Bondia Dubois amtwanga Wardley
Muktasari:
- Dubois alilipuka kwa mashambulizi makali tangu mwanzo wa pambano hilo lililofanyika katika ukumbi wa O2, akimstua Wardley ndani ya sekunde 17 kwa konde la kulia lililokuwa na nguvu kubwa, kabla ya kuendeleza kipigo kilichofanya pambano hilo lisifikie raundi ya tatu.
LONDON, ENGLAND; BONDIA Daniel Dubois ameonyesha ubabe wa aina yake baada ya kumchapa Fabio Wardley katika pambano la marudiano, akituma ujumbe mzito kwa mabondia wa uzito wa juu duniani kuhusu azma yake ya kutwaa mataji yote makubwa.
Dubois alilipuka kwa mashambulizi makali tangu mwanzo wa pambano hilo lililofanyika katika ukumbi wa O2, akimstua Wardley ndani ya sekunde 17 kwa konde la kulia lililokuwa na nguvu kubwa, kabla ya kuendeleza kipigo kilichofanya pambano hilo lisifikie raundi ya tatu.
Wardley, ambaye alikuwa akitafuta kurejesha taji la WBO alilopoteza dhidi ya Dubois miezi mitano iliyopita, alijikuta katika wakati mgumu kutokana na mashambulizi ya mpinzani wake yaliyokuja kwa kasi na nguvu kubwa.
Safari hii, kona ya Wardley haikusubiri mambo yaendelee kuwa mabaya zaidi, ikatupa taulo kuashiria kusitisha pambano hilo na kumwepusha bondia huyo na kipigo zaidi.
“Fabio ni kijana mzuri, amekuja kupambana nami kwa mara ya pili, lakini huu ni wakati wangu na zama zangu,” amesema Dubois.
“Nilikuwa na nia ya kufanya mambo makubwa tangu mwanzo wa pambano.”
Dubois alionyesha nguvu na ukakamavu uliowafanya mashabiki na wadau wa ndondi kumtazama upya, hasa baada ya hapo awali kuhojiwa kuhusu uwezo wake wa kustahimili presha katika mapambano makubwa.
Bondia Filip Hrgovic, mmoja wa mabingwa wa uzito wa juu waliokuwepo kushuhudia pambano hilo, alishuhudia mwenyewe makali ya Dubois. Hrgovic, ambaye hivi karibuni alikuwa amemshinda Moses Itauma, alionekana kushangazwa na kiwango cha mashambulizi ya Dubois.
Ushindi huo umeongeza hamasa kuhusu uwezekano wa Dubois kukutana na mabondia wengine wakubwa, akiwemo Agit Kabayel, huku macho pia yakielekezwa kwa mshindi wa pambano linalotarajiwa kufanyika Desemba kati ya Tyson Fury na Anthony Joshua.
Kwa Dubois, ushindi huo ni hatua muhimu katika harakati zake za kutwaa hadhi ya bingwa wa dunia asiye na mpinzani katika mataji makubwa ya uzito wa juu, akilenga kufuata nyayo za Oleksandr Usyk.
“Nimekuwa bingwa sasa, na ninataka mapambano makubwa zaidi. Katika hatua hii ya taaluma yangu, ninataka mapambano makubwa na fedha nyingi,” amesema Dubois.
Pambano hilo lilikuwa mwendelezo wa ushindani mkali kati ya mabondia hao wawili. Katika pambano lao la awali, Dubois aliinuka kutoka sakafuni mara mbili kabla ya kuibuka mshindi na kutwaa taji lake la pili la uzito wa juu duniani.
Wardley, ambaye alishindwa kumalizia pambano wakati Dubois akianguka, alilipa gharama kubwa kwa kushindwa kutumia nafasi hiyo, huku akitoka kwenye pambano hilo akiwa amejeruhiwa usoni baada ya kushambuliwa mfululizo.
Ushindi wa Dubois umeweka wazi kuwa kizazi kipya cha mabondia wa uzito wa juu kinaendelea kujipambanua, huku bondia huyo akituma ujumbe kuwa yuko tayari kupambana na majina makubwa zaidi katika ndondi za kulipwa.