Cheki Feb 5 ilivyoleta mastaa wa soka duniani

Muktasari:
- Ni hivi. Februari 5 ni siku ambayo ilishuhudia mastaa matata kabisa kwenye mchezo wa soka wakiwa wamezaliwa.
LONDON, ENGLAND: KAMA ulizaliwa Februari 5, unacheza soka na huna maajabu, basi achana na boli, kwani hiyo itakuwa kazi isiyokuhusu.
Ni hivi. Februari 5 ni siku ambayo ilishuhudia mastaa matata kabisa kwenye mchezo wa soka wakiwa wamezaliwa.
Kuna mastaa wengi wa soka waliozaliwa siku kama hiyo na wametamba na wengine wanaendelea kutamba kwenye mchezo huo.
Unataka kuwafahamu?
Cristiano Ronaldo - Februari 5, 1985
Mshindi mara tano wa Ballon d'Or, Cristiano Ronaldo leo, Jumatano amesherehekea kutimiza umri wa miaka 40. Anatimiza umri huo huku akiwa mmoja wa wanasoka mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye mchezo huo, ambapo kwa sasa anakipiga katika kikosi cha Al Nassr ya Saudi Arabia. Ronaldo amefanya kila kitu cha maajabu kwenye mchezo wa soka akipita katika timu kibao ikiwamo Manchester United, Juventus na Real Madrid.
Neymar - Februari 5, 1992
Aliweka rekodi ya dunia kwenye uhamisho wakati aliponaswa na Paris Saint-Germain akitokea Barcelona kwa ada ya Pauni 198 milioni. Baada ya kutamba kwenye soka la Ulaya, Neymar alipata dili la pesa nyingi kwenda kuitumikia miamba ya Saudi Arabia, Al Hilal, ambayo ilikuwa ikimlipa mshahara wa kibosi kwelikweli. Majeraha ya mara kwa mara yametibua maisha ya Neymar huko Saudia na hivyo mkataba wake kuvunjwa. Amerudi klabu yake ya zamani ya Santos.
Carlos Tevez - Februari 5, 1984
Straika wa boli, Carlos Tevez hajawahi kuwa mtu wa mashaka linapokuja suala la kuujua mpira wa miguu. Ametamba kwenye timu kibao, ikiwamo mahasimu wa Ligi Kuu England, Manchester United na Manchester City, kabla ya kwenda kuitumikia pia Juventus. Boca Juniors ni mahali penye kumbukumbu nyingi tamu za staa huyo wa Kiargentina, ambaye uchezaji wake umeacha alama kubwa kwa vijana waliokuwa wakiibukia kwenye soka.
Gheorghe Hagi - Februari 5, 1965
Staa wa zamani wa Barcelona, Real Madrid na Steaua Bucharest, aliyekuwa fundi wa pasi za mwisho na kutengeneza nafasi nyingi za mabao, Gheorghe Hagi ni mchezaji mwenye hadhi kubwa sana huko Romania. Alichezea timu yake ya taifa mechi 124 kati ya 1983 na 2000 na mambo matamu aliyofanya kwenye timu yake ya taifa yanamfanya mashabiki kuamini anastahili heshima ya juu. Anaripotiwa kuwa mmiliki wa timu ya Viitorul Constanta ya huko Romania.
Adnan Januzaj - Februari 5, 1995
Januzaj alianza maisha yake ya soka klabuni FC Brussels, lakini alikwenda kujiunga na Anderlecht akiwa na umri wa miaka 10 mwaka 2005. Kisha aliondoka kwenye timu hiyo kwenda Manchester United akiwa na umri wa miaka 16, Machi 2011. Kwenye kikosi cha Man United ndiko alikofanya balaa kubwa uwanjani na kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na soka lake. Kwa sasa winga huyo anachezea Las Palmas kwa mkopo, akitokea Sevilla.
Wengine waliozaliwa Februari 5
Soka imeshuhudia mastaa wengi wa maana waliozaliwa siku hiyo ya Februari 5. Miongoni mwao ni pamoja na Billy Sharp, Sven-Goran Eriksson, Jordan Rhodes na Vedran Corluka kwa kuwataja kwa uchache.