Simba Queens inavyoipa heshima Simba Day
Muktasari:
- Hiyo ni Simba Queens, mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ambao wameendelea kuandika historia ndani na nje ya nchi.
WAKATI Simba ikijiandaa kuonyesha kikosi chake kipya kwenye Simba Day, kuna timu nyingine ambayo imekuwa sehemu muhimu ya tamasha hilo kwa takribani msimu wa saba sasa kutokana na mafanikio yake makubwa.
Hiyo ni Simba Queens, mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ambao wameendelea kuandika historia ndani na nje ya nchi.
Tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, macho yote yalikuwa kwa kikosi cha wanaume, sasa Simba Queens imekuwa kivutio kikubwa kutokana na rekodi ilizoziweka.
MATAJI YANAONGEA
Tangu Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ilipoanzishwa mwaka 2017, Simba imebeba mataji matano ya ligi, rekodi inayoiweka miongoni mwa klabu zilizofanikiwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Mataji hayo waliyabeba misimu ya 2019/20, 2020/21, 2021/22, 2023/24 na 2025/26, yakionesha uimara wa kikosi hicho kwa kipindi kirefu licha ya ushindani kuongezeka kila msimu.
Mbali na mafanikio ya ligi, Simba pia ilitwaa Ngao ya Jamii ya wanawake msimu wa 2024/25, ikithibitisha ubora wake katika mechi za ufunguzi wa msimu. Mafanikio hayo yameifanya Simba kuwa moja ya timu chache za wanawake nchini zilizojenga utamaduni wa kushindania mataji kila msimu.
REKODI YA AFRIKA
Mbali na kutawala ndani ya Tanzania, Simba ina rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake.
Msimu wa 2022/23 Simba iliwakilisha ukanda wa CECAFA kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na kuweka rekodi ya kucheza nusu fainali ambayo haijavunjwa hadi sasa na timu za ukanda huo.
Miongoni mwa timu zilizowahi kushiriki lakini zikashindwa kuvuka hatua hiyo ni Vihiga Queens ya Kenya, JKT Queens ya Tanzania pamoja na Commercial Bank of Ethiopia (CBE) ya Ethiopia na zote ziliishia makundi.
UBABE WA DABI
Mbali na mataji na rekodi za kimataifa, Simba ina historia nyingine kupitia mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga Princess yaani Kariakoo Dabi.
Tangu timu hizo zilipoanza kukutana Ligi Kuu ya Wanawake, Simba imekuwa ikipewa nafasi kubwa kutokana na matokeo yake mazuri na katika mechi 14 kati ya mwaka 2019 na 2026, imeshinda mara tisa, Yanga ikishinda mara mbili huku mechi tatu zikiisha kwa sare.
Ubora huo umeifanya Simba Queens kuwa timu iliyotawala dabi ya wanawake kwa kipindi kirefu. Mara nyingi mechi hizo zimekuwa zikiamua mbio za ubingwa, jambo lililoongeza ushindani na mvuto wa soka la wanawake nchini.
USHINDI MKUBWA DABI
Katika historia ya dabi hiyo, Simba imeandika ushindi ambao bado unatajwa na mashabiki wao.
Miongoni mwa matokeo makubwa zaidi ni ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Yanga Januari 13-2019, ukiwa ndio ushindi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika dabi hiyo.
Pia Simba iliwahi kushinda mabao 5-1 mara mbili April 22, 2019, ushindi wa 4-1 pamoja na ushindi mwingine wa 3-1 ulioonyesha namna timu hiyo ilivyokuwa na ubora mkubwa dhidi ya wapinzani wake.
Ingawa Yanga imewahi kupata ushindi katika baadhi ya misimu, mara nyingi Simba ndiyo imekuwa ikipewa nafasi kutokana na ubora wake, uzoefu wa kikosi na uwezo wa kutumia nafasi za kufunga.
Rekodi hizo zimeifanya dabi ya wanawake kuwa moja ya mechi zinazosubiriwa zaidi katika soka la wanawake Tanzania, huku mashabiki wa pande zote mbili wakitarajia kuona ushindani mpya kila zinapokutana.
MGOSI ANA REKODI
Nyuma ya mafanikio ya Simba kuna jina la kocha Mussa Hassan ‘Mgosi’, ambaye amekuwa sehemu muhimu ya benchi la ufundi kwa miaka kadhaa.
Mgosi alianza kuandika historia yake na Simba Queens msimu wa 2019/20 alipokuwa sehemu ya benchi lililoiongoza timu kutwaa ubingwa wa ligi.
Msimu uliofuata wa 2020/21 alichangia tena mafanikio hayo kabla ya timu kutwaa ubingwa wa 2021/22 chini ya makocha wengine.
Baada ya kurejea kwenye benchi la ufundi, aliendelea kushiriki mafanikio ya Simba Queens katika misimu ya 2023/24 na 2025/26, rekodi iliyomfanya kufikisha mataji manne ya ligi akiwa sehemu ya benchi la timu hiyo.
Rekodi hiyo inamuweka miongoni mwa makocha waliofanikiwa zaidi katika historia ya soka la wanawake Tanzania.
Katika kipindi hicho amefanya kazi na makocha mbalimbali akiwemo Hababuu Ally, Sebastian Nkoma, Charles Lukula na Juma Mgunda, lakini mchango wake umeendelea kuonekana kupitia uimara wa kikosi na matokeo yaliyopatikana.
Ubingwa wa msimu wa 2025/26 umeongeza uzito wa rekodi yake, ukiifanya Simba Day ya mwaka huu kuwa fursa nyingine kwa mashabiki wa Simba kusherehekea si mafanikio ya wachezaji pekee, bali pia benchi la ufundi lililokuwa sehemu ya safari ya kuifanya Simba Queens kuwa moja ya timu bora zaidi kuwahi kutokea katika soka la wanawake Tanzania.