Why always me? Safari ya Balotelli yenye vituko, migogoro
Muktasari:
- Akiwa na miaka 36, mshambuliaji huyo raia wa Italia bado hajakata tamaa ya kucheza soka, kwa sasa akiitumikia Al-Ittifaq inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Falme za Kiarabu (UAE), ambako anacheza pamoja na kaka yake wa damu, Enock Barwuah.
LONDON, England: MARIO Balotelli ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kuwa na kipaji kikubwa katika soka la dunia, lakini safari yake imejaa visa na matukio ya utata yaliyofanya maisha yake nje ya uwanja yazungumzwe zaidi kuliko mafanikio yake ya kucheza mpira.
Akiwa na miaka 36, mshambuliaji huyo raia wa Italia bado hajakata tamaa ya kucheza soka, kwa sasa akiitumikia Al-Ittifaq inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Falme za Kiarabu (UAE), ambako anacheza pamoja na kaka yake wa damu, Enock Barwuah.
Katika kipindi chote cha maisha yake ya soka, Balotelli amezichezea klabu 13 katika nchi sita tofauti, huku akihusika pia katika bao ambalo linatajwa kuwa miongoni mwa mabao maarufu zaidi katika historia ya Ligi Kuu England.
Miaka 15 imepita tangu alipofanya sherehe maarufu ya kuonyesha jezi yenye ujumbe wa “Why Always Me?” baada ya kufunga bao katika mchezo wa watani wa jadi wa Manchester, Manchester City dhidi ya Manchester United.
Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya nyumba yake kushika moto kufuatia kuwashwa fataki akiwa ndani ya bafu. Huo ni mfano mmoja tu wa matukio yaliyomfanya mshambuliaji huyo kuwa gumzo nje ya uwanja.
MANCINI HADI MOURINHO, MIGOGORO YAANZA
Tofauti na wachezaji wengi wanaoanza safari zao katika akademi za klabu kubwa, Balotelli alianza kucheza soka katika timu ya Lumezzane iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Tatu nchini Italia, karibu na nyumbani kwa familia yake mjini Concesio.
Akiwa kijana, alifanya majaribio katika klabu ya Barcelona, lakini hakufanikiwa kupata nafasi ya kubaki hapo. Badala yake, mwaka 2006 alisajiliwa na Inter Milan.
Huko ndiko alipokutana na kocha Roberto Mancini, ambaye alikuja kuwa mmoja wa watu muhimu zaidi katika maisha yake ya soka.
Uhusiano wa wawili hao ulifanananishwa na ule wa baba na mwana, huku Mancini akionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kukiongoza kipaji cha Balotelli na kukifanya kiwe na manufaa kwa timu.
Akiwa na miaka 17 pekee, Balotelli alisaidia Inter kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Italia msimu wa 2007/08 na kufika fainali ya Kombe la Italia. Miongoni mwa matukio yaliyokumbukwa ni alipofunga mabao mawili dhidi ya Juventus na kuiwezesha Inter kufuzu hatua ya nusu fainali.
Hata hivyo, maisha yake yalibadilika baada ya Jose Mourinho kuchukua nafasi ya Mancini, wiki chache baada ya msimu huo kumalizika.
Uhusiano wake na Mourinho haukuwa mzuri, kukiwa na kutokubaliana, hatua za kinidhamu na malalamiko kuhusu mwenendo wake.
Mourinho aliwahi kumwelezea Balotelli kuwa mchezaji asiyeweza kudhibitiwa, huku akitaja moja ya kiwango chake uwanjani kuwa kilikaribia kupata alama sifuri.
Pamoja na changamoto hizo, Balotelli alifanikiwa kutwaa mataji matatu ya Serie A na Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Inter, lakini tabia zake zilianza kufunika mafanikio aliyokuwa akiyapata uwanjani.
ENGLAND YAMFANYA GUMZO
Hatua iliyofuata katika maisha ya Balotelli ilikuwa kuungana tena na kocha wake wa zamani, Mancini, aliyekuwa amejiunga na Manchester City.
Agosti 2010, akiwa na miaka 20, Balotelli alisajiliwa na City, huku Mancini akiwa na matumaini ya kukitumia kipaji chake licha ya tabia zake zisizotabirika.
Kocha huyo alijaribu kumdhibiti kwa kutumia nidhamu, lakini mara kadhaa alionekana kuwa mvumilivu zaidi kwake kuliko ilivyokuwa kwa wachezaji wengine.
Kufikia mwanzoni mwa mwaka 2011, Balotelli alikuwa amejijengea jina England kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa, lakini aliyekuwa akijikuta katika matatizo mara kwa mara.
Alikuwa tayari amepata kadi nyekundu mara mbili akiwa na City na kuhusika katika ajali ya gari aina ya Audi R8, kabla ya tukio jingine la utovu wa nidhamu alipomrushia mshambuliaji chipukizi wa klabu hiyo mshale.
Tukio hilo lilionyesha kiwango cha utoto katika baadhi ya matendo yake.
Pamoja na hayo, alisaidia Manchester City kutwaa Kombe la FA mwaka 2011, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kushinda taji kubwa baada ya miaka 35.
Hata hivyo, hakukosa kuibua utata. Katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu dhidi ya LA Galaxy, alijaribu kufunga kwa kutumia kisigino akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, jambo lililomfanya Mancini amtoe uwanjani haraka.
Baadaye kocha huyo alihoji umakini wake akisema kama alikuwa makini angeweza kucheza dakika zote 90, lakini kama sivyo, angeweza kukaa naye benchi.
Wakati mwingine, vituko vyake vilimpa umaarufu mzuri, kama ilivyokuwa alipofunga bao kwa kutumia bega dhidi ya Norwich City na kusherehekea kwa utulivu mkubwa.
Lakini Oktoba 2011, alijikuta tena katika habari baada ya nyumba yake iliyopo Cheshire kushika moto kutokana na fataki kuwashwa ndani ya bafu. Balotelli alisema rafiki yake ndiye aliyesababisha tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wakati huo, wazima moto wanne walifika eneo hilo na kutumia vifaa vya kuzimia moto kudhibiti hali hiyo.
Siku chache baadaye, Balotelli alirejea katika vichwa vya habari kwa sababu nzuri baada ya kufunga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 6-1 wa Manchester City dhidi ya Manchester United.
Baada ya kufunga, alionyesha ujumbe kwenye jezi yake uliosomeka “Why Always Me?” (Kwa nini kila mara ni mimi?), ambao baadaye ukawa moja ya sherehe maarufu katika historia ya Ligi Kuu England.
Kulikuwa na simulizi nyingine nyingi kuhusu maisha yake, ikiwemo madai kuwa aliwahi kumpa ombaomba pauni 1,000, kwenda shuleni kwa mtoto aliyekuwa akinyanyaswa ili kuzungumza na mkuu wa shule na kuzunguka Manchester akigawa zawadi akiwa amevalia mavazi ya Santa Claus.
Hata hivyo, ukweli wa baadhi ya simulizi hizo haukuthibitishwa, huku Balotelli mwenyewe akiwahi kukanusha baadhi yake.
Umaarufu wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba mashabiki wa City walitengeneza wimbo uliotaja utani kuhusu madai ya kuwa na mzio wa majani, hali iliyowahi kumzuia kucheza mechi ya Europa Ligi mwaka 2011, pamoja na kuendesha gari katika eneo la Moss Side akiwa na pochi iliyojaa fedha.
JE, VITUKO VILISTAHILI KULIKO KIPAJI?
Licha ya matukio yake nje ya uwanja, Balotelli aliendelea kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Manchester City.
Aprili 2012, alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Arsenal, tukio lililoonekana kuhatarisha matumaini ya City kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huo.
Hata hivyo, mwezi mmoja baadaye, alikuwa sehemu muhimu ya historia ya klabu hiyo alipotoa pasi iliyotumiwa na Sergio Aguero kufunga bao la ushindi katika dakika za mwisho dhidi ya Queens Park Rangers.
Bao hilo liliipa Manchester City ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu England katika zama za kisasa. Pasi hiyo pia ilikuwa ya pekee aliyotoa katika Ligi Kuu msimu huo.
Aliyekuwa beki wa City na rafiki yake, Micah Richards, alimwelezea Balotelli kama mtu mwenye vituko lakini aliyekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi.
Alisema alikuwa mtu mzuri, asiye na majivuno kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vikimwelezea, ingawa alikuwa na tabia zisizotabirika.
Pamoja na vipaji vyake na nyakati za kung’ara, Mancini alianza kuona kuwa hawezi kuendelea kuvumilia mwenendo wa mshambuliaji huyo.
Januari 2013, wawili hao waligombana katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo, tukio lililokuwa mwisho wa ushirikiano wao. Baadaye mwezi huo, Balotelli aliondoka City na kujiunga na AC Milan.
Mancini alisema Balotelli hakuwa mtu mbaya na alikuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa, lakini alisikitishwa kuona akiendelea kupoteza uwezo wake kutokana na tabia zake.
Alitumaini mshambuliaji huyo angetambua kuwa mwenendo wake ungeweza kuathiri mustakabali wake wa soka.
Hata hivyo, pamoja na migogoro yao, bado kulikuwa na heshima kati yao.
Aliyekuwa mchezaji mwingine wa Manchester City, Nedum Onuoha, alikumbuka namna Balotelli alivyokuwa akijiamini kiasi cha kujiona kuwa alikuwa na uwezo sawa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Alisema tukio hilo lilitokea katika uwanja wa zamani wa mazoezi wa City, Carrington, wakati wachezaji walipokuwa wakizungumza kuhusu ubora wa mastaa hao wawili.
“Mario aliwahi kuamini kweli kuwa alikuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani. Nakumbuka mtu alipokuwa akizungumzia Messi na Ronaldo, Mario alisema alikuwa na uwezo sawa na wao, na alikuwa akimaanisha kabisa,” alisema Onuoha.
Aliongeza kuwa ingawa mambo hayakuishia kama Balotelli alivyokuwa akitarajia, bado amefanikiwa kufanya mambo mengi katika soka ambayo wachezaji wengi wangetamani kuyafikia.
Kwa Balotelli, historia itamkumbuka kama mchezaji aliyekuwa na kipaji cha kiwango cha juu, lakini ambaye safari yake ya soka iliambatana na vituko, migogoro.