Kimmich aivaa Bayern Munich ishu ya Musiala
Muktasari:
- Kimmich amesema Bayern imekosea kuibua mjadala wa hadharani kuhusu mustakabali wa Musiala, akisisitiza kuwa masuala hayo yalipaswa kujadiliwa kwa faragha kati ya uongozi wa klabu, mchezaji na wawakilishi wake.
MUNICH, UJERUMANI: NAHODHA wa Bayern Munich, Joshua Kimmich ameikosoa vikali klabu hiyo kwa kile alichokiita kitendo kisichoeleweka na kisichokubalika cha kuzungumzia hadharani masuala ya afya na mkataba wa Jamal Musiala, ambaye amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya.
Kimmich amesema Bayern imekosea kuibua mjadala wa hadharani kuhusu mustakabali wa Musiala, akisisitiza kuwa masuala hayo yalipaswa kujadiliwa kwa faragha kati ya uongozi wa klabu, mchezaji na wawakilishi wake.
Musiala, mwenye umri wa miaka 23, ni miongoni mwa vipaji vikubwa vya soka la Ujerumani, lakini amekuwa na wakati mgumu kutokana na majeraha na changamoto za kiafya zilizomfanya akose michezo mingi msimu huu.
Kiungo huyo anatajwa kulipwa mshahara wa takribani pauni milioni 18 kwa mwaka, huku akiwa na mkataba wa Bayern hadi mwaka 2030.
Mvutano huo ulianza kushika kasi baada ya mmoja wa viongozi wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge, kupendekeza kuwa klabu inaweza kujadiliana na Musiala kuhusu kupunguza mshahara wake endapo hatarejea katika kiwango chake cha zamani.
Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa katika ulimwengu wa soka, huku mastaa mbalimbali akiwemo Jude Bellingham, Michael Olise na Rio Ferdinand wakionyesha kumuunga mkono Musiala.
Akizungumza baada ya Bayern kupoteza mabao 2-1 dhidi ya Lille katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku, Kimmich hakuficha hasira zake.
"Kilichotokea sasa hakikupaswa kutokea kwa namna hii. Kwangu mimi, jambo hili halieleweki kabisa.
"Nadhani mambo kama haya yanapaswa kujadiliwa faraghani. Mnaweza kuzungumza na wakala wa Jamal au hata yeye mwenyewe. Kile nisichokielewa ni namna suala hili linavyowasilishwa hadharani.
"Haiwezi kukubalika mchezaji mmoja kubebeshwa lawama zote. Ni kweli klabu inakuja kwanza na ni kubwa kuliko sisi wachezaji, lakini si kubwa kuliko utu wa mtu. Hilo halikubaliki kabisa," alisema Kimmich.
Aliongeza kuwa namna Bayern ilivyoshughulikia suala hilo si utamaduni wa klabu hiyo, hasa katika kipindi ambacho imekuwa ikijivunia mshikamano na umoja wake.
AMTETEA MUSIALA
Kimmich pia alisisitiza kuwa matatizo ya Musiala hayajatokana na kukosa nidhamu au kutokuwa na bidii katika mazoezi.
Alisema amekuwa akimuona kiungo huyo kila siku na kushuhudia juhudi zake za kurejea katika kiwango bora.
"Tusisahau kuwa alifanyiwa upasuaji mwingine wakati wa majira ya kiangazi, kisha akapata jeraha jingine.
"Ninamuona kila siku na ninajua jinsi anavyofanya kazi kwa bidii. Si kwamba ana matatizo haya kwa sababu hana weledi au hajitumi. Kinyume chake, yupo hapa kila siku, anafanya kazi kwa juhudi kubwa na anatamani kuipa timu yake kilicho bora.
"Natumaini anafahamu kuwa sisi sote tupo nyuma yake kwa asilimia 100, kuanzia wachezaji hadi viongozi wa klabu," alisema.
Hata hivyo, Kimmich alikiri kuwa anaelewa changamoto ya kifedha inayokabili Bayern kutokana na kuwa na mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa lakini ameshindwa kucheza mara kwa mara kutokana na matatizo ya kiafya.
Alisema Musiala amepitia safari ngumu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, licha ya kuwa alikuwa miongoni mwa wachezaji waliobeba matumaini ya Bayern na timu ya taifa ya Ujerumani.
VIONGOZI WA BAYERN WAMZUNGUMZIA
Musiala aligundulika kuwa na tatizo la 'absence seizures', aina ya kifafa kinachosababisha mtu kupoteza fahamu kwa muda mfupi kutokana na shughuli zisizo za kawaida za umeme kwenye ubongo.
Mchezaji huyo aliwashangaza mashabiki baada ya kuanguka mara mbili ndani ya kipindi kifupi msimu huu. Kocha wa Bayern, Vincent Kompany, alieleza kuwa tukio moja lilihusishwa na mwitikio wa mwili wake baada ya mabadiliko ya dawa alizokuwa akitumia.
Rais wa heshima wa Bayern, Uli Hoeness, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kuzungumzia athari za ugonjwa huo, akieleza kuwa Musiala huenda asirejee katika kiwango alichokuwa nacho awali.
Hoeness alisema klabu inakabiliwa na hali ngumu kwa sababu ugonjwa wa mchezaji huyo hauwezi kuondolewa kirahisi, ingawa unaweza kudhibitiwa kwa msaada wa dawa.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bayern, Jan-Christian Dreesen, alisema klabu itaendelea kufuatilia kiwango cha Musiala kabla ya kufanya tathmini ya mustakabali wake.
Kauli hizo zilifuatwa na Rummenigge, ambaye naye aliona kuna uwezekano wa kujadili upya masharti ya mkataba wa kiungo huyo endapo hatarudi katika kiwango chake cha zamani.
FIFPRO YAINGILIA KATI
Mvutano huo uliifikia pia chama cha kimataifa cha wachezaji wa kulipwa, FIFPRO, ambacho kilikosoa vikali namna viongozi wa Bayern walivyokuwa wakizungumzia mkataba wa Musiala hadharani.
Katika taarifa yake, FIFPRO ilisema kauli zilizotolewa kwa mfululizo na viongozi wa Bayern zinaonekana kuwa mkakati wa kumwekea shinikizo mchezaji huyo pamoja na wawakilishi wake kabla ya mazungumzo yoyote ya kimkataba.
Chama hicho kilisema klabu kubwa kama Bayern inapaswa kuwa na uelewa zaidi kuhusu namna ya kushughulikia masuala yanayohusu afya na mikataba ya wachezaji.
Nchini Ujerumani, Makamu wa Rais wa chama cha wachezaji, Michael Franz, alienda mbali zaidi kwa kuikosoa klabu hiyo na kueleza kuwa mwenendo wa baadhi ya viongozi wake unafanana na unyanyasaji.
Franz alisema hakuna tatizo kujadili kiwango cha mchezaji uwanjani, lakini si sahihi kuzungumzia ugonjwa wake na mshahara wake kwa namna inayoweza kumuumiza kisaikolojia.
Alisisitiza kuwa Musiala amefanya kila linalowezekana kurejea uwanjani.
AANZA KUREJEA
Musiala alianguka mara mbili ndani ya siku nne katikati ya Agosti, kwanza katika mchezo dhidi ya RB Leipzig muda mfupi baada ya kufunga bao, kisha akakumbwa na tukio jingine dhidi ya Heidenheim.
Alirejea uwanjani Septemba na kufanikiwa kufunga mabao katika michezo dhidi ya Bodo/Glimt kwenye Ligi ya Mabingwa na Union Berlin.
Hata hivyo, jeraha la misuli ya nyuma ya paja lilimrudisha tena nje ya uwanja kabla ya kuanza kurejea mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika mchezo dhidi ya Lille, Musiala aliingia akitokea benchi na kucheza dakika 15 za mwisho, ingawa Bayern ilipoteza kwa mabao 2-1.
Kwa sasa, macho ya mashabiki wa Bayern yanaendelea kumtazama kiungo huyo, huku mjadala mkubwa ukiwa si tu kuhusu kurejea kwake uwanjani, bali pia namna klabu itakavyosimamia mustakabali wa mmoja wa vipaji vyake vikubwa.