Brentford yamshtaki aliyepiga mpira uwanjani
Muktasari:
- Tukio hilo limeibua mjadala baada ya video yake kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, huku uongozi wa Brentford ukilielezea kitendo hicho kuwa cha hatari na kinachoweza kusababisha madhara makubwa.
LONDON, ENGLAND: KLABU ya Brentford imefungua mashtaka kuchunguza shabiki aliyerusha mpira wa raga kutoka juu ya jengo la makazi hadi ndani ya Uwanja wa Gtech Community, tukio lililotokea wakati timu hiyo ikichapwa mabao 2-1 na Liverpool Jumamosi.
Tukio hilo limeibua mjadala baada ya video yake kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, huku uongozi wa Brentford ukilielezea kitendo hicho kuwa cha hatari na kinachoweza kusababisha madhara makubwa.
Mpira huo ulitua karibu na eneo la kuchezea kabla ya kuchukuliwa na mmoja wa wafanyakazi wa uwanja huo. Hakukuwa na taarifa za mtu kujeruhiwa kutokana na tukio hilo.
Uwanja wa Brentford umezungukwa na majengo marefu ya makazi, na uchunguzi wa awali unaashiria kuwa mpira huo huenda ulirushwa kutoka kwenye jengo la kifahari la Memento Kew Bridge.
Jengo hilo lina jumla ya vyumba 487 vya makazi, huku baadhi ya wakazi wakipata mwonekano wa moja kwa moja wa uwanja huo.
Katika taarifa yake, Brentford imesema suala hilo limefikishwa kwa polisi na klabu itashirikiana na mamlaka husika kuwabaini waliohusika ili hatua stahiki zichukuliwe, ikiwamo uwezekano wa kufunguliwa mashtaka ya jinai.
Klabu hiyo imesisitiza kuwa usalama wa mashabiki, wachezaji, viongozi na wafanyakazi wakati wa mechi ni kipaumbele chake kikuu.
Cha kufurahisha, uwanja huo uliwahi kutumiwa na klabu ya raga ya London Irish kati ya mwaka 2020 na 2023 kabla ya kusimamishwa kushiriki Ligi ya Premiership kutokana na matatizo ya kifedha.
Wakati tukio hilo likizua gumzo nje ya uwanja, Brentford ilipoteza mchezo dhidi ya Liverpool baada ya wageni hao kufanya mabadiliko makubwa katika kipindi cha pili.
Brentford ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza kupitia kwa Keane Lewis-Potter, lakini kadi nyekundu aliyoonyeshwa Yehor Yarmolyuk mwishoni mwa kipindi cha kwanza kwa kumpiga kichwa Jeremy Jacquet ilibadilisha mwelekeo wa mchezo.
Liverpool ilitumia nafasi hiyo kurejea mchezoni, huku winga Victor Munoz akisawazisha kabla ya Alexander Isak kufunga bao la ushindi, ambalo lilikuwa la tano kwake msimu huu, baada ya kurejea kutoka kwenye majeruhi.
Majengo yanayozunguka uwanja huo yamewahi pia kuibua gumzo. Mwaka 2024, mwimbaji Noemi Oberhauser alifichua kuwa baadhi ya wanaume walikuwa wakimwalika kwenye miadi kwa lengo la kupata nafasi ya kutazama mechi za soka kupitia dirisha la makazi yake.