Bondia afariki siku 11 baada ya kichapo cha KO
Muktasari:
- Akushey aliyekuwa akipigana katika uzito wa light heavyweight alisimamishwa katika raundi ya nane na Mghana mwenzake Jacob Dickson.
Accra, Ghana: BONDIA wa Ghana, Ernest Akushey amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 32 siku chache baada ya kupoteza pambano kwa kichapo cha knockout (KO).
Akushey aliyekuwa akipigana katika uzito wa light heavyweight alisimamishwa katika raundi ya nane na Mghana mwenzake Jacob Dickson.
Taarifa zinaeleza baada ya kipigo hicho Septemba 12 huko Accra, Ghana, bondia huyo alianza kulalamika kwamba hajisikii vizuri na hali yake iliendelea kubadilika siku hadi siku mpaka alipofariki dunia jana, Jumanne, Septemba 23.
Akushey alikuwa anaheshimika zaidi katika jumuiya ya mabondia wa Ghana kutokana na uthubutu na mtindo aliokuwa nao wa kupigana bila woga. Kifo chake kimewaumiza Waghana wengi hasa katika mji aliozaliwa wa Chorkor.
Bondia huyo alianza ngumi za kulipwa 2019 na kushinda mapambano sita ya kwanza kabla ya kufuzu kwa pambano la ubingwa wa light heavyweight nchini humo, Mei mwaka huu.
Akushey alipoteza pambano hilo kwa TKO ya raundi ya saba dhidi ya Jonathan Tetteh kabla ya kupoteza tena la pili mfululizo ndani ya muda mfupi dhidi ya Dickson ikiwa ni miezi minne baadaye.
Katika pambano lake la mwisho dhidi ya Dickson alipokea vipigo kadhaa mfululizo kichwani vya ngumi za mkono wa kulia kabla ya kuanguka chini.
Mpinzani wake, Dickson, ameongoza utoaji heshima kupitia taarifa ya hisia aliyoichapisha kwenye mtandao wa Instagram akisema: “Nimeumizwa sana na nina huzuni kubwa kusikia kuhusu kifo cha Ernest Akushey (Bahubali).
“Ingawa tulikuwa wapinzani nilikuwa naheshimu nguvu zako, ujasiri na moto uliokuwa ndani ya moyo wako. Tulipokuwa wapinzani bado ulikuwa unanipata heshima kwa kila namna.
“Nianjisikia vibaya kujua kwamba haupo tena na hakika siamini. Hili ni pigo kubwa na siyo tu kwa wale waliokujua na kukupenda, bali kwa kila mtu aliyewahi kushuhudia pambano ulilocheza, moyo na utu wako.
“Maisha mara nyingine huwa ya ajabu katika wakati wake. Mara moja tunazichapa kama wapinzani, wakati mwingine tunalia kama binadamu.”
Shirikisho la Michezo Ghana (NSA), pia limetuma rambirambi kwa familia ya Akushey anayekuwa bondia wa nne kufariki dunia kutokana na madhara ya ngumi mwaka huu.
Bondia wa Ireland, John Cooney alifariki dunia Februari ikiwa ni siku saba baada ya kupoteza dhidi ya Mwingereza Nathan Howells.
Kabla ya mauti Cooney alitokwa damu nyingi ndani ya fuvu na kufanyiwa upasuaji kupunguza shinikizo la damu kwenye ubongo, lakini akafariki wiki moja baada ya pambano.
Agosti nchini Japan mabondia wawili walifariki dunia katika tukio moja, ambapo Shigetoshi Kotari alivuja damu kwenye ubongo baada ya kupigana raundi 12 dhidi ya Yamato Hata — pambano lililoisha kwa sare.
Agosti 8, siku tano tu baada ya pambano hilo, Kotari alitangazwa kufariki dunia.
Naye Hiromasa Urakawa aliyepigana kwenye ulingo mmoja na Kotari akapigwa knockout katika raundi ya nane na Yoji Saito alipoteza maisha kwa kuvuja damu kwenye ubongo na kufariki dunia Agosti 9.
Mwaka jana mabondia wanne walifariki dunia akiwemo Sherif Lawal kutoka Uingereza ambaye alipigwa knockout na Malam Varela katika pambano lake la kwanza la kulipwa.