Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Banda aitaka WAFCON itangazwe zaidi duniani

Muktasari:

  • Banda anayekipiga Orlando Prides ya Ligi Kuu ya Wanawake Marekani alisema mashindano hayo yana wachezaji wengi wa Afrika wanaocheza Ulaya lakini hawapati matangazo yatakayowafikisha duniani.

NAHODHA wa Zambia, Barbra Banda amesema mwonekano mdogo wa mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON) kunawanyima wachezaji fursa ya kuonekana duniani.

Banda anayekipiga Orlando Prides ya Ligi Kuu ya Wanawake Marekani alisema mashindano hayo yana wachezaji wengi wa Afrika wanaocheza Ulaya lakini hawapati matangazo yatakayowafikisha duniani.

Kwa mujibu wa Banda, changamoto za maandalizi ya mashindano hayo, ikiwamo mabadiliko ya ghafla ya tarehe kutoka Machi hadi Julai, pamoja na ukosefu wa matangazo ya kutosha katika miji mwenyeji, vimechangia kupunguza mwonekano wa WAFCON.

Pia kumekuwa na mkanganyiko kuhusu namna mashabiki wanavyoweza kutazama mechi hiyo, hali iliyopunguza hamasa na motisha ya mashindano.

“Kuna maskauti wengi hapa wanaotafuta wachezaji, kwa hiyo ikiwa mashindano hayatangazwi vizuri, watu wachache zaidi wataweza kutazama,” alisema Banda.

Nahodha huyo wa Copper Queens alisisitiza umuhimu wa WAFCON kuonyeshwa moja kwa moja katika nchi mbalimbali duniani ili kusaidia nyota wenye vipaji kuonekana moja kwa moja.

Alisema ikiwa mashindano hayo yatafikia hadhira ya kimataifa, watazamaji wengi zaidi watapata nafasi ya kuwafahamu wachezaji, makocha na vipaji vipya kutoka Afrika.

Banda aliongeza kuonyeshwa kwa mechi hizo duniani kunaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wachezaji chipukizi ambao bado hawajapata nafasi ya kutambulika katika soko la kimataifa.

“Ikiwa wataweza kupata nafasi ya kutazama mechi hizi, zitawapa faida wachezaji wengi vijana ambao bado hawajaonekana.”

Anaamini pia maendeleo ya ligi za wanawake barani Afrika yamechangia na kuongezeka kwa ushindani katika WAFCON.

“Ukiangalia ligi sasa barani Afrika, nadhani kila nchi imeendelea kuwa na ligi yake ya taifa. Kwa hiyo kiwango kinaweza kuwa sawa, kwa sababu unapocheza soka la kulipwa, linahitaji mambo mengi.”

Banda alisisitiza timu zote zilizofika Morocco hazijaja kushiriki kwa ajili ya kutimiza idadi, bali zinataka kushindana.

“Kila timu iko hapa kushindana, hakuna aliyekuja kushiriki tu, timu zimeboresha kiwango chake. Kwa hiyo ni vigumu kwangu kutabiri ni ipi itaibuka na ubingwa.”