Barcelona yatangaza kuachana na Lewandowski
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 alijiunga na Barcelona 2022, na ameichezea klabu hiyo mechi 191, akifunga mabao 119.
SIKU chache baada ya Barcelona kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu Hispania (LaLiga), wamesema mshambuliaji wao Robert Lewandowski ataondoka klabuni mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake wa miaka minne kumalizika.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 alijiunga na Barcelona 2022, na ameichezea klabu hiyo mechi 191, akifunga mabao 119.
Nyota huyo ataondoka akiwa mmoja wa wafungaji bora wa muda wote wa Barcelona akiwa ameshinda mataji matatu ya LaLiga, Super Cup tatu za Hispania pamoja na Copa del Rey.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Jumamosi, kupitia X, uongozi wa Barcelona umeandika: “Alikuja akiwa nyota. Anaondoka akiwa lejendari. Asante Robert Lewandowski kwa kila bao, kila pambano, na kila wakati wa kipekee ukiwa umevaa rangi hizi. Culer milele.”
Lewandowski naye alitoa ujumbe wa kuaga kupitia mitandao ya kijamii, akiwashukuru mashabiki kwa upendo waliompa akiwa mchezaji wa Barca.
Naye nyota huyo wa kimataifa wa Poland aliandika kwenye Instagram: “Baada ya miaka minne iliyojaa changamoto na kazi kubwa, ni wakati wa kusonga mbele.
Ninaondoka nikiwa na hisia kwamba mpango umekamilika. Misimu minne, mataji matatu ya ligi. Sitasahau upendo nilioupokea kutoka kwa mashabiki tangu siku yangu ya kwanza. Catalonia ni nyumbani kwangu duniani. Asante kwa kila mtu niliyepata nafasi ya kukutana naye katika miaka hii minne mizuri. Asante maalumu kwa Rais Laporta kwa kunipa nafasi ya kuishi sura bora zaidi ya maisha yangu ya soka.
Barca imerudi mahali pake panapostahili. Visca el Barça. Visca Catalunya.”
Katika kipindi chake akiwa Barcelona, Lewandowski amefunga mabao 119 katika mashindano yote, huku akitoa asisti 24 kwenye takriban dakika 14,000 alizocheza. Mabao 82 kati ya hayo alifunga LaLiga, huku msimu wake bora ukiwa uliopita ambapo alifunga 27 katika michezo 34 ya ligi.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Lewandowski alifunga mabao 23 katika mechi 38, na kufikisha mabao 100 katika historia ya mashindano hayo akiwa mchezaji wa Barcelona. Kwa upande wa mataji, ataondoka akiwa ametwaa jumla ya mataji saba na kuongeza jingine msimu huu.
Wakati habari za kuondoka kwake zikisambaa, mwenzake Marcus Rashford alimtumia ujumbe wa kumuaga.
Rashford aliandika: “Lejendari! Imekuwa furaha kucheza pamoja nawe. Kutoka kwenye picha za Nike hadi uhalisia.”
Nyota huyo wa Manchester United ambaye yupo Barcelona kwa mkopo, huenda pia akaondoka mwishoni mwa msimu huku mustakabali wake ukiendelea kuwa na sintofahamu. Rashford amekiri wazi kuwa anatamani kubaki Hispania baada ya kufufua kiwango chake akiwa Barcelona.
Hata hivyo, bado hakuna taarifa rasmi kuhusu hatua yake inayofuata licha ya Barcelona kuwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja.
Ripoti zinaeleza kuwa licha ya kutaka kumbakisha mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England, Barcelona hawapo tayari kulipa Pauni 26 milioni zinazohitajika kumchukua jumla bila kwanza kujadili njia nyingine za kifedha.