Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msije: Mwakinyo, Kiduku kioo cha ngumi Tanzania

MSIJE Pict

Muktasari:

  • Kocha huyo ambaye alianzia kucheza kwenye Karate alipopata ujuzi chini ya kocha Juma Mwigaya maarufu Sydool tangu mwaka 2006 kabla ya kuingia kwenye ngumi mwaka 2018 alipofundishwa na kaka yake Juma Mseje.

MIONGONI mwa makocha vijana wanaomfanya bondia, Hamad Furahisha anakuwa fiti na mwenye stamina akiwa ulingoni ni kocha wake Abdallah Mseje kutoka Friends Gym iliyopo Tandika.

Kocha huyo ambaye alianzia kucheza kwenye Karate alipopata ujuzi chini ya kocha Juma Mwigaya maarufu Sydool tangu mwaka 2006 kabla ya kuingia kwenye ngumi mwaka 2018 alipofundishwa na kaka yake Juma Mseje.

“Nilicheza kwanza karate tunauita Mufu baadae nikaachana na mchezo huo nikaenda kujifunza mambo ya ngumi lakini kwenye ukocha ndipo hadi sasa nipo na aliyenishawishi ni kaka yangu Juma,” anasema Mseje

Chini ya Gym hiyo anafundisha mabondia tofauti lakini maarufu zaidi ni Furahisha ambaye ni miongoni mwa mabondia wenye uwezo mkubwa wa kupigana.

Makala haya yanakuletea undani wa safari ya kocha huyo, mtazamo wake kuhusu mabondia wakubwa kama Hassan Mwakinyo na Twaha Kiduku, changamoto za lishe zinazowamaliza mabondia, na rekodi za Hamadi Furahisha chini ya mikono yake.


MSI 01

ANAFUNDISHA WOTE

Kocha huyo anasema mbali na kumsimamia Furahisha kwenye gym hiyo anawafundisha wachezaji mbalimbali wa Ligi Kuu hususani kwenye eneo la ufiti akimtaja miongoni mwa nyota wa zamani wa Azam, Abdulrahim Humoud na nyota wa Yanga Princess, Lucy Mrema.

“Mimi huwapenda sana wanamichezo wa aina zote; nimekuwa nikiwafundisha wachezaji wa mpira kutoka klabu kubwa kama Yanga, Simba, na hata wachezaji wa timu ya taifa (Taifa Stars) waliowahi kufika hapa kwa ajili ya kujenga ufiti,” anasema Mseje

Anaeleza kuwa michezo mingi inafanana kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la nidhamu ya mazoezi, ingawa ngumi zinahitaji umakini mkubwa zaidi na uvumilivu wa hali ya juu. Anasema mafunzo ya viungo anayowapatia wachezaji yanayowasaidia kuongeza nguvu, kasi, na  stamina ya kudumu uwanjani.


ANACHOKIONA KWA FURAHISHA

Mseje anamtaja Furahisha kuwa mmoja wa mabondia wenye nidhamu ya hali ya juu na anaamini mafanikio yake yanatokana na kusikiliza kile anachoambiwa na makocha wake.

Tangu Hamadi Furahisha aanze kupigana ngumi za kulipwa mwaka 2017, amecheza jumla ya mapambano 17, ambapo kati ya hayo ameshinda mapambano 13, amepoteza mapambano mawili, na kutoka sare katika mapambano mawili.

“Huyu Hamadi ni bondia mzuri sana, kwanza napenda anachofanya. Nikimwambia fanya hivi, anafanya papo hapo kwa hatua aliyofikia tunaona mabondia wanachofanya kwa makocha waliowafundisha wengi wana dharau wakifanikiwa ndio maana baadhi wanapotea,” anasema


MSI 02

MSEJE VS PHIRI

Kocha huyo anasema miongoni mwa kumbukumbu nzuri ambayo hataisahau ilikuwa kwenye pambano kati ya Furahisha na Hannock Phiri ‘Kumbakumba’ kutoka Malawi mwaka 2025 katika pambano la kuwania Ubingwa wa Tanzanian Super Light wa Pugilistic Syndicate of Tanzania, anasema kabla hajapanda ulingoni alimwambia anapaswa kucheza ile staili yake ya kutembea wakati mpinzani wake anakuja na akakifanyia kazi.

“Lile pambano na Phiri lilikuwa bora na sitalisahau ukiachana na ushindi alikuwa na mchezo wa mzuri  kwa kuweza kumdhibiti katika raundi  kumi za pambano hilo na kuweza kumpiga kwa hesabu kali kiasi cha kumfanya Phiri akose kujitetea,” anasema kocha huyo.

Kocha huyu anaamini kuwa rekodi za Furahisha zinazidi kuimarika kila siku kutokana na utayari wake wa kujifunza na kutenda yale anayoelekezwa wakati wa mazoezi mazito ya asubuhi na jioni.


ZINAPOKWAMA NGUMI ZA BONGO

Akizungumzia changamoto zinazokwamisha maendeleo ya ngumi za Tanzania, Kocha Mseje anataja mfumo wa maandalizi na ukosefu wa mapambano ya mara kwa mara kuwa ni vikwazo vikubwa.

“Sasa unakuta bondia anakesha wiki nzima Gym kufanya mazoezi wakati anajiandaa na pambano hiyo haijakaa sawa, anapaswa kufanya mazoezi hayo kama ni siku mbili zingine ni kwa ajili ya ulingoni kufanyia marekebisho na kutengeneza pumzi,” anasema kocha huyo na kuongeza

“Lakini pia kama bondia mwaka mzima anacheza pambano moja tu unategemea atakuwa bora bondia anapoifanya mazoezi maana yake mwili unataka pambano.”


MSI 03

RATIBA YA FURAHISHA

Kocha huyo anasema ili bondia awe mzuri anapaswa kupumzika muda mrefu halafu mazoezi kidogo ndicho anachofanya kwa Furahisha ambaye ameonekana kuwa na ubora mkubwa ulingoni.

“Wengi wanaamini mazoezi sana unakuta bondia anafanya mazoezi makali halafu usiku unamkuta anazurura huwezi kuwa mzuri kwa sababu unakuwa umechoka na mwili hujaupumzisha vya kutosha,” anasema Mseje na kuongeza

“Huwa tunafanya mazoezi asubuhi saa 4 kisha anakwenda kupumzika na tunamuelekeza apate muda mwingi wa kuuweka mwili sawa na uzuri Hamadi anafanya kwa sababu ni kitu amabcho anakipenda kisha baadae jioni tena kuna mazoezi mengine, kama asubuhi tukifanya Gym jioni maazoezi ya ulingoni.”


MSI 06

MWAKINYO, KIDUKU KIOO

Licha ya hayo, anawataja mastaa kama Hassan Mwakinyo na Twaha Kiduku kuwa ni vioo na malejendi wa ngumi za Tanzania kutokana na namna walivyojitengenezea majina na kuwavuta mashabiki wengi kuupenda mchezo huo.

“Mwakinyo na Kiduku wameonyesha njia kubwa sana wao ni kioo cha ngumi zetu. Hata hivyo, ili kufika mbali zaidi, mabondia wetu wanatakiwa kubadilisha mfumo wa kujiandaa na kuacha mazoea yanayoshusha viwango vyao,” anaongeza.

Anasisitiza kuwa mafanikio ya mabondia hao wawili yanapaswa kuwa chachu kwa vijana wadogo wanaochipukia ili wajue kuwa ngumi zinalipa endapo zitachezwa kwa nidhamu, kujituma, na kufuata misingi sahihi ya kitaalamu na kibiashara.


MSI 07

LISHE CHANGAMOTO

Eneo ambalo Mseje analizungumzia kwa uzito mkubwa ni suala la lishe na afya kwa mabondia wa Tanzania. Anaonya kuwa kutokuwa na uangalifu kwenye lishe na kupunguza uzito kupita kiasi kwa muda mfupi  kunachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha afya za wachezaji na hata kuhatarisha maisha yao uwanjani.

“Lishe ni jambo la msingi sana. Mabondia wengi wanakufa ulingoni au kupotea mapema kwenye tasnia kwa sababu hawazingatii mpango sahihi wa lishe. Mtu anapunguza uzito kwa njia za mkato kiasi kwamba mwili unakuwa dhaifu, pindi apigwapo ulingoni kinakuwa kifo au dharuba nzito,” anasema kocha huyo

Anasisitiza kuwa ili bondia adumu kwa muda mrefu, lazima azingatie ratiba ya kula vyakula vinavyojenga miili yao na kupumzisha misuli kulingana na ushauri wa wataalam na makocha wao.


MSI 04

PAMBANO DESEMBA

Kocha huyo anasema wanaendelea na mazoezi wakijiandaa na pambano la mwezi Desemba ambalo hakutaka kuliweka wazi hadi mambo yatakapokuwa sawa.

“Ni kweli tunajiandaa na mechi itapigwa hapa mwezi wa 12 ila sisi hatuwezi kumtaja mpinzani wetu hadi atakaposema ila tunapambana kuhakikisha mambo yanakuwa sawa na kama mnavyojua muda wowote tuko tayari na mechi.”


KINACHOWAFELISHA KIMATAIFA

Kocha huyo anasema kinachowafelisha mabondia wengi kushindwa kufanya vizuri kimataifa hasa wanapokutana na mabondia wagumu ni pamoja na mechi za mchongo wanazotengenezewa Tanzania.

“Unajua unapopigana na mpinzani mgumu ndio unapata ladha sasa kama unapewa ushindi wa mezani unategemea kimataifa utafanyaje na kule yanaandaliwa na mapromota tofauti unakutana na majaji wengine kabisa.”

“Mimi nasema mechi za kupeana sio nzuri kwa sababu hutafika mbali unaweza kupata umaarufu hapa lakini nyuma tayari umeshatengenezewa michongo lakini kwenye maisha ya ngumi hakuna kitu kama hicho piga mazoezi sana.”


MSI 05

VIKIACHWA HIVI

Anaamini jambo la upendeleo kwenye ngumi likipigwa vita linaweza kusaidia tasnia hiyo kwa kiasi kikubwa na kufanya mchezo huo ukue zaidi.

“Ngumi zimekua ndio maana ukisikia pambano la bondia fulani mashabiki wanajazana kwenda kuangalia pambano lakini bado kuna changamoto za upendeleo hasa kwa baadhi ya majaji pia kumpa bondia ushindi ambaye hakustahili sasa hivi watu wanaona na wanajua aliyecheza vizuri.”