Prime
Sayansi na ugomvi wa pacha wa P-Square
Agosti 2026 umekuwa mwezi mbaya zaidi kwa pacha wa kundi la muziki kutoka Nigeria, P-Square.
Pacha hawa ni Peter na Paul, ugomvi ambao pia unamhusisha kaka yao Jude ‘Engees’ ambaye alikuwa meneja wao wakati wa ukali wa kundi lao.
P-Square ni kundi la muziki wa kizazi kipya Nigeria, Afro Pop, ambalo lilitawala sana Afrika na duniani katikati ya miaka ya 2000.
Albamu yao ya Get Squared ya 2005 iliyokuwa na nyimbo kama Temptation na Bizy Body ziliichukua Afrika kwa mshangao mkubwa sana.
Baada ya hapo yakawa mangoma kwa mangoma na kuwafanya kuwa nyota wakubwa sana Afrika.
Wasanii hawa ni ndugu kutoka familia ya Okoye, Peter Okoye aka Mr P, Paul Okoye aka Rudeboy na kaka yao Jude ‘Engees’ Okoye ambaye alikuwa meneja wao.
Ukimuacha kaka yao, hawa wawili ambao ndio walikuwa wasanii ni pacha, kama nilivyoanza kuzungumzia huko juu.
Pacha ni watoto wanaofanana kiasi hujui kulwa yupi na doto yupi. Kwa kiingereza huitwa ‘Identical Twins’.
Kisayansi pacha hawa ni wa asili moja katika mchakato wa uzazi. Yaani mbegu moja ya baba ikagawangika mara mbili wakati wa kutunga mimba.
Pacha wa aina hii hufanana sana muonekano wao, na ni lazima wawe wa jinsi moja....yaani kama ni wanaume basi ni wote, na kama ni wanawake basi ni wote. Ni tofauti na pacha wengine ambao huwa ni mbegu mbili tofauti huingia wakati wa utungaji wa mimba. Hawa sio lazima wafanane na sio lazima wawe wa jinsi moja.
P-Square ni pacha-ndugu na leo nitakuletea uchambuzi wa kisayansi kutoka vyanzo mbalimbali kuonesha namna matatizo ya watu wa aina hii na kinachoendelea kwao.
Vita ya P-Square sio ya nani yuko sahihi baina yao bali ni yanayotokea yametokeaje, kwa kuwatumia Peter, Paul na Jude kama mfano halisi ili kuzisaidia familia zenye watu wa aina hii kutatua changamoto zinazoweza kuwatokea.
MKASA WAO
Mtafaruku baina yao ulianza muda mrefu hadi kundi lao likavunjika.
Mambo mengi yanaendelea baina yao wakirushiana maneno na kuvifaidisha vyombo vya habari, hasa vya udaku. Lakini kufikia Agosti mwaka huu hali ikawa mbaya zaidi.
Peter Okoye au Mr. P alitoa video yake aliyojirekodi akielezea mambo mengi sana yanayowagombanisha.
Video hiyo iliyokuwa na sehemu tano, ilimlenga zaidi kaka yao Jude ‘Engees’ Okoye aliyekuwa meneja wao kwamba alichepusha fedha kiasi cha dola milioni moja na laki mbili za Marekani, sawa na zaidi ya Sh3 bilioni, kutoka haki zao za mirabaha kupitia kampuni ya Northside Music huku yeye (Mr. P) akiondolewa kama mmoja wa watia saini.
Pia akaongeza kaka huyo alimtishia maisha juu ya jumba lao la kifahari wanalomiliki Marekani.
Mr. P alisema jumba hilo limebadilishwa umiliki na sasa linasomeka kama ni la Ifeoma, mke wa Jude.
Jude naye akatoa video ndefu alijibu hoja moja moja.
Kuhusu mapato ya mirabaha, akasema ilifuata maelekezo ambayo Mr P mwenyewe aliyatoa mwaka 2016...na hadi wakati huo hilo pia lilikuwa mahakamani.
Kuhusu lile jumba la Marekani, mke wa Jude, Ifeoma, akajitokeza na kukanusha kumilikishwa jumba hilo.
Hii ni familia ambayo imeamua kuyaweka hadharani matatizo yao ya ndani, mbele ya mamilioni ya watu.
YAMEFIKAJE HAPA
Kuyajua zaidi, turudi nyuma kidogo.
2003 - 2011 P-Square wanaibuka na kuwa kundi kubwa na maarufu zaidi la muziki kutoka Afrika kuishika dunia.
2013-2017
Mipasuko ikaanza kujitokeza juu ya ubunifu wa kazi na udhibiti wa pesa na mapato. Peter anajitoa kwenye kundi na kila mmoja anasimama kama msanii huru. Ndipo majina ya Mr P na Rudeboy yalipoanza.
2021
Tetesi juu ya kurudi kwa P-Square kama kundi zinazuma, lakini baadaye Peter anaibuka na kusema ni za uongo.
2024
Peter akafungua malalamiko rasmi kwenye tume ya taifa ya uchumi na uhalifu wa kifedha - Economic and Financial Crimes Commission (EFCC) ya Nigeria kutaka ufanyike uchunguzi juu ya mirahaba ya kazi zao baada ya kugundua upigaji wa kaka yao Jude na mkewe kupitia kampuni ya Northside Music. Jude anakamatwa lakini baadaye anaachiwa kwa dhamana...lakini akaunti zake zote zinapigwa tanji kupisha uchunguzi.
2025-2026
Kesi inaendelea kwenye mahakama za Lagos. Peter anarekodi video yenye sehemu tano kumshambulia kaka yake Jude, naye anajibu mapigo. Ndugu waliojenga himaya yao sasa wanapambana hadharani kuiangusha.
NI MAMBO YA KISAYANSI
Badala ya kulitazama hili suala kwa jicho la kuwaona Peter, Paul na Jude tu, ni vyema kuelewa maugomvi ya ndugu kama haya yana asili ya kisayansi.
Sayansi inayohusika na mambo haya inaitwa Anthropolojia.
Ni sayansi inayochunguza na kusoma binadamu kwa upande wa baiolojia, jamii, na utamaduni wao, kuanzia nyakati za kale hadi sasa.
Watalaamu wa sayansi hii wananyooshea kidole chao kwa kitu kinachoitwa nadharia ya uwekezaji wa wazazi (Parental investment theory).
Hii ni dhana ya mageuzi ya kibaolojia ya mwili iliyotanbulishwa na mwanayansi aliyeitwa Robert Trivers mwaka 1972.
Hii ni dhana inayoelezea namna gani muda, nishati, na raslimali ambazo wazazi huwekeza katika malezi ya watoto wao zinavyokuja kuathiri tabia za baadaye za watoto wao kuanzia mahusiano, kuchagua wenza wao na tofauti za jinsi.
Nadharia hii hutabiri kwamba jinsi (baba au mama) inayowekeza zaidi kwa watoto wao ndio itakayotawala hisia za baadaye za mtoto.
Baba akiwekeza zaidi kwa mtoto, atatawala kwa asilimia kubwa hisia, mienendo, matendo na tabia za mwanaye...hali kadhalika mama.
Katika familia za kawaida, uwekezaji unaozungumziwa hapa ni upendo, na huduma, lakini kwa familia ya P-Square, ikawa tofauti.
Maisha yao yakaathiriwa na ushindani baina yao katika sanaa na kuelekezewa kwenye kitu kilichokuja kushikilia hatma yao; chapa ya muziki na biashara ya mabilioni ya pesa iliyosimama na urithi wa pamoja.
Ndugu mmoja, kwa sakata hili ni Jude aliyekuwa meneja wao, anapotuhumiwa kujichotea urithi huu wa pamoja, inaonekana ni kitisho cha maisha kwa wengine. Hiki ndicho kinachowatokea pacha hawa.
MTEGO WA MAPACHA
Kwenye tamaduni nyingi pacha huchukuliwa kama kitu kimoja. Kwa P-Square hii ilienda hadi kibiashara.
Kwa wakati wao wote wakiwa kileleni, tasnia ya muziki na burudani iliwachukulia kama kitu kimoja.
Walitakiwa wavae sare, watembee sare, na hata matamasha yao wayafanye kama msanii mmoja, sio kundi.
Lakini pesa zilipoingia zikaanza kutengeneza presha kwa kila mmoja wao kusimama kama na kujenga utambulisho wake.
Hizi vita za sasa baada ya kundi kuvumilia sio za kimuziki zaidi bali kila mmoja akipambana kutambulika kama ni mkali dhidi ya mwenzake.
Hii inathibitishwa na barua ya Mr. P (Peter) aliyoiandika kumjibu Rudeboy (Paul) mwaka 2024.
Ndugu yangu mpendwa Paul
Kama ambavyo nimekwambia mara kadhaa, sipo kwenye mashindano yoyote na wewe au na mtu mwingine yeyote.
Lakini kukuona mara kadhaa ukifanya mahojiano na kudogosha jitihada zangu kwenye kundi letu tulilolianzisha na kulikuza pamoja, inasikitisha sana.
Kwenye mahojiano yako ya hivi karibuni ulidai ulitunga asilimia 99 ya nyimbo za P-Square na kusema wimbo wetu wa EjeaJo ambao niliutunga mimi na tuliuimba na TI eti ulifeli.
Kupitia barua hii utaona kabisa kwamba baina yao kulikuwa na mapambano ya nani mkali.
KAKA YAO AKAGEUKA MZIGO
Kwa tamaduni za kiafrika, ikiwemo Nigeria wanakotoka P-Square, mpangilio wa kuzaliwa ndio mpangilio wa kimamlaka na amri.
Ndugu mkubwa hulelewa kuwaongoza wadogo zake...ndivyo ilivyokuwa kwa kaka yao, Jude.
Alisimama kama kiongozi wa Peter na Paul, kiutamaduni kama kaka na kikazi kama meneja.
Lakini wadogo zake walipokuja kuwa ndio nguzo kuu ya mapato (wao kama wasanii), ule mpangilio wa kiasili (kwamba kaka ana mamlaka yote) ukaanza kuhojiwa.
Kukosa imani katika masuala ya fedha kulipoibuka kwa wadogo, heshima ya kiutamaduni kwa kaka ikapotea.
HOJA YA TATU KATIKA UTATU
Tutumie nadharia ya mtaalamu wa masuala ya kifamilia, Murray Bowel, mfumo wa familia, kujadili suala hili kutoka kwenye sayansi ya anthropolojia na kuja kwenye sayansi ya saikolojia.
Katika familia ya P-Square, Jude, alikuwa hoja ya tatu katika utatu wao akiwemo Peter na Paul.
Utatu (familia) wa aina hii ukiwa madhubuti, nguzo mbili (ndugu wawili) huungana dhidi ya nguzo ya tatu.
Na nguzo ya tatu ikiona hivyo, huchukua hatua za kujihami...ndicho kilichotokea kwa Jude dhidi ya wadogo zake.
Tuhuma za wazi za Peter ikiwemo zilizomuingiza Paul kwenye kesi ya Jude mbele ya time ya EFCC, inadhihirisha wazi hilo.
Hakika kuna mengi sana ndani ya mgogoro wa P-Square ambao ukiangalia tu kwa jicho la sanaa huwezi kupatia majibu yake sahihi.
Inabidi uchanganye sayansi na utamaduni ndani yake ndipo uje uone kilichopo ndani ya sanaa yao.