Carrick aandaa mbinu tatu kuiteka Hull City EPL
Muktasari:
- Mashetani Wekundu wana rekodi nzuri dhidi ya Hull City, maarufu kama Tigers, huku pia wakiwa na historia nzuri wanapokutana na timu zilizopandishwa daraja katika mchezo wa kwanza wa msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United itaanza safari yake ya msimu mpya wa Ligi Kuu England kwa kuikabili Hull City katika mchezo wao wa kwanza wa msimu utakaopigwa leo Jumamosi muda wa chakula cha mchana.
Mashetani Wekundu wana rekodi nzuri dhidi ya Hull City, maarufu kama Tigers, huku pia wakiwa na historia nzuri wanapokutana na timu zilizopandishwa daraja katika mchezo wa kwanza wa msimu.
Hata hivyo, historia hiyo haitakuwa na maana kubwa siku ya mchezo, kwani kikosi cha Michael Carrick kinahitaji kutumia mbinu sahihi ili kuhakikisha kinapata pointi zote tatu.
SUBIRA
Jambo la kwanza ambalo Manchester United italazimika kuwa nalo ni subira.
Kuna uwezekano mkubwa Hull City ikatumia mfumo wa kujilinda kwa wachezaji wengi nyuma, yaani 'low block', na kuiacha Manchester United ikiwa na muda mwingi wa kumiliki mpira.
United imekuwa ikipata changamoto katika michezo ya aina hiyo katika kipindi cha hivi karibuni. Kikosi hicho kimeonekana kufanya vizuri zaidi kwenye mechi ambazo kinapata nafasi ya kutumia mashambulizi ya haraka, kubadilisha kasi na kuwashambulia wapinzani kupitia 'counter-attack'.
Carrick amejaribu kuijenga United yenye mchezo wa kumiliki mpira zaidi katika maandalizi ya msimu huu, na eneo la kiungo litakuwa muhimu sana katika utekelezaji wa mpango huo.
Andrey Santos, Youri Tielemans na Bruno Fernandes wote watakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha United inaendelea kumiliki mpira huku wakitafuta mianya ya kuipasua safu ya ulinzi ya Tigers.
MABEKI WA PEMBENI
Manchester United, kama ilivyo kwa timu nyingi, huonekana kuwa na nguvu na uhai zaidi inapochezesha mpira kwa malengo na kuusambaza katika maeneo mbalimbali ya uwanja.
Mashetani Wekundu wanapokuwa katika kiwango chao bora, mara nyingi mabeki wa pembeni huwa sehemu muhimu ya mashambulizi.
Kwa sababu hiyo, Luke Shaw pamoja na Diogo Dalot au Noussair Mazraoui watakuwa na jukumu la kutafuta mpira, kupanda mbele na kufanya mbio za pembeni ili kutoa chaguo la 'overlap' kwa wachezaji kama Matheus Cunha, Bryan Mbeumo au Amad ambao watakuwa wakicheza pembeni.
Ushiriki huo wa mabeki unaweza kuwa muhimu hasa iwapo Hull itaamua kujilinda kwa wachezaji wengi katikati. Kwa kuwapeleka mabeki mbele, United inaweza kulazimisha safu ya ulinzi ya Tigers kutanuka na hivyo kuacha nafasi ambazo washambuliaji wanaweza kuzitumia.
MSHAMBULIAJI HATARI
Kwa mujibu wa The Athletic, Hull City ilimtumia kwa kiasi kikubwa mshambuliaji mwenye nguvu za mwili, Oli McBurnie, katika msimu uliopita wa Championship.
Ingawa bado haijulikani ni kwa namna gani Hull itacheza baada ya kupanda daraja na kuingia Ligi Kuu, ni jambo la kimantiki kutarajia kwamba baadhi ya mbinu hizo zinaweza kuendelea kutumika.
Hilo linaweza kumfanya Harry Maguire kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika safu ya ulinzi ya United, hasa kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za kimwili ambazo McBurnie anaweza kuleta.
Maguire ana baadhi ya mapungufu katika mchezo wake, lakini eneo ambalo anaonekana kuwa bora zaidi ni katika mapambano ya kimwili dhidi ya washambuliaji wenye nguvu pamoja na kutawala mipira ya juu.
Kwa hiyo, iwapo Hull itatumia mipira mirefu na kumtafuta McBurnie, uwezo wa Maguire katika mapambano ya angani unaweza kuwa silaha muhimu kwa United.
MSIMU ULIOPITA
Msimu wa Ligi Kuu England ulianza jana, siku 33 baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia, ukiwa umebeba simulizi na maswali mengi kama ilivyo kawaida.
Maswali hayo yatahitaji miezi tisa yenye drama nyingi kabla ya kupata majibu.
Hata hivyo, baadhi ya dalili zinaweza kupatikana katika takwimu za msimu uliopita. Ingawa vikosi vya timu mbalimbali vimebadilika kwa kiwango fulani, bado kuna wachezaji na msingi wa kutosha uliosalia ambao unaruhusu takwimu za msingi za msimu uliopita kutumika katika kufanya makadirio ya msimu huu.
Mfano mzuri ni Wolverhampton Wanderers, ambayo kabla ya msimu uliopita ilikuwa ikitoa dalili kupitia takwimu zake za msingi kwamba ilikuwa katika hatari ya kushuka daraja kwa miaka kadhaa.
Kwa upande mwingine, takwimu za Bournemouth zilionyesha kwamba timu hiyo ilikuwa na uwezo wa kupigania nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
DALILI HIZO MBILI HATIMAYE ZILITIMIA.
Wolves ilishuka daraja, huku Bournemouth ikimaliza katika nafasi ya sita.
Kwa Manchester United, hilo linaonyesha kwamba licha ya mchezo wa kwanza wa msimu kuamua pointi tatu pekee, namna timu itakavyocheza, takwimu zake na mwenendo wa msingi vinaweza kutoa picha muhimu kuhusu kinachoweza kutokea katika miezi tisa ijayo.
MECHI NYINGINE
Ipswich Town vs Sundeland
Nottigham Forest vs Leeds
Brentford vs Spurs
Everton vs Palace