Kagere, Niyonzima wagawana upande
Muktasari:
- Leo Ijumaa, macho yote yataelekezwa Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali wakati Rayon Sports ya Rwanda itakapovaana na Gor Mahia ya Kenya katika pambano la kutafuta bingwa mpya wa Afrika Mashariki na Kati baada ya Al Hilal ya Sudan kucheza mechi ya mashindi wa tatu dhidi ya Jamus.
KUNA msemo maarufu hapa Rwanda unaosema ‘Umutima ntushobora gukunda impande ebyiri icyarimwe’ ukiwa na maana moyo hauwezi kupenda pande mbili kwa wakati mmoja. Ndivyo ilivyo kwa mastaa wawili waliowahi kutamba na timu ya taifa ya nchi hiyo, Meddie Kagere na Haruna Niyonzima saa chache kabla ya fainali ya Kombe la CECAFA Kagame 2026.
Leo Ijumaa, macho yote yataelekezwa Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali wakati Rayon Sports ya Rwanda itakapovaana na Gor Mahia ya Kenya katika pambano la kutafuta bingwa mpya wa Afrika Mashariki na Kati baada ya Al Hilal ya Sudan kucheza mechi ya mashindi wa tatu dhidi ya Jamus.
Nje ya uwanja, kuna bato lingine kati ya mastaa wawili hao waliowahi kuandika historia kubwa katika soka la Rwanda ambao sasa kila mmoja ana sababu ya kuitakia ushindi timu tofauti.
Kagere anaegemea upande wa Gor Mahia, klabu iliyomjengea hadhi kubwa nchini Kenya. Niyonzima anasimama upande wa Rayon Sports, timu iliyompa nafasi ya kwanza kujitangaza kabla ya kuwa mmoja wa viungo bora kabisa kuwahi kutokea Rwanda.
KAGERE, MTU WA GOR MAHIA
Kwa mashabiki wa Gor Mahia, jina la Kagere halihitaji utambulisho mrefu. Alifika Nairobi mwaka 2015 na ndani ya muda mfupi akawa mmoja wa washambuliaji waliotikisa Ligi Kuu ya Kenya.
Katika vipindi vyake viwili akiwa Gor Mahia kati ya 2015 na 2018, Kagere aliifungia klabu hiyo mabao 50 katika mashindano yote, jambo linalomweka miongoni mwa wafungaji 10 bora wa muda wote wa klabu hiyo.
Mbali na mabao, aliiwezesha Gor Mahia kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Kenya mfululizo (2015, 2017 na 2018), huku mara mbili akimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa ligi.
Mwaka 2017 pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka nchini Kenya (SJAK MVP) baada ya msimu bora akiwa na jezi ya K’Ogalo.
Hadi leo, mashabiki wa Gor Mahia bado wanamtaja Kagere kama mmoja wa washambuliaji bora wa kizazi cha sasa waliowahi kuivaa jezi ya kijani.
Ndiyo maana fainali ya leo inamgusa moja kwa moja mshambuliaji huyo. Ni timu ambayo ilimpa mafanikio makubwa kabla ya kuhamia Simba SC ambako pia aliandika historia.
Akizungumzia fainali hiyo, Kagere amesema anaamini mashabiki watashuhudia mchezo wenye ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili, lakini amesisitiza moyo wake uko upande wa Gor Mahia.
“Gor Mahia ni sehemu muhimu ya maisha yangu ya soka. Nilipata mafanikio makubwa nikiwa pale, nilishinda mataji, nikawa mfungaji bora na nilipata upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki. Hivyo ni kawaida kuwa naitakia kila la kheri,” alisema Kagere.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Amavubi, alisema anafahamu ugumu wa kucheza dhidi ya Rayon Sports, hasa inapokuwa mbele ya mashabiki wake kwenye Uwanja wa Amahoro.
“Rayon ni timu nzuri sana na kucheza nyumbani kutawapa nguvu kubwa. Mashabiki wao wanajua kuisukuma timu, lakini Gor Mahia pia ni timu yenye uzoefu wa mechi kubwa na wachezaji wake wanajua namna ya kucheza kwenye presha,” alisema.
Kagere anaamini mchezo huo utaamuliwa na nidhamu, utulivu na uwezo wa kutumia nafasi chache zitakazojitokeza.
Licha ya kuutaka ushindi wa Gor Mahia, Kagere amesema jambo muhimu zaidi kwake ni kuona fainali hiyo inakuwa ya kiwango cha juu na kuendelea kuonyesha ukuaji wa soka la Afrika Mashariki.
“Ninaamini mashabiki watapata burudani nzuri. Haya ni mashindano yenye historia kubwa katika ukanda wetu na ni vizuri kuona timu mbili kubwa zikimalizia kwa mchezo mzuri,” alisema Kagere.
NIYONZIMA MTOTO WA RAYON
Upande wa pili yupo Niyonzima ambaye kabla ya kuwa nyota wa APR, Yanga, Simba na nahodha wa muda mrefu wa Amavubi, safari yake ilianzia Rayon Sports.
Aliichezea Rayon kati ya mwaka 2006 na 2007 akiwa bado kijana mwenye ndoto za kutengeneza jina.
Ingawa baadaye alihamia APR na kuwa mmoja wa viungo bora zaidi kuwahi kutokea Rwanda, Niyonzima hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Rayon Sports, klabu iliyomfungulia milango ya soka la ushindani.
Akiwa na Amavubi, aliweka rekodi ya kuichezea Rwanda mechi 112, nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote katika historia ya timu hiyo.
Kutoka hapo alijenga jina kubwa, akatwaa mataji mengi akiwa APR kabla ya kuhamia Yanga na baadaye Simba nchini Tanzania.
Akizungumzia fainali hiyo, Niyonzima alisema anatarajia ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili, lakini amesisitiza anatamani kuona Rayon Sports ikitumia vizuri faida ya kucheza nyumbani na kubakiza kombe nchini Rwanda.
“Ni mchezo mkubwa sana kwa soka la ukanda wetu. Gor Mahia ni timu yenye historia na uzoefu mkubwa, lakini naamini Rayon Sports ina kila sababu ya kujiamini kwa sababu imefika fainali kwa kiwango kizuri na itakuwa inacheza mbele ya mashabiki wake,” alisema Niyonzima.
Kiungo huyo wa zamani wa Amavubi, amesema nguvu ya mashabiki inaweza kuwa silaha muhimu kwa Rayon Sports, lakini akasisitiza wachezaji wanapaswa kuwa watulivu na kuepuka kubebwa na presha ya fainali.
“Mashabiki watakuwa wengi na watatoa sapoti kubwa, lakini katika mechi kama hizi kinachohitajika ni nidhamu, umakini na kutumia nafasi chache zinazopatikana. Fainali huamuliwa na makosa madogo,” alisema.
Niyonzima amesema kuona timu ya Rwanda ikicheza fainali ya CECAFA Kagame mbele ya mashabiki wake ni jambo linalompa fahari kubwa, akiamini ubingwa huo utakuwa zawadi nzuri kwa mashabiki ambao wameiunga mkono Rayon Sports tangu mwanzo wa mashindano.
FAINALI YA KUMBUKUMBU
Kwa namna moja au nyingine, fainali ya leo inawarejesha Kagere na Niyonzima kwenye kumbukumbu zao.
Mmoja anakumbuka miaka ya makubwa aliyoyafanya Nairobi mwingine anakumbuka siku alipoanza kuamini anaweza kuwa mchezaji mkubwa akiwa Kigali.
Ni hadithi ya mastaa wawili waliotoka nchi moja, wakaitumikia Amavubi kwa mafanikio, lakini sasa mioyo yao imegawanyika.
Mmoja anatamani Gor Mahia iongeze historia yake kwa kutwaa ubingwa mwingine wa michuano hiyo, huku mwingine akitamani Rayon Sports iibebe Rwanda mabegani kwa kubakiza kombe nyumbani.
Leo usiku majira ya saa 1:00 kwa Afrika ya Kati huku Afrika Mashariki na Tanzania kwa ujumla ikiwa saa 2:00 usiku, ndani ya Uwanja wa Amahoro, mmoja atakuwa na sababu ya kutabasamu zaidi.
NJIA YA GOR, RAYON FAINALI
Gor Mahia ambayo ilikuwa kundi A, ilianza mashindano hayo kwa kishindo kufuatia kuichapa APR ya Rwanda mabao 5-0 kisha ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Vipers.
Baada ya kupoteza dhidi ya mabingwa hao wa Uganda, Gor Mahia ilijibu mapigo kwa kuichapa Garde Republicaine ya Djibouti bao 1-0 na kutinga nusu fainali kabla ya kukutana na Al Hilal.
Gor Mahia ilikuwa na pointi sita sawa na Vipers lakini ilibebwa na wastani mzuri wa mabao hivyo ikasonga mbele.
Rayon Sports iliyokuwa kundi C yenyewe ilitinga kwa kishindo hatua na nusu fainali kufuatia kushinda mechi zake zote za hatua ya makundi.
Walianza kwa kuichapa KVZ ya Zanzibar kwa mabao 2-0, Tusker na Al Hilal bao 1-0 katika kila mchezo hivyo kumaliza kinara wa kundi hilo ikiwa na pointi tisa kabla ya kuichapa Jamus na kutinga fainali.
Mbali na historia na heshima ya ubingwa, timu hizo mbili ambazo zimetinga fainali ya michuano hiyo pia zinawania zawadi ya fedha.
Mshindi wa CECAFA Kagame 2026 ataondoka na Dola 30,000 za Marekani, huku mshindi wa pili akipata Dola 20,000 na mshindi wa tatu ni Dola 10, 000.