Bifu la Mourinho, Casillas sasa ni hatari zaidi
Muktasari:
Wakati huu ambapo Mourinho amekuwa akihusishwa kurudi zake Chelsea baada ya kukutana katika chakula cha jioni na tajiri wa timu hiyo, Roman Abramovich, inaonekana hajali kuhusu hali ya baadaye ya Real Madrid na bifu baina yake na Casillas liko wazi zaidi.
BIFU baina ya kocha wa Real Madrid mwenye maneno mengi, Jose Mourinho na aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Iker Casillas ambaye anasugulishwa benchi na kipa Diego Lopez aliyenunuliwa kutoka Sevilla Januari mwaka huu, limezidi kuwa kubwa.
Wakati huu ambapo Mourinho amekuwa akihusishwa kurudi zake Chelsea baada ya kukutana katika chakula cha jioni na tajiri wa timu hiyo, Roman Abramovich, inaonekana hajali kuhusu hali ya baadaye ya Real Madrid na bifu baina yake na Casillas liko wazi zaidi.
Adai amechelewa kumsajili Lopez
Katika kuonekana kuwaumiza moyo mashabiki wa Real Madrid ambao wanaamini kuwa Mourinho anamkosea heshima shujaa wao Casillas kwa kumpiga benchi, Mourinho ameshindilia msumari wa moto katika kidonda hicho kwa kudai kwamba alichelewa kumsajili Lopez.
“Kuna kitu chochote ambacho ningepewa nafasi ya kubadili katika miaka mitatu iliyopita? Nadhani ningemleta Diego Lopez katika mwaka wangu wa kwanza. Hatukufanya jitihada kubwa za kumsajili. Ni fedheha.” Alisema Mourinho.
Maneno hayo yalikuwa yanamaanisha kwamba Lopez amefanya kazi nzuri sana tangu asajiliwe kutoka Sevilla Januari mwaka huu na kwamba angekuwa ameshachukua nafasi ya Casillas tangu miaka mitatu iliyopita.
Kwa mara ya kwanza Mourinho alimpiga benchi Casillas katika pambano dhidi ya Malaga la Desemba22, 2012 ikiwa ni mara ya kwanza kwa kipa huyo kukaa benchi baada ya miaka 10 ya kucheza mfululizo.
Badala yake Mourinho alimpanga kipa, Lopez ambaye alichangia katika kipigo cha mechi hiyo. Mwishowe Mourinho alitoa kauli ya kushangaza kuwa kipa huyo alikuwa bora kuliko Casillas.
“Nayachukua maoni ya wasaidizi wangu. Waliamua Casillas akae katika benchi. Tunaelewa kuwa kwa sasa Lopez ni bora kuliko Casillas."
Mourinho azomewa, Casillas ashangiliwa
Katika pambano la Ligi Kuu Hispania dhidi ya Real Valladolid, dakika sita kabla ya mechi hiyo haijaanza, mashabiki 30,000 waliokuwa jukwaani walianza kupiga kelele za kumzomea Mourinho mara picha yake ilipoonekana katika televisheni ya uwanja wa Santiago Bernabeu huku mtangazaji akitaja jina lake. Lakini lilipotajwa jina la Iker Casillas mashabiki walilipuka kwa furaha na kushangilia.
Pepe amlaumu Mourinho
Kufuatia madai kwamba alichelewa kumsajili kipa Diego Lopez, beki wa Real Madrid, Pepe ambaye ni raia mwenzake wa Ureno alijitokeza hadharani na kumshambulia Mourinho kuwa hakufanya kitendo cha kiungwana kutoa madai hayo, huku akidai kwamba alikuwa anamkosea heshima Casillas ambaye anaheshimika na mashabiki wa klabu hiyo pamoja na taifa zima la Hispania.
“Inabidi tuwe na heshima kidogo kwa Iker. Maneno ya bosi hayakuwa mazuri. Iker ni kama taasisi kwa klabu hii na Hispania. Inabidi ajue kuwa sisi wachezaji na mashabiki tupo nyuma ya kipa huyu,” alisema Pepe mara baada ya ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Valladolid.
Chilavert ambwatukia Mourinho
Kipa mahiri wa zamani wa timu ya taifa ya Paraguay, Jose Luis Chilavert, amembwatukia Mourinho kutokana na kitendo chake cha kumweka benchi Casillas huku akisema haki haitendeki.
“Ni kweli kwamba Diego Lopez amekuwa akifanya kazi nzuri, lakini kwa heshima aliyonayo Casillas kutokana na rekodi yake nzuri Real Madrid ilibidi acheze mechi,” alisema.
“Hauwezi tu kumuweka katika benchi na akamaliza msimu vibaya. Kuna makipa wachache kama yeye duniani kwa sasa na inabidi watazamwe vizuri.”
Kipa huyo ambaye kwa sasa anaishi katika Jiji la Buenos Aires, nchini Argentina, aliongeza: “Namwomba Iker awe na uvumilivu na busara katika hali kama hii. Lazima aendelee kuwa mpole na akubali kuwa mashabiki wanampenda na wanajua thamani yake.
“Mourinho kama mwanadamu mwingine yeyote, kuna wakati naye anakosea, lakini ukweli halisi ni kwamba bila ya Iker, Real Madrid haina mtu madhubuti katika lango lake.”
Mourinho amshutumu Casillas
Chanzo cha ugomvi mkubwa baina yao inasemekana kilianza Desemba mwaka jana wakati Mourinho alipomshutumu kisirisiri Casillas kuwa amekuwa akivujisha siri za timu hiyo kwa vyombo vya habari vya Hispania.
Mourinho alimkaripia mtangazaji wa redio maarufu ya Marca, Anton Meana, amtajie mtu aliyekuwa akimpa siri za ndani ya klabu hiyo huku ikisemekana kuwa Casillas ndiye ambaye amekuwa akimpa siri hizo mwandishi huyo.
Utaifa umeiua Real Madrid
Chanzo kikubwa cha kudorora kwa uhusiano wa Casillas na Mourinho kimechangiwa pia na ukweli kwamba msimu huu Madrid iligawanyika vipande vipande miongoni mwa wachezaji wanaoongea Kireno wakiongozwa na staa Cristiano Ronaldo pamoja na wale wanaoongea Kihispaniola wanaoongozwa na Casillas na Sergio Ramos.
Inasemekana kuwa uhusiano wa Mourinho na wachezaji wa Kihispaniola ulikuwa duni huku wakati fulani akitajwa kubwatukiana na Ramos kufuatia makosa aliyofanya langoni na mwishowe beki huyo akamwambia Mourinho kuwa hajui analofanya katika suala la ulinzi wa timu kwa sababu yeye mwenyewe hakucheza soka.