi kwenye nafasi ya pili katika msimamo.
Katika mchezo huo, Man United ilitangulia kufunga kwa bao la kichwa cha Bryan Mbeumo, aliyeunganisha vyema krosi ya Amad Diallo kwenye kipindi cha kwanza na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Matokeo hayo yanaifanya Man United kufikisha pointi 18 sawa na ilivyo kwa Spurs, zote zikicheza mechi 11. Katika mechi hizo, Man United imeshinda tano, sare tatu na vichapo vitatu, sawa na Spurs, ambayo pia imeshinda tano, sare tatu na vichapo vitatu, huku timu hizo zikitofautiana kwenye nafasi ya katika msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Spurs imefunga mabao 19 na kufungwa 10, hivyo ikiwa na +9 ya mabao ya kufungwa na kufungwa, wakati Man United imefunga 19 na kufungwa 18, ikiwa na +1 ya tofauti hiyo ya mabao, jambo linalofanya baada ya mechi hiyo kumalizika, Spurs ikiwa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo na Man United nafasi ya saba.
Kikosi cha Tottenham: Vicario; Porro, Van de Ven, Romero, Spence; Sarr, Palhinha, Simons; Johnson, Richarlison, Kolo Muani.
Kikosi cha Man Utd: Lammens; De Ligt, Maguire, Shaw; Mazraoui, Casemiro, Fernandes, Dorgu; Amad, Mbeumo, Cunha.