De Gea anarudi Old Trafford
Muktasari:
- De Gea alirudi kwa mara nyingine Old Trafford kwa lengo la kuwaaga mashabiki wa klabu yake hiyo, akikutana pia ana viongozi ikiwamo Kocha aliyemleta, Sir Alex Ferguson.
MANCHESTER, ENGLAND: NDIYO hivyo. Taarifa zinasema mawasiliano ya siri yameanza baina ya mabosi wa Manchester United na David de Gea tangu timu hiyo ilipocheza na Fiorentina mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Old Trafford na huedna akarudi katika kikosi hicho dirisha hili kabla halijafungwa.
De Gea alirudi kwa mara nyingine Old Trafford kwa lengo la kuwaaga mashabiki wa klabu yake hiyo, akikutana pia ana viongozi ikiwamo Kocha aliyemleta, Sir Alex Ferguson.
Sasa kinachoelezwa ni Man United inaangalia uwezekano wa kumchukua kwa mkopo au kumnunua jumla De Gea ambaye na imearifiwa Mhispania huyo, 34, ana kifungu katika mkataba wake na Fiorentina kinachomruhusu kuondoka kwa kiasi kidogo cha fedha.
Mawasiliano hayo ya siri yameanza ikiwa ni wiki moja tangu mchezo huo wa kirafiki De Gea akiwa langoni kwa Fiorentina na baadaye alisema “njia zetu zinaweza kukutana tena.”
Taarifa za ndani zinaeleza, kabla ya mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Arsenal iliyopigwa jana, Kocha wa Man United, Ruben Amorim aliendelea kuwa na mashaka juu ya Andre Onana ambaye anaona bado hatoshi kuwa kipa wake namba moja.
Amorim alisema: “Ni kama wachezaji wengine. Wote lazima wapambanie nafasi yao. Siwezi kusema kama mtu mmoja ndiye namba moja.”
De Gea alicheza mechi 545 akiwa na Man United kati ya 2011 na 2023, akipanda nafasi ya saba kwenye orodha yao ya wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi katika timu hiyo.
Lakini kupungua kwa kiwango na mgogoro wa mkataba kulisababisha kuondoka kwake, kisha kocha wa zamani Erik ten Hag alipendekeza kusajiliwa kwa Andre Onana kutoka Inter Milan.
De Gea alikaa nje bila klabu kwa msimu wote wa 2023-24, kabla ya kutua Fiorentina ambako anaonekana kurudi katika kiwango chake.
Man United inamwona De Gea kama kipa ambaye hatowagharimu kiasi kikubwa cha pesa kuanzia usajli na mshahara kuliko makipa wengine ambao wapo sokoni kwa sasa.
Kipa huyu alipatiwa picha iliyowekwa kwenye fremu na Bruno Fernandes wakati wa mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu, ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mbali ya De Gea mashetani hao wekundu pia wanahusishwa na Emi Martinez kutoka Aston Villa, Gianluigi Donnarumma wa Paris Saint-Germain na John Victor wa Botafogo.
Emiliano Martinez wa Aston anahusishwa sana kuondoka baada ya msimu uliopita kumalizika kuonyesha ishara ya kuaga mashabiki hali iliyoibua tetesi kwamba anaondoka ingawa hadi sasa bado hilo halijatokea na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Donnarumma naye kwa sasa yupo sokoni anauzwa baada ya kocha Luis Enrique kuweka wazi kwamba hamhitaji katika kikosi chake kwa msimu huu.
Kipa huyu ambaye alionyesha kiwango bora msimu uliopita akiisaidia PSG kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu Ufaransa msimu uliopita.
Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani na PSG inahitaji kiasi kisichopungua Euro 40 milioni ili kumuuza.
Kipa John Victor wa Batafogo ameripotiwa kuzivutia timu nyingi ikiwemo Man United baada ya kiwango chake bora alichoonyesha katika michuano ya Kombe la Dunia kwa Klabu lililofanyika mwaka huu huko Marekani.