Carlos Forbs mrithi wa Ronaldo Ureno
Muktasari:
- Forbs, mwenye umri wa miaka 22, alifanya mambo makubwa ndani ya dakika 11 tu baada ya kuingia akitokea benchi, akifunga bao lililoibua kumbukumbu za aina ya magoli ambayo Ronaldo alikuwa akifunga katika miaka yake ya mwanzo akiwa Manchester United.
LISBON, URENO: JE, Ureno imepata mrithi wa Cristiano Ronaldo? Hilo ndilo swali linalozidi kuzungumzwa baada ya kinda Carlos Forbs kuonyesha kiwango bora na kufunga bao la ushindi katika mchezo dhidi ya Wales Jumanne.
Forbs, mwenye umri wa miaka 22, alifanya mambo makubwa ndani ya dakika 11 tu baada ya kuingia akitokea benchi, akifunga bao lililoibua kumbukumbu za aina ya magoli ambayo Ronaldo alikuwa akifunga katika miaka yake ya mwanzo akiwa Manchester United.
Akiwa upande wa kulia wa uwanja, Forbs alionyesha kasi, akimkabili beki Ben Davies aliyekuwa akirudi nyuma, kabla ya kuingia ndani kwa mguu wake wa kushoto na kupiga shuti lililojaa wavuni.
Bao hilo limeongeza mjadala kuhusu uwezekano wa mshambuliaji huyo kuwa mmoja wa wachezaji watakaobeba jukumu la kuiongoza Ureno baada ya zama za Ronaldo.
Kwa miaka 20, jezi namba saba ya timu ya taifa ya Ureno ilikuwa ikivaliwa na Ronaldo, ambaye aliirithi kutoka kwa gwiji Luis Figo.
Hivyo, jezi hiyo ina historia kubwa katika soka la Ureno na mchezaji atakayepewa jukumu la kuivaa kwa kudumu atakuwa na jukumu kubwa la kuendeleza heshima yake.
Kwa sasa Forbs bado hajathibitishwa kuwa mrithi wa kudumu wa jezi hiyo, huku taarifa kutoka ndani ya kambi ya Ureno zikieleza kuwa bado kuna ushindani kati yake na Rafael Leao.
Leao ndiye aliyekuwa akitarajiwa kuvaa jezi hiyo katika mechi za mapumziko ya kimataifa, lakini alikosa nafasi hiyo kutokana na majeraha.
Hata hivyo, baada ya kiwango chake dhidi ya Wales, jina la Forbs limekuwa gumzo kwa mashabiki, baadhi yao wakianza kumuita 'CF7'.
Gazeti maarufu la michezo la Ureno, O Jogo, limemtaja kama shujaa mpya wa taifa hilo.
SAFARI YAKE
Forbs alizaliwa Sintra, Ureno, katika familia yenye asili ya Guinea-Bissau. Alianza kucheza soka la futsal kabla ya kujiunga na akademi ya Sporting Lisbon, klabu ambayo pia ilimlea Ronaldo katika hatua za mwanzo za maisha yake ya soka.
Akiwa na umri wa miaka 11, familia yake ilihamia England na haikuchukua muda mrefu kabla ya Manchester City kumchukua katika akademi yake.
Alitumia miaka minane katika mfumo wa vijana wa City na kutajwa kuwa miongoni mwa vipaji vilivyokuwa na matumaini makubwa.
Msimu wa 2022/23, alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Premier League 2 baada ya kufunga mabao 29 na kutoa pasi 18 za mabao katika mashindano yote.
Forbs alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao mengi katika mchezo mmoja, ikiwamo mechi ambayo aliifunga Manchester United mabao manne.
Wakati huo alikuwa akionekana kuwa karibu kujiunga na kikosi cha kwanza cha Pep Guardiola, huku wachezaji kama Kyle Walker na Bernardo Silva wakitajwa kumkaribisha vizuri katika mazoezi ya timu kubwa.
Hata mshambuliaji Erling Haaland aliwahi kuvutiwa na uwezo wake baada ya kutazama mkusanyiko wa mabao yake.
"Je, huyo ni Carlos? Nimekuwa nikifanya mazoezi na vijana hawa mara nyingi. Carlos ni mzuri," amesema Haaland.
Pamoja na kiwango hicho, Forbs hakupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha City kutokana na ushindani mkubwa wa nafasi.
Mwaka 2023 aliamua kuondoka na kujiunga na Ajax ya Uholanzi kwa ada ya uhamisho ya pauni 17 milioni.
Akizungumza na chombo cha habari cha AD Oktoba 2023, wakati huo akiwa bado anajulikana kwa jina la Carlos Borges, alieleza kuwa alihitaji mazingira ambayo yangempa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.
Amesema Manchester City ilikuwa na wachezaji wengi wenye uwezo, hivyo akaona kuhamia Ajax kungeongeza nafasi yake ya kuonyesha kipaji.
Hata hivyo, safari yake Uholanzi haikuwa kama alivyotarajia.
Katika msimu wake wa kwanza hakuwa chaguo la kudumu, huku msimu uliofuata akipelekwa kwa mkopo Wolverhampton Wanderers.
Alicheza mechi 10 za Ligi Kuu England akiwa Wolves, lakini hakufanikiwa kupata nafasi kubwa ya kujidhihirisha.
Mabadiliko ya kocha kutoka Gary O'Neil kwenda Vitor Pereira pia yaliathiri nafasi yake baada ya mfumo mpya wa 3-4-2-1 kutegemea zaidi mabeki wa pembeni wanaopanda kushambulia.
AJAX YAMTEMA
Mambo yalizidi kuwa magumu mwaka 2025 baada ya Ajax kuamua kutomuhitaji tena.
Mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, Alex Kroes, aliripotiwa kuwajulisha wachezaji saba kupitia WhatsApp kuwa hawakuwa tena sehemu ya mipango ya timu na hawakuruhusiwa kutumia baadhi ya maeneo ya mazoezi wakati kikosi cha kwanza kikiwa kinatumia.
Miongoni mwa wachezaji hao alikuwa pia Chuba Akpom, aliyewahi kucheza Arsenal.
Forbs alilazimika kusubiri hadi mazoezi ya kikosi cha kwanza yakamilike kabla ya kupata nafasi ya kufanya mazoezi, huku matumizi ya gym na eneo la chakula yakiwekewa masharti.
Baada ya kipindi hicho kigumu, alihamia Club Brugge ya Ubelgiji, ambako ameanza upya safari yake ya soka.
Novemba 2025 alijitambulisha kwa kishindo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao katika sare dhidi ya Barcelona.
Baada ya mchezo huo, alieleza furaha yake kwa kusema ilikuwa ndoto iliyotimia.
Msimu uliopita alifunga mabao 10 katika mashindano yote, huku msimu huu akiwa tayari amefikisha mabao matano.
Kwa sasa ana mechi tatu akiwa na timu ya taifa ya Ureno, baada ya kufanya debut yake mwaka uliopita, na ameanza kupata imani ya kocha mpya Jorge Jesus.
Alipoulizwa kama atakuwa mvaaji wa kudumu wa jezi namba saba, Forbs amesema:
"Ninajaribu kufanya vizuri kadiri ninavyoweza. Tunajua hii ni namba kubwa na yenye baraka. Natumaini nitaendelea kuivaa na kufunga mabao mengi."
Hata hivyo, bado kuna ushindani kutoka kwa Rafael Leao, ambaye tayari ana uzoefu mkubwa wa soka la kimataifa na amewahi kutwaa ubingwa wa Serie A akiwa AC Milan.
Kwa sasa macho ya mashabiki wa Ureno yataendelea kumwangalia Forbs kuona kama anaweza kuendeleza kiwango hicho na siku moja kubeba jukumu la kuendeleza urithi wa Ronaldo, aliyefunga mabao 146 kwa timu ya taifa.