Clippers yamtema Chris Paul NBA
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40, aliambiwa aondoke kikosini na kureshwa nyumbani na Clippers usiku wa Jumatano katikati ya ziara ya michezo mitano ugenini.
LOS ANGELES, MAREKANI: LOS Angeles Clippers wameachana na Chris Paul katika mazingira yaliyoacha maswali kwa mashabiki wanaofuatilia Ligi ya Kikapu Marekani (NBA).
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40, aliambiwa aondoke kikosini na kureshwa nyumbani na Clippers usiku wa Jumatano katikati ya ziara ya michezo mitano ugenini.
“Tunaachana na Chris na hatakuwa tena na timu hii. Tutashirikiana naye kuhusu hatua inayofuata ya maisha yake ya kitaaluma,” Clippers ilisema katika taarifa kupitia mwandishi wa habari za NBA, Chris Haynes.
“Chris ni gwiji wa Clippers ambaye amekuwa na historia bora. Nataka kuweka jambo moja wazi, hakuna anayemlaumu Chris kwa matokeo duni ya kikosi hicho.
“Tunakubali kuwajibika kwa rekodi tuliyonayo sasa. Kuna sababu nyingi kwa nini tumekuwa tukihangaika kusaka matokeo bora. Tunashukuru kwa kuishi na Chris katika klabu yetu.”
Uamuzi wa kushangaza wa Clippers kuvunja uhusiano na mkongwe huyo ulimshangaza hata Paul mwenyewe ambaye alichapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akisema: “Nilichojua tu ni kwamba narudishwa nyumbani.”
Mchezaji huyo ambaye mara 12 amechezea kikosi cha NBA All-Star alidai Novemba kwamba msimu huu ungekuwa wa mwisho kwake.
Alidai angeachana na Clipperss ambako alitumia miaka sita kuanzia 2011–17 akiwa sehemu ya kikosi hicho pamoja na mastaa wengine kama Blake Griffin na DeAndre Jordan.
Lakini, Clippers sasa wakiongozwa na Kawhi Leonard na James Harden wamekuwa wakipata ushindi kwa shida wakiwa na rekodi ya ushindi mara tano katika mechi 16 wakishika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Kanda ya Magharibi.