Bifu la Scholes, Martinez limefikia patamu balaa
Muktasari:
- Kiungo huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 51 alimdhihaki vikali mshindi huyo wa Kombe la Dunia kabla ya kukutana na wapinzani wao wakubwa, Manchester City kwenye kipute cha Manchester derby, Jumamosi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: KUMEKUCHA. Mvutano kati ya Paul Scholes na beki wa Manchester United, Lisandro Martinez hauonekani kumalizika hivi karibuni baada ya gwiji huyo wa Old Trafford kujibu kwa mzaha kupitia mitandao ya kijamii.
Kiungo huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 51 alimdhihaki vikali mshindi huyo wa Kombe la Dunia kabla ya kukutana na wapinzani wao wakubwa, Manchester City kwenye kipute cha Manchester derby, Jumamosi iliyopita.
Scholes, akizungumza kwenye redio mtandao ya The Good, The Bad and The Football, alidai Martinez angekuwa na kazi ngumu sana dhidi ya Erling Haaland. Hata hivyo, beki huyo ndiye aliyekuwa na kicheko cha mwisho katika mechi ya kwanza ya Michael Carrick akiwa kocha wa muda wa Man United na alimdhibiti vikali Haaland, ambaye hakupata nafasi hata moja ya kupiga shuti hadi alipotolewa.
Mashetani Wekundu waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa, mabao yakifungwa na Bryan Mbeumo na Patrick Dorgu kwenye kipindi cha pili. Martinez, 28, alimjibu Scholes baada ya kufahamishwa kuhusu kauli zake.
Muargentina huyo, ambaye aliwahi kufikiria kuacha soka baada ya kuumia goti (ACL) mwaka jana, alisema: “Kwa kweli, anaweza kusema chochote anachotaka.
“Nimemwambia tayari, kama anataka kuniambia jambo lolote, anaweza kuja popote anapotaka. Nyumbani kwangu, mahali popote. Sijali.
“Na kwa upande wangu, naheshimu mahusiano pale wanapotaka kusaidia klabu, kwa sababu kila mtu anaweza kuzungumza akiwa kwenye televisheni.
“Lakini mkikaa uso kwa uso, hakuna anayesema chochote moja kwa moja. Hivyo basi, sijali wanachosema. Ninaweka umakini wangu kwenye kiwango changu, kiwango cha timu na nitatoa kila kitu kwa klabu hii hadi siku yangu ya mwisho.”
Lakini, Scholes anaonekana kutaka neno la mwisho na kwa mshangao akaonyesha yuko tayari kukubali mwaliko wa Martinez wa kukutana ana kwa ana.
Mchezaji huyo wa zamani wa England aliandika oda yake ya kinywaji alipoweka ujumbe kwenye Instagram Stories.
Scholes aliandika: “Mtu fulani amecheza mechi nzuri, nilifurahi sana kwa ajili yako… Chai, tafadhali bila sukari.”
Akizungumza kabla ya mechi kwenye redio mtandao hiyo, Scholes alisema kwa wasiwasi: “Martinez dhidi ya Haaland… unahitaji Matthijs De Ligt na Harry Maguire warudi kwa hilo.”
Nicky Butt, aliyekuwa pamoja na Scholes, aliongeza: “Haaland angemchukua Martinez na kukimbia naye. Itakuwa kama baba anayemkimbiza mtoto mdogo baada ya shule. Ndivyo itakavyokuwa.”
Scholes kisha akaongeza kwa mzaha: “Angefunga bao halafu amtupe ndani ya wavu.”
Martinez alimzuia mfungaji bora wa Ligi Kuu, Haaland, asifanye lolote wakati wa dabi ya Manchester. Mchezaji huyo wa zamani wa Ajax atarejea uwanjani wakati Man United itakapokwenda kukabiliana na vinara wa ligi Arsenal, Jumapili hii.