Dakika 17 bao 4, PSG kiboko
Muktasari:
- Baadhi ya mashabiki wa Villarreal walianza kuondoka uwanjani kabla ya dakika 20, baada ya PSG kufunga mabao manne ndani ya dakika 17 za mwanzo wa mchezo.
PARIS, UFARANSA: PARIS Saint-Germain (PSG) imeendeleza ubabe wake katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichakaza Villarreal kwa mabao 6-0, huku mabao nne yakifungwa ndani ya dakika 17 za kwanza katika mchezo ambao wenyeji walionekana kupoteza mwelekeo mapema.
Baadhi ya mashabiki wa Villarreal walianza kuondoka uwanjani kabla ya dakika 20, baada ya PSG kufunga mabao manne ndani ya dakika 17 za mwanzo wa mchezo.
Mabao hayo yalitokana kwa kiasi kikubwa na uzembe wa safu ya ulinzi ya Villarreal, iliyoshindwa kuhimili mashambulizi ya PSG ambayo msimu huu tayari imeifunga Barcelona na Manchester City mabao manne kila moja katika michuano hiyo.
Joao Neves alikuwa wa kwanza kutikisa nyavu baada ya kuunganisha mpira uliotokana na kona, kufuatia Villarreal kushindwa kuondoa hatari langoni mwao.
PSG iliendelea kuongeza presha na kupata bao la pili baada ya kipa Peter Gulacsi kufanya makosa katika kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma. PSG iliutwaa mpira na kuufikisha kwa Desire Doue, aliyefumua shuti lililojaa wavuni.
Dakika moja baadaye, Villarreal ilifanya kosa jingine iliponyang'anywa mpira wakati ikijaribu kuanzisha mashambulizi kutoka eneo lake la ulinzi, hali iliyompa Senny Mayulu nafasi ya kufunga bao la tatu kwa shuti lililomshinda Gulacsi.
Fabian Ruiz aliongeza bao la nne baada ya PSG kuurudisha mpira ndani ya eneo la hatari kwa kiungo huyo wa Hispania, aliyepiga shuti kali lililojaa katika kona ya karibu ya lango.
Ruiz alifunga bao lake la pili baada ya mapumziko, akionyesha ufundi kwa kumwacha beki aliyekuwa akimkaba akiwa chini kabla ya kuutumbukiza mpira wavuni na kumwacha Gulacsi bila majibu.
Ushindi huo ulipambwa na kinda mwenye umri wa miaka 17, David Boly, aliyepiga shambulizi kali kupitia upande wa pembeni kabla ya shuti lake kugonga mguu wa beki wa Villarreal na kuingia wavuni.
Matokeo hayo yanaifanya PSG kuongoza msimamo wa hatua ya ligi ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda mechi zote nne ilizocheza.
Mchezo wake unaofuata wa PSG ni dhidi ya Roma, Novemba 25.