Cheki bili za klabu za EPL zinavyolipa mastaa wake kwa mwaka
Muktasari:
- Na kinachovutia, vinara wa sasa wa ligi hiyo, Liverpool wenyewe wanashika namba tano kwa kulipa mishahara mikubwa kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu England 2024-25 unaohusu bili za mishahara za klabu kwenye ligi hiyo kwa mujibu wa Capology.
LONDON, ENGLAND: MABINGWA wa Ligi Kuu England, Manchester City ndiyo wanaotumia pesa nyingi kulipa mishahara kuliko nyingine zote ze ligi.
Na kinachovutia, vinara wa sasa wa ligi hiyo, Liverpool wenyewe wanashika namba tano kwa kulipa mishahara mikubwa kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu England 2024-25 unaohusu bili za mishahara za klabu kwenye ligi hiyo kwa mujibu wa Capology.
Man City ya Pep Guardiola inapambana kunyakua taji lake la tano mfululizo kwenye Ligi Kuu England msimu huu, wakati ikiachwa nyuma na Liverpool kwa pointi 12, huku vijana hao wa Arne Slot wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Baada ya kuanza msimu vibaya, Man City imeongeza bajeti kwenye bili ya mishahara baada ya kuwasajili Abdukodir Khusanov, Vitor Reis na Omar Marmoush, ambapo sasa wanafanya bili ya mishahara ya klabu hiyo kufikia Pauni 224 milioni.
Msimu uliopita, Manchester United ndiyo iliyokuwa namba moja kwa kuwa na bili kubwa ya mishahara. Lakini, miamba hiyo ya Old Trafford imepunguza watu kwenye kikosi ikiwamo Donny van de Beek, Raphael Varane na Anthony Martial na kushusha bili ya mishahara, ambapo sasa inatumia Pauni 34 milioni pungufu ya wapinzani wao Man City kwa mwaka. Kwa msimu huu, Man United inashika namba mbili.
Chelsea ipo nafasi ya tatu na hiyo haishangazi kutokana na kikosi kipana cha kocha Enzo Maresca, huku Arsenal ikishika namba nne kwa maana kwamba inalipa mastaa wake mishahara mikubwa kuliko wapinzani wao wengine wa Big Six, Liverpool na Tottenham Hotspur. Miamba mingine ukiondoa vigogo hao wa Big Six yenye bili kubwa za mishahara ni Aston Villa na Newcastle United ambazo zimevuka bili ya mishahara ya Pauni 100 milioni na hilo limeonekana ndani ya uwanja baada ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2023-24 na 2022-23 mtawalia.
Kwingineko, Everton ni miongoni mwa timu zinazolipa mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu England kuzidi timu za Bournemouth, Brighton, Fulham na Wolves – ambazo kwa msimu uliopita zote zilikuwa juu yao kwenye msimamo wa bili kubwa za mishahara kwenye ligi.
Ipswich Town iliyopanda daraja msimu huu ndiyo inayoshika nafasi ya mwisho kwa kuwa na bili ndogo zaidi, ikitumia Pauni 34 milioni kwa mwaka.
MSIMAMO WA LIGI KUU ENGLAND KWA KUZINGATIA BILI ZA MISHAHARA YA WACHEZAJI KWA MWAKA
1. Man City – Pauni 224,640,000
2. Man United – Pauni 190,320,000
3. Chelsea – Pauni 174,070,000
4. Arsenal – Pauni 172,146,000
5. Liverpool – Pauni 128,804,000
6. Aston Villa – Pauni 108,836,000
7. Newcastle – Pauni 105,352,000
8. Tottenham – Pauni 104,806,000
9. West Ham United – Pauni 92,560,000
10. Everton – Pauni 71,422,000
11. Fulham – Pauni 68,406,000
12. Crystal Palace – Pauni 67,314,000
13. Nottingham Forest – Pauni 66,456,000
14. Leicester City – Pauni 65,416,000
15. Brighton – Pauni 59,202,000
16. Wolves – Pauni 55,562,000
17. Bournemouth – Pauni 50,544,000
18. Southampton – Pauni 50,206,000
19. Brentford – Pauni 42,250,000
20. Ipswich Town – Pauni 34,996,000