Bellingham kala umeme, Real Madrid chali
Muktasari:
- Bellingham alidhani ameipatia Real Madrid penalti baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari wakati timu hiyo ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imekosa nafasi ya kufungana pointi na Barcelona kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) baada ya kukubali kichapo cha kushtukiza cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Alaves.
Matokeo hayo yamezidi kuongeza presha kwa kikosi cha kocha Jose Mourinho, huku kiungo wake Jude Bellingham akitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika za mwisho za mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Bellingham alidhani ameipatia Real Madrid penalti baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari wakati timu hiyo ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Hata hivyo, mwamuzi Cesar Soto Grado alibatilisha uamuzi wake wa awali baada ya kwenda kutazama tukio hilo kwenye kifaa cha VAR kilichopo pembeni mwa uwanja.
Kiungo huyo wa England, ambaye tayari alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano dakika ya 74 kwa kupinga uamuzi wa mwamuzi, alionyeshwa kadi nyingine ya njano kwa kile kilichoonekana kuwa kujirusha ili kupata penalti, na hivyo kutolewa nje ya mchezo.
Hata hivyo, Mourinho aliutetea uamuzi wa mchezaji wake, akisema Bellingham mwenyewe alisisitiza kuwa alistahili kupewa penalti.
"Jude amesema baada ya mchezo kuwa ilikuwa penalti. Mchezaji anaposema ni penalti, ninapaswa kuamini hivyo. Lazima niwaamini wachezaji wangu," amesema Mourinho.
Kocha huyo pia alionekana kumkosoa mwamuzi huyo, akidai kuwa amekuwa na tabia ya kuwaonyesha wachezaji wa Real Madrid kadi nyekundu katika misimu tofauti.
"Misimu miwili iliyopita alimtoa Kylian Mbappe, msimu uliopita akamtoa Vinicius Junior na msimu huu ni Jude Bellingham. Tusubiri kuona kama msimu ujao atakuwa Thibaut Courtois," amesema Mourinho.
Hata hivyo, Mourinho alisisitiza kuwa hakutaka kutumia uamuzi wa mwamuzi kama sababu ya kushindwa kwa timu yake.
"Naamini mwamuzi huyu anapenda kuonyesha mamlaka yake. Ni wazi sitaki kusema tumepoteza kwa sababu ya mwamuzi. Sikupendezwa na namna alivyoendesha mchezo, lakini hatukupoteza kwa sababu yake," ameongeza.
MAKOSA YA ULINZI YAIGHARIMU REAL
Licha ya Real Madrid kutawala sehemu kubwa ya mchezo na kutengeneza nafasi nyingi za wazi za kufunga, ilijikuta ikianza kuwa nyuma baada ya Toni Martinez kuifungia Alaves bao la kwanza dakika ya 22.
Bao hilo lilitokana na kosa la beki Dean Huijsen, aliyepiga pasi dhaifu ya kurudisha mpira kwa kipa Thibaut Courtois.
Martinez aliwahi mpira huo, akampita Courtois na kuutumbukiza wavuni huku Ibrahima Konate akijaribu kuokoa bila mafanikio.
Akitafuta namna ya kubadilisha mwenendo wa mchezo, Mourinho alifanya mabadiliko wakati wa mapumziko kwa kuwaingiza Yan Diomande na Bernardo Silva.
Dakika tatu tu baada ya kuanza kipindi cha pili, Alaves ilidhani imeongeza bao la pili kupitia Abde Rebbach, aliyempita Federico Valverde kabla ya kupiga shuti lililomshinda Courtois.
Hata hivyo, bao hilo lilikataliwa kutokana na Rebbach kuwa ameotea.
Real iliendelea kukumbwa na matatizo ya ulinzi na dakika ya 58 ilijikuta nyuma kwa mabao 2-0 baada ya Angel Perez kutumia uzembe wa safu ya ulinzi kuvunja mtego wa kuotea na kuufunga mpira katika lango la Courtois.
Mourinho aliendelea kufanya mabadiliko akiwatumia Bernardo Silva na Carlos Espi, ambao walikaribia kuifungia Real mabao kabla ya Kylian Mbappe kupunguza pengo dakika ya 69.
Mbappe alifunga bao hilo kwa shuti kali lililoishia kwenye sehemu ya juu ya nyavu za Alaves, akiipa Real matumaini ya kurejea mchezoni.
Baada ya bao hilo, Real iliendelea kutawala mchezo na kumiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 74, lakini ilishindwa kupata bao la kusawazisha.
Tukio la Bellingham kuanguka ndani ya eneo la hatari na uamuzi wa mwamuzi kubatilisha penalti vilikuwa miongoni mwa matukio makubwa ya dakika za mwisho, kabla Real haijaondoka uwanjani ikiwa imepoteza kwa mara ya kwanza katika mechi 11.
Kipigo hicho kimekuwa pigo kwa Real Madrid katika mbio za ubingwa wa La Liga, huku Barcelona ikiendelea kuwa na nafasi ya kuimarisha uongozi wake kileleni.