Ciro Messi aiga ustadi wa baba yake
Muktasari:
- Ciro ni sehemu ya mfumo wa vijana wa klabu hiyo pamoja na kaka zake Mateo na Thiago na katika picha za video zilizosambaa mtandaoni akiwa amevaa jezi namba 10 kama baba yake
MIAMI, MAREKANI: MTOTO wa staa wa Inter Miami, Lionel Messi mwenye umri wa miaka sita, Ciro, ameonekana kuiga mtindo wa baba yake kwa kufunga bao la kuvutia katika mchezo wa akademi ya timu hiyo ya baba'ke.
Ciro ni sehemu ya mfumo wa vijana wa klabu hiyo pamoja na kaka zake Mateo na Thiago na katika picha za video zilizosambaa mtandaoni akiwa amevaa jezi namba 10 kama baba yake, anaonekana kuupokea mpira akiwa ndani ya nusu yake ya uwanja kabla ya kuwapita wachezaji watatu wa timu pinzani kwa ustadi mkubwa na kisha kufunga kwa shuti lililotinga moja kwa moja kwenye kona moja chini ya lango.
Namna alivyokuwa akikokota mpira ilifanana na mzazi wake, jambo ambalo mashabiki wengi mitandaoni walionekana kuvutiwa na kipaji chake.
Shabiki mmoja aliandika: “Ndiyo, huyo kweli ni mtoto wa Messi. Huwezi kufundisha kwa urahisi ule ustadi wa kushusha mabega akiwa anakokota mpira.” Mwingine aliongeza: “Angalia namna alivyomalizia nafasi ile, mtoto huyu anacheza kama baba yake kabisa.”
Bao la Ciro limefananishwa zaidi na lile maarufu ambalo Messi aliifungia Barcelona dhidi ya Getafe 2007 wakati huo akiwa na miaka 19 alipoanza kukimbia kutoka ndani ya nusu yake ya uwanja kabla ya kuwapita wachezaji kadhaa wa wapinzani, kisha akaingia eneo la hatari akamzunguka kipa Luis Garcia na kuusukuma mpira wavuni.
Bao hilo lilimfanya Messi kulinganishwa na gwiji wa Argentina, Diego Maradona. Katika kipindi chake cha miaka 18 akiwa na kikosi cha Barcelona, Messi alifunga mabao 672 kwa miamba hiyo ya Hispania.
Kwa sasa Messi anacheza Ligi Kuu Hispania akiwa na Inter Miami aliyojiunga nayo 2023 akitokea PSG ambako alicheza kwa misimu miwili. Tangu ajiunge nahodha huyo amefunga mabao 34 na kutoa pasi 18 za mabao katika michezo 39 ya mashindano yote.