Bukayo Saka nje wiki nane
Muktasari:
- Nyota huyo wa England alilazimika kusaidiwa kutoka uwanjani na madaktari wa timu hiyo, huku Arsenal sasa ikisubiri matokeo zaidi ya vipimo kubaini ukubwa halisi wa tatizo hilo.
LONDON, ENGLAND: NYOTA wa Arsenal, Bukayo Saka, anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki sita hadi nane baada ya kupata jeraha la paja, hali inayoongeza maumivu kwa kikosi hicho katika kipindi muhimu cha msimu.
Saka mwenye umri wa miaka 25, alipata jeraha hilo dakika ya 10 tu ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Jumatano usiku na kutolewa uwanjani.
Nyota huyo wa England alilazimika kusaidiwa kutoka uwanjani na madaktari wa timu hiyo, huku Arsenal sasa ikisubiri matokeo zaidi ya vipimo kubaini ukubwa halisi wa tatizo hilo.
Jeraha hilo linaongeza orodha ya majeraha ambayo Saka amekuwa akipata mara kwa mara, likiwa la 11 tangu Septemba 2024. Awali, mchezaji huyo pia aliwahi kusumbuliwa na tatizo la muda mrefu la kisigino, ambalo aliendelea kucheza nalo wakati wa Kombe la Dunia.
Akizungumzia hali ya Saka na kama mchezaji huyo amepoteza uimara wake wa kimwili, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alisema mahitaji makubwa ya soka la kisasa yanaweza kuwa na mchango katika changamoto zinazowakabili wachezaji.
Arteta alisema ratiba yenye michezo mingi, kasi kubwa ya mechi na muda mfupi wa kupumzika vinaongeza mzigo kwa wachezaji.
Alifafanua kuwa Arsenal inakabiliwa na ratiba inayowalazimu kucheza Jumapili, kusafiri kwa ajili ya mchezo wa Jumatano na kurejea uwanjani tena Jumamosi, huku muda wa mapumziko kati ya baadhi ya mechi ukiwa chini ya saa 67.
Kocha huyo alizitaka mamlaka zinazosimamia soka kuzingatia mzigo unaowekwa kwa wachezaji na kusaidia kutafuta mazingira yatakayowawezesha kukabiliana na mahitaji hayo.
Amesisitiza kuwa suala hilo haliihusu Arsenal pekee, bali ni changamoto inayoweza kuzikabili timu nyingine kutokana na wingi wa mashindano na ratiba zinazobana.
Arteta alifichua kuwa Saka alihitaji kufanyiwa kipimo kingine cha MRI kutokana na kujaa kwa majimaji mengi katika eneo lililoumia, jambo lililofanya iwe vigumu kutambua ukubwa wa jeraha hilo kwa uharaka.
Alisema majibu zaidi yalitarajiwa kupatikana baada ya vipimo vya ziada na maoni ya wataalamu wa afya.
Kwa mujibu wa Arteta, kitendo cha mchezaji kushindwa kuendelea na mchezo, kupata maumivu anapotembea na kushindwa kusogeza sehemu ya mwili kwa uhuru ni viashiria vinavyohitaji kuangaliwa kwa umakini.
Licha ya majeraha ya mara kwa mara, Arteta alisema hana hisia kwamba Saka atafikia hatua ya kuchoka na kupoteza uwezo wake akiwa na umri wa miaka 30.
Badala yake, amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira sahihi yatakayomsaidia mchezaji huyo kutumia kikamilifu vipaji vyake na kulinda afya yake ya muda mrefu.
Kocha huyo alisema Arsenal itahitaji kutathmini kwa makini namna ya kusimamia mzigo wa michezo wa Saka atakaporejea uwanjani, bila kujali muda atakaotumia kupona.
Kwa Arsenal, kukosekana kwa Saka kwa muda huo kunaweza kuwa pigo kubwa kutokana na mchango wake katika safu ya ushambuliaji, huku macho yakielekezwa katika maendeleo ya matibabu yake na namna timu itakavyoziba pengo lake katika michezo ijayo.