BOLKIAH: Mchezaji tajiri kuliko Messi, Ronaldo
Muktasari:
- Hata hivyo, tofauti na wachezaji wengi ambao hutajirika kupitia mishahara na mikataba minono ya timu na kampuni, Faiq anaingiza pesa kupitia urithi mkubwa kutoka kwa familia yake inayomiliki hisa katika sekta za kampuni mbalimbali duniani pamoja na madili yake mengine anayopiga kama mshahara wa timu na mikataba ya udhamini.
BANDAR SERI BEGAWAN, BRUNEI: FAIQ Jefri Bolkiah si jina maarufu katika ulimwengu wa soka. Ni mtoto katika familia ya kifalme ya Brunei ambaye anatajwa kuwa mchezaji wa soka mwenye utajiri mkubwa zaidi duniani, akiwazidi hata mastaa kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Hata hivyo, tofauti na wachezaji wengi ambao hutajirika kupitia mishahara na mikataba minono ya timu na kampuni, Faiq anaingiza pesa kupitia urithi mkubwa kutoka kwa familia yake inayomiliki hisa katika sekta za kampuni mbalimbali duniani pamoja na madili yake mengine anayopiga kama mshahara wa timu na mikataba ya udhamini.
Hapa chini tumekuchambulia utajiri wa staa huyu mwenye umri wa miaka 27 na namna anavyoishi kishua.
ANAPIGAJE PESA
Bolkiiah, anatokea familia ya kifalme ya Brunei pia ni mtoto wa Prince Jefri Bolkiiah. Anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 20 bilioni.
Kiasi hicho cha utajiri wake ndio kimemfanya kuwa mchezaji tajiri kuliko hata Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Kiasi kikubwa cha mali yake kinatokana na urithi alionao katika ufalme. Familia yake ina hisa kubwa katika sekta ya mafuta, gesi, nyumba na majengo mengine pamoja na biashara zilizopo Brunei na sehemu nyingine duniani kama London, England, Dubai, UAE, Monte Carlo, Ufaransa na Beverly Hills, Marekani.
Vilevile anapata pesa kupitia mshahara wake anaolipwa na timu anayoichezea kwa sasa ambayo Ratchaburi FC inayoshiriki Ligi Kuu Thailand, ambako kwa mwezi anapata dola 2,900 ambao ni mshahara mdogo ukilinganishwa na nyota wakubwa wa ligi kuu za Ulaya
Inaelezwa pia staa huyu ni balozi wa kampuni kadhaa za huko Brunei ambako kwa pamoja ndani ya mwaka humwezesha kupata Dola 100,000.
NYUMBA
Kama sehemu ya urithi wake, staa huyu anamililki mijengo ya kifahari ndani na nje ya Brunei ambayo kwa asilimia kubwa hutumika kama sehemu ya biashara.
Muda mwingi baada ya kurudi kwa ajili ya mapumziko ya kumaliza msimu huwa anaonekana sana Brunei badala ya hizo sehemu nyingine ambako kuna nyumba za familia yake.
MSAADA KWA JAMII
Ingawa Faiq hajashiriki sana hadharani katika masuala ya misaada kwa jamii, anatambulika sana kusaidia kupitia familia yake ambayo imekuwa ikiendesha miradi mbalimbali inayohusu elimu, huduma za afya, maendeleo ya kijamii, pamoja na maendeleo ya vijana kupitia michezo na mafunzo.
Kwa asilimia kubwa amekuwa akishiriki katika upangaji wa miradi hiyo.
VITU VYA KIFAHARI
Jamaa anamiliki saa za gharama kama Patek Philippe na Rolex. Pia, taarifa zinaeleza anapenda sana wanyama na huko katika jengo analokaa anamiliki wanyama hatari kama chui na tiger.
Hata hivyo, hadi sasa anadaiwa kuwa hajaoa ingawa baadhi ya watu wanaamini ameoa kwa siri.
Baadhi ya taarifa zake zimetunzwa kwa siri sana kwa kutokana na hadhi yake katika ufalme wa Brunei.
Aliwahi kucheza katika timu za vijana za Chelsea, Leicester City pamoja na Southampton.