Real Madrid ya Mourinho inayotisha kotekote
Muktasari:
- Hilo ndilo lilikuwa jibu la kiungo Jude Bellingham alipoulizwa kueleza siri ya kiwango chake bora hivi karibuni, baada ya kuingia kipindi cha pili na kuisaidia Real Madrid kugeuza matokeo dhidi ya PSV na kupata ushindi mnono.
AMSTERDAM, UHOLANZI: BAADA ya Real Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya PSV Eindhoven, wakitoka nyuma kwa bao moja, sasa wamepanda kileleni mwa msimamo wa hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Je, José Mourinho anaweza kuiongoza timu hiyo kutwaa tena ubingwa wa Ulaya?
“Mourinho. Hakuna mwingine.”
Hilo ndilo lilikuwa jibu la kiungo Jude Bellingham alipoulizwa kueleza siri ya kiwango chake bora hivi karibuni, baada ya kuingia kipindi cha pili na kuisaidia Real Madrid kugeuza matokeo dhidi ya PSV na kupata ushindi mnono.
Bellingham alisema: “Nampenda kocha, benchi lake la ufundi na wachezaji wenzangu wananisaidia sana. Ndiyo maana ninacheza vizuri kwa sababu ninapata msaada mkubwa.”
Kwa kuangalia mwenendo wa Mourinho katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya watu walikuwa wameanza kuamini kwamba amepoteza makali ya kuifundisha timu katika kiwango cha juu kabla ya kurejea kwake Santiago Bernabéu msimu huu.
Ubora wa timu alizokuwa akizifundisha ulionekana kushuka tangu alipomaliza kipindi chake cha mwisho Real Madrid mwaka 2013.
Baada ya kuondoka Tottenham Hotspur mwaka 2021, alikwenda AS Roma, kisha Fenerbahçe ya Uturuki kabla ya kujiunga na Benfica ya Ureno. Wachache walitarajia angerudi kwenye ligi kubwa Ulaya na kufanya vizuri kiasi hiki.
Hata hivyo, Mourinho amekuwa mtu wa kushangaza mara kwa mara. Ushindi dhidi ya PSV umeifanya Real Madrid kufikisha ushindi 10 mfululizo.
Kwa sasa wanaongoza msimamo wa hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa wakiwa wameshinda mechi zote tano. Pia, baada ya kuanza vibaya kwenye mashindano ya ndani, wamepunguza pengo la pointi dhidi ya vinara wa La Liga, Barcelona, hadi tatu.
Baada ya misimu miwili iliyopita isiyo na mafanikio makubwa, ambapo hawakutwaa taji lolote kubwa, kikosi cha Mourinho sasa kinaonekana kuwa na uwezo wa kupambana kuwania mataji katika mashindano yote. Kama Bellingham anavyosema, kocha huyo amekuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko hayo.
KAGEUZA PICHA MADRID
Baada ya kucheza mechi saba za ligi, Real Madrid walikuwa wameachwa kwa pointi sita na Barcelona iliyokuwa na mwanzo mzuri wa msimu. Katika kipindi hicho walikuwa wamepoteza mechi mbili.
Hali hiyo ilisababisha wengi kuamini kuwa Mourinho asingekuwa na uwezo wa kuirekebisha timu hiyo. Hata hivyo, vipigo hivyo vilikuwa na sababu zake.
Katika mchezo wa kupoteza kwa mabao 1-0 dhidi ya Real Betis, Madrid walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini wakashindwa kuzitumia.
Katika kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Atlético Madrid, kadi nyekundu aliyoonyeshwa Dean Huijsen mwanzoni mwa kipindi cha pili ilibadilisha mwelekeo wa mchezo.
Tangu kipigo hicho, Madrid wameshinda mechi 10 mfululizo, ukiwemo ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Barcelona katika mchezo wa El Clásico uliofanyika Camp Nou mwezi uliopita.
Kwa ujumla, Madrid wamepata ushindi mara 16 katika mechi 18 tangu Mourinho arejee kuinoa timu hiyo.
Barcelona nao wamekuwa na mwendo mzuri kileleni mwa La Liga, wakiwa wameshinda mechi 12 kati ya 13. Kasi hiyo imeifanya vita ya ubingwa kuwa ngumu, lakini kiwango cha sasa cha Madrid kinaonyesha wana uwezo wa kuendelea kupambana, huku Atlético Madrid wakishikilia nafasi ya tatu.
DAKIKA ZA JIONI, KUREJEA MCHEZONI
Kama ilivyo kawaida kwa timu nyingi zilizowahi kufundishwa na Mourinho, safari ya Real Madrid msimu huu haijawa na utulivu kila wakati. Kumekuwa na ushindi mwingi wa dakika za mwisho na uwezo wa kugeuza matokeo.
Tayari msimu huu, Madrid wameshinda mechi nne kupitia mabao yaliyofungwa dakika ya 90, huku mechi nyingine mbili wakipata mabao ya ushindi kuanzia dakika ya 85 na kuendelea.
Baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya PSV, walioupata baada ya kuruhusu bao la kwanza kipindi cha kwanza, Madrid wamegeuza matokeo mara tatu katika mechi zao nne zilizopita.
Ushindi huo pia ulikuwa miongoni mwa ushindi mkubwa katika historia ya Ligi ya Mabingwa kwa timu iliyokuwa nyuma kwa bao moja au zaidi wakati wa mapumziko.
Madrid walikuwa wakifanana na Lazio iliyoshinda Shakhtar Donetsk mabao 5-1 Oktoba 2000 na Bayern Munich iliyoichapa Arsenal kwa matokeo hayo Machi 2017.
Mourinho anastahili pongezi kwa namna alivyoweza kujenga mshikamano ndani ya kikosi chake, kiasi kwamba wachezaji hawakati tamaa hata wanapokuwa nyuma kwenye mchezo. Hali hiyo ilikosekana wakati wa makocha waliomtangulia, Xabi Alonso na Álvaro Arbeloa.
NAMBA VS FALSAFA
Takwimu zinaonyesha mabadiliko ya falsafa ya Madrid. Msimu huu wanamiliki mpira kwa wastani wa asilimia 53.9 katika mechi za La Liga. Hicho ndicho kiwango chao cha chini zaidi cha umiliki wa mpira katika msimu mmoja tangu 2008/09.
Hata hivyo, wamekuwa wakitumia vizuri mashambulizi ya kushtukiza. Wanapiga wastani wa mashuti mawili kwa kila mchezo kupitia mashambulizi ya haraka, idadi kubwa zaidi ikilinganishwa na misimu yao iliyorekodiwa tangu 2005/06.
Katika kipimo cha PPDA, kinachoonyesha kiwango cha timu katika kuzuia wapinzani kupiga pasi kabla ya kuingilia mchezo, Madrid wanashika nafasi ya 12 La Liga kwa wastani wa 13.1.
Pia wamefanya mashambulizi ya moja kwa moja mara 42, idadi kubwa kuliko timu nyingine yoyote katika ligi hiyo. Katika mechi 13 za La Liga, Madrid wamefunga mabao 33 na kuruhusu 11 pekee.
Takwimu hizo za ulinzi zina umuhimu mkubwa ikizingatiwa kuwa katika miaka ya hivi karibuni timu hiyo imekuwa na matatizo ya kujilinda.
Jambo lililovutia zaidi ni namna walivyofanikiwa kuizuia Barcelona katika mchezo wa El Clásico, hasa ikizingatiwa kuwa katika mechi zao nane zilizotangulia walikuwa wameruhusu jumla ya mabao 24.
Mourinho amekuwa akijulikana kwa uwezo wake wa kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kuwafanya kuwa na umoja ndani ya kikosi. Namna alivyoweza kuigeuza Real Madrid kuwa timu yenye mshikamano, inayocheza kwa ushirikiano na kupambana hadi mwisho, inastahili pongezi.
Iwapo wataendelea na kiwango hicho, hakuna sababu ya kuamini kwamba kikosi chake hakiwezi kurejea kwenye mafanikio ya kutwaa mataji makubwa.
Baada ya wengi kufikiri kwamba Mourinho alikuwa amemaliza safari yake katika kiwango cha juu cha soka la Ulaya, kazi anayoifanya sasa Real Madrid inaweza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi katika maisha yake ya ukocha.