Burkina Faso yashinda kwa mabao ya jioniii
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyoonekana kutokuwa na purukushani nyingi kwenye kipindi cha kwanza na kufanya ubao wa matokeo usomeke 0-0, uliwapa burudani mashabiki kwenye kipindi cha pili baada ya kushuhudia mabao matatu yakitinga kwenye nyavu.
RABAT, MOROCCO: BURKINA Faso ilifunga mara mbili ndani ya dakika za majeruhi kupindua meza dhidi ya Equatorial Guinea na kushinda 2-1 katika mchezo wa Kundi E mashindano ya Afcon 2025 uliofanyika uwanjani Stade Mohamed V jioni ya Jumatano.
Mechi hiyo iliyoonekana kutokuwa na purukushani nyingi kwenye kipindi cha kwanza na kufanya ubao wa matokeo usomeke 0-0, uliwapa burudani mashabiki kwenye kipindi cha pili baada ya kushuhudia mabao matatu yakitinga kwenye nyavu.
Mwanzoni kwa kipindi cha pili, Equatorial Guinea ilijikuta ikicheza pungufu kufuatia beki wa kushoto Basilio Ndong kutolewa kwa kadi nyekundu na kuacha mzigo mkubwa kwa wenzake uwanjani. Hata hivyo, Equatorial Guinea ilionekana kutokuwa na shida ya kucheza pungufu baada ya kutangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa mtokea benchini Marvin Anieboh, ambaye alihitaji dakika tatu tu ndani ya uwanja kutikisa nyavu na kuitanguliza timu yake.
Bao hilo liliwashtua Burkina Faso, ambao walishuhudia bao la Lassina Franck Traore, aliyetokea benchini likikataliwa na VAR.
Kocha wa Burkina Faso, Brama Traore alifanya mabadiliko ya mastaa kadhaa, ambapo alimwingiza pia Stephane Aziz Ki kuchukua nafasi ya Gustavo Sangare kwenye dakika ya 70, mabadiliko ambayo yaliongeza nguvu kwa timu hiyo na kufanikiwa kufunga mabao ya haraka kwenye dakika za majeruhi, kupitia kwa Georgi Minoungou, aliyetokea benchini na Edmond Tapsoba akafunga hesabu za kuipa Burkina Faso ushindi muhimu katika mechi yao ya kwanza ya Kundi E.
Katika mechi hiyo, Burkina Faso ilipiga mashuti 13, ambapo matano yalilenga golini, huku Equatorial Guinea ikipiga mashuti matano, manne to ndiyo yaliyolenga goli. Burkina Faso ilimiliki mpira kwa asilimia 66, dhidi ya 34 za Equatorial Guinea, ambaye kipa wao, Jesús Owono akifanya sevu tatu licha ya kuruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili kwenye dakika za lala salama.