Mo awataja Okwi, Phiri Simba
Muktasari:
- Mo ambaye ameifanyia Simba mambo makubwa na kuifanya kuwa klabu maarufu Afrika huku timu hiyo ikitajwa kuwa moja kati ya zile zenye mafanikio makubwa zaidi Tanzania, amesema anaheshimu mchango wa kila mmoja kwenye kikosi hicho.
MWEKEZAJI wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema Simba wamepita wachezaji wengi bora, lakini kwake kuna baadhi ambao anaweza kuwakumbuka kwenye maisha yake yote.
Mo ambaye ameifanyia Simba mambo makubwa na kuifanya kuwa klabu maarufu Afrika huku timu hiyo ikitajwa kuwa moja kati ya zile zenye mafanikio makubwa zaidi Tanzania, amesema anaheshimu mchango wa kila mmoja kwenye kikosi hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalumu wakati Simba ikiadhimisha miaka 90 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936, mwekezaji huyo amesema anaamini kwa kipindi kijacho timu hiyo inaweza kufanya mambo makubwa zaidi Afrika kuliko ilivyofanya kwenye miaka 90 iliyopita.
Mo ambaye kabla hajawa mwekezaji alikuwa shabiki kindakindaki wa Simba, amesema kwenye klabu hiyo wamepita wachezaji wengi na makocha lakini kwake kuna baadhi wameifanya Simba mambo makubwa sana na kwake hao ndiyo bora zaidi kwake.
“Simba wamepita wachezaji wengi wakubwa lakini pia makocha bora, siyo kwamba wengine hawajafanya vizuri hapana, kila mmoja ameonyesha ubora wake kwa kipindi chake na kupeperusha bendera ya klabu hii kwa ubora wa hali ya juu.
“Hata sasa bado Simba ina kikosi bora sana kuanzia makocha na hata wachezaji waliopo lakini kwa kipindi changu naamini Patrick Phiri ndiye kocha bora zaidi kuwahi kuifudisha Simba,” amesema MO huku akitabasamu.
Phiri, raia wa Zambia ni kati ya makocha ambao waliwahi kuifundisha Simba na kupata mafanikio makubwa ambapo aliweka rekodi ya kuiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2009-2010 bila kupoteza mchezo akiwa ni kocha wa kwanza kufanya hivyo kwenye kikosi hicho.
Kocha huyo ambaye alikuwa kiboko ya Yanga, alifanikiwa kuifundisha Simba kwa vipindi vitatu tofauti mwisho ukiwa msimu wa 2014–2015 na mara kwa mara amekuwa akitajwa kuwa mmoja kati ya makocha bora zaidi kuwahi kufundisha soka hapa nchini.
Kocha huyo ambaye amefanikiwa kuzifudisha timu 13 tofauti kwenye maisha yake, pia ameshaifundisha timu ya Taifa ya Zambia kwa vipindi viwili tofauti na kupata mafanikio makubwa sana.
MO ambaye aliingia Simba kama mwekezaji mwaka 2017, timu hiyo imekuwa na mafanikio makubwa zaidi kwa kipindi chake ikifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano pamoja na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, amesema mbali na kocha huyo pia kuna wachezaji ambao kwake ni bora zaidi kwa kipindi chote.
“Simba wamepita wachezaji wengi sana mahiri, naheshimu mchango wa kila mmoja kwa kuwa wote kwangu wamekuwa na mchango, lakini kuna wale ambao ni bora zaidi kwangu baadhi yao ni Edward Chumila, Zamoyoni Mogela, Mohamed Kajole, Twaha Hamidu, Emmanuel Okwi, Yusuph Macho ‘Musso’, pamoja na Meddie Kagere.
“Hawa ni bora na walifanya kazi nzuri, ingawa kila mmoja anatakiwa kufahamu kuwa hawa ni mfano tu lakini kuna wachezaji wengi sana bora kwenye timu hii waliowahi kupita na wengine wapo kikosini hadi sasa,” amesema Mo ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kwenye klabu hiyo kwa vipindi tofauti.
MO ambaye ni shabiki wa Arsenal ya England, ameisaidia Simba kuwa na mafanikio makubwa kipindi chake chote cha uwekezaji huku timu hiyo ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo kwenye kipindi chake.