Bayern Munich haijakata tamaa kwa Nico Williams

Muktasari:
- Vigogo wa Bayern wana matumaini kwa sababu wanaamini huenda Barca ikashindwa kulipa gharama za ada ya uhamisho kutokana na hali yao ya kiuchumi.
BAYERN Munich bado ina matumaini ya kumsajili winga wa Athletic Bilbao na timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams, 22, katika dirisha hili licha ya mchezaji huyo kufikia makubaliano ya kujiunga na Barcelona.
Vigogo wa Bayern wana matumaini kwa sababu wanaamini huenda Barca ikashindwa kulipa gharama za ada ya uhamisho kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Kwa sasa Barca inapambana kuhakikisha inakuwa na pesa za kutosha kukamilisha usajili wa fundi huyu ambaye mwenyewe anatamani sana kujiunga nao ili kucheza pamoja na mastaa wenzake wa timu ya taifa ya Hispania, huku Lamine Yamal akitajwa kuhusika kumshawishi.
Nico amabaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 11.
Marc Guehi
BEKI wa kati wa Crystal Palace, Marc Guehi, mwenye umri wa miaka 24 anayewindwa na Liverpool, yuko tayari kumaliza mwaka wa mwisho wa mkataba wake na timu hiyo na hatolazimisha kuondoka ikiwa hajapata ofa sahihi. Inaelezwa Guehi anataka kubakia kwa mwaka mmoja zaidi akiamini itamsaidia sana katika ukuaji wake kama mchezaji. Liverpool na klabu nyingine kubwa Ulaya zinaiwinda saini ya beki huyu ambaye amekuwa mhimili mkubwa kwa Palace na anaweza akaondoka japo hataki kuharakisha kufanya hivyo.
Rodrygo
MPANGO wa Arsenal kumsajili winga wa Real Madrid, Rodrygo, 24, umekwama kutokana na hitaji la mshahara la staa huyo kuwa kubwa. Ripoti kutoka tovuti ya AS zinaeleza Rodrygo anahitaji mshahara wa Pauni 10.2 milioni kwa mwaka. Mkataba wake wa sasa na Madrid unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Hata hivyo, huenda pia Arsenal ikashindwa kumsajili kutokana na Kocha mpya wa Madrid, Xavi Alonso kuwa na mipango na nyota huyo wa Brazil msimu ujao.
Rasmus Hojlund
NAPOLI imeingia katika vita dhidi ya Inter Milan ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Denmark, Rasmus Hojlund, mwenye umri wa miaka 22. Hojlund ni miongoni mwa mastaa ambao wapo tayari kuondoka Man United kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Napoli inataka straika wa kutupia mabao msimu ujao na inaona nyota huyo ambaye ameshindwa kuonyesha makali Ligi Kuu England licha ya kufanya makubwa Atalanta alikokuwa, atabadilika na kuwa bora ikiwa naye.
Scott McTominay
Al-Hilal ya Saudi Arabia inatamani kumsajili kiungo wa kati wa Napoli, Scott McTominay, 28, lakini inaonekana kuwa ngumu kuipata saini yake kwani Napoli haitaji kumuuza. McTominay ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Napoli, msimu uliopita alicheza mechi 39 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na tangu ajiunge nayo akitokea Manchester United ya England amekuwa mmoja wa nyota muhimu kikosini.
Nicolas Jackson
CHELSEA iko tayari kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa Senegal, Nicolas Jackson, 24, dirisha hili na timu kadhaa kutoka Italia zikiwamo Juventus na Napoli zimeonyesha nia ya kumsajili. Jackson ambaye msimu uliopita alicheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao 13, inadaiwa kuwa kiwango chake hakimridhishi Kocha Enzo Maresca ambaye ametoa ruhusa ya kuuzwa kwake.
Andre Onana
KIPA wa Manchester United Andre Onana, 29, anataka kubaki na kupigania nafasi yake licha ya Monaco kuonesha nia ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon. Ripoti zinaeleza Man United imepanga kusajili kipa katika dirisha hili kwa ajili ya kumpa changamoto Onana ambaye msimu uliopita alionekana kuwa na makosa mengi.
Marcus Rashford
MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Marcus Rashford, 27, bado hajakata tamaa kuhusu dili la kwenda Barcelona licha ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, kuonekana haina tena mpango wa kumsajili. Rashford ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Aston Villa, amewekwa na Barca kama mbadala wa Nico Williams ikiwa wababe hao watashindwa kumpata staa huyo.