Chelsea yahitaji zaidi ya kipa kutwaa ubingwa
Muktasari:
- Martinez, 33, aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza baada ya kocha Xabi Alonso kumwamini tangu dakika ya kwanza, lakini mchezo huo ulionyesha wazi kuwa ujio wake pekee hauwezi kutatua matatizo ya Chelsea kwenye safu ya ulinzi.
LONDON, ENGLAND: MASAA matano tu baada ya Chelsea kuthibitisha usajili wa kipa Emiliano Martinez, nyota huyo alijikuta akicheza mechi yake ya kwanza akiwa Stamford Bridge dhidi ya Brighton.
Martinez, 33, aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza baada ya kocha Xabi Alonso kumwamini tangu dakika ya kwanza, lakini mchezo huo ulionyesha wazi kuwa ujio wake pekee hauwezi kutatua matatizo ya Chelsea kwenye safu ya ulinzi.
Martinez amesema alikuwa "fiti na tayari" kucheza licha ya usajili wake wa Pauni 7.5milioni kutoka Aston Villa kuthibitishwa muda mfupi kabla ya mchezo kuanza.
Hata hivyo, mlinda mlango huyo wa Argentina tayari alikuwa amefanya mazoezi na wachezaji wenzake wapya baada ya kukamilisha uhamisho wake kabla ya muda wa mwisho wa usajili Ijumaa, huku Chelsea ikichelewesha tangazo rasmi kwa sababu za kimkakati za masoko.
Tofauti na Robert Sanchez, ambaye alikosolewa baada ya kuhusika moja kwa moja kwenye bao la kwanza na kwa kiasi fulani la pili katika ushindi wa Chelsea wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham Jumatatu, Martinez hakubebeshwa lawama kubwa kwa mabao matatu waliyofungwa dhidi ya Brighton.
Hata hivyo, Chelsea sasa imefungwa mabao matano katika michezo miwili, ingawa imeendelea kuwa na rekodi ya kushinda kwa asilimia 100 kutokana na ubora wa safu yake mpya ya ushambuliaji.
"Ushindi ni ushindi. Najua haikuwa mechi nzuri, lakini mwishowe tunahitaji kushinda na kuendelea," amesema Martinez baada ya mchezo huo alipokuwa akizungumza na Sky Sports.
"Nipo hapa kwa sababu. Wachezaji watatu wa mbele ni bora sana. Tunapokwenda mbele, tunaweza kuumiza timu pinzani. Tulipata nafasi nyingi za kumaliza mchezo. Cole Palmer na Joao Pedro walipata nafasi za kuufunga mchezo, lakini nyuma tunahitaji kupunguza idadi ya mabao tunayofungwa."
GIVEN: MARTINEZ NI USAJILI BORA
Kipa wa zamani wa Ligi Kuu England, Shay Given, ambaye sasa ni mchambuzi wa televisheni, amemsifu Martinez akisema ni "usajili bora".
"Martinez ni mchezaji wa kuvutia. Amejiunga hivi karibuni tu, lakini Alonso ameona hakuna haja ya kusubiri, amemuingiza moja kwa moja kwenye kikosi," Given aliiambia BBC Sport.
"Kocha anaonekana wazi kuwa alihitaji kipa mwenye kiwango na haiba kama yake."
Hata hivyo, pamoja na Chelsea kuibuka na ushindi huo wa mabao 4-3 katika mchezo uliokuwa na vurugu nyingi za kimchezo, Alonso atalazimika kutafuta namna ya kukifanya kikosi chake kitawale mechi ikiwa kweli kinataka kuingia kwenye mbio za ubingwa.
Mtihani mwingine mkubwa unawasubiri dhidi ya Arsenal katika mchezo wao ujao.
Martinez ni mshindi mara mbili wa tuzo ya Kipa Bora wa FIFA, huku akiwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Argentina yaliyowapa Kombe la Dunia mwaka 2022 na Aston Villa iliyotwaa Europa Ligi mwezi Mei.
"Nimefurahishwa na namna alivyoanza," amesema Alonso baada ya ushindi dhidi ya Brighton.
"Amekuwa hapa kwa saa 48, hivyo sasa tutakuwa na wiki nzima ya kujiandaa kwa mchezo unaofuata. Kadiri siku zinavyokwenda, tutaendelea kuona uwepo wake kwa sababu ana haiba na uwezo wa kuleta ushawishi mzuri pamoja na kujenga uhusiano chanya na wachezaji wenzake."
SANCHEZ AANZA KUPOTEZA NAFASI
Kwa upande mwingine, Robert Sanchez hakuwa ameshinda taji lolote kubwa kabla ya kujiunga na Chelsea akitokea Brighton kwa ada ya Pauni 25milioni mwaka 2023.
Kwa kuangalia takwimu na uwezo wake uwanjani, Sanchez amekuwa akilinganishwa vizuri na makipa wengi, jambo lililomfanya mkuu wa makipa Chelsea, Ben Roberts, kuendelea kumuamini kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Sanchez amekuwa akifanya makosa mara kwa mara, hasa katika msimu wa 2024-25, hali iliyomfanya apoteze kwa muda nafasi yake kwa Djordje Petrovic, ambaye sasa yupo Bournemouth, na Filip Jorgensen, anayekipiga Strasbourg.