Barcola atua Liverpool kwa Sh123 bilioni
Muktasari:
- Akiwa PSG, tayari ameshatwaa mataji matatu ya Ligue 1, Ligi ya Mabingwa mara mbili, Kombe la Ufaransa mara mbili, UEFA Super Cup pamoja na FIFA Intercontinental Cup.
LIVERPOOL imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Bradley Barcola kutoka Paris Saint-Germain (PSG), katika dili lenye thamani ya hadi Pauni123 milioni, (zaidi ya Sh123 bilioni).
Liverpool imelipa Pauni106 milioni kama ada ya awali, huku Pauni nyingine milioni 17 zikitarajiwa kulipwa kupitia bonasi mbalimbali zitakazotegemea mafanikio ya mchezaji huyo.
Awali, PSG ilikuwa imemuweka Barcola kwenye thamani ya Pauni145 milioni, lakini Liverpool imefanikiwa kukamilisha dili hilo kwa kiasi cha chini baada ya mazungumzo marefu.
Barcola, 23, amesaini mkataba wa miaka mitano na kuwa mchezaji mpya wa tano kutua Anfield katika dirisha hili la usajili.
Anajiunga na kikosi hicho baada ya Victor Munoz, Jeremy Jacquet, Ronald Araujo na Ifeanyi Ndukwe, ambao nao wamesajiliwa katika kipindi hiki.
Akizungumza baada ya kukamilisha uhamisho huo, Barcola alisema anafurahia kujiunga na Liverpool na anatamani kuanza kuonyesha uwezo wake uwanjani.
“Ilichukua muda mrefu, lakini nina furaha sana leo kuweza kucheza Liverpool. Ninachotaka ni kuwa uwanjani na kucheza,” alisema.
Barcola alisema moja ya ndoto zake kubwa ni kuisaidia Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.
“Natumaini tutafanikiwa kufanya mambo makubwa sana. Kwanza kabisa, kushinda Ligi Kuu England ni moja ya ndoto zangu kubwa maishani.
“Nataka kufanya hivyo na kubaki katika timu hii kwa muda mrefu. Ndiyo maana nimesaini mkataba mrefu na natumaini nitaweza kutimiza hilo.”
Mshambuliaji huyo ambaye atavaa jezi namba 29 Liverpool, anapendelea kucheza upande wa kushoto wa safu ya ushambuliaji, lakini pia ana uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za mbele.
Ujio wake unatarajiwa kuongeza nguvu na upana katika kikosi cha kocha Andoni Iraola, hasa baada ya kuondoka kwa Mohamed Salah, huku Hugo Ekitike akiwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha na uwezekano wa Cody Gakpo kuondoka ukitajwa.
Barcola alifanya vizuri msimu uliopita akiwa PSG, akifunga mabao 13 na kutoa asisti saba katika mechi 49 alizoicheza kwenye mashindano yote.
Katika Kombe la Dunia 2026, alicheza mechi zote nane za Ufaransa na kufunga mabao matatu, huku Les Bleus wakifika katika mchezo wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu.
Barcola alijiunga na PSG mwaka 2023 akitokea Lyon kwa ada iliyoripotiwa kuwa Pauni milioni 38.5.
Akiwa PSG, tayari ameshatwaa mataji matatu ya Ligue 1, Ligi ya Mabingwa mara mbili, Kombe la Ufaransa mara mbili, UEFA Super Cup pamoja na FIFA Intercontinental Cup.
Ada ambayo Liverpool imelipa pia inahusisha kiasi cha fedha kinachohitajika kulipwa kwa Lyon kama sehemu ya malipo ya mshikamano kutokana na uhamisho wa Barcola kwenda PSG miaka mitatu iliyopita.